Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi na mimi leo kuchangia katika taarifa hii ambayo imewasilishwa na Kamati ya LAAC.
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende ku-declare interest ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC. hivyo basi mambo mengi tumeyaona kupitia ukaguzi ambao tumefanya katika muda ambao tuliokuwa tunashiriki hapa Dodoma na Dar es Salaam. Lakini yako mengi tumeyabaini katika Halmashauri zetu nyingi nchini kama siyo asilimia 100 basi asilimia 99 katika usimamizi hazifanyi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu unaweza ukakuta unapata taarifa ya Halmashauri, lakini ukienda kukagua kwa ndani unakuta wamefanya manunuzi yasiyofuata Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004. Wanajifanyia utaratibu ambao wenyewe wanaona unafaa sasa mwisho wa siku ukikaa ukagundua ukachimba kwa ndani unakuta tayari wana-interest labda na yule mtu ambaye anataka kufanya ile kazi ama na mambo mengineyo ambayo yapo katika Halmashauri husika na miradi ambayo wanakuwa wanayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii katika report hizi za Halmashauri ambazo tumezikagua na tumeziona, tunagundua kabisa kwamba kutokana na Halmashauri nyingi nchini kupata fedha katika robo ya mwisho au robo ya tatu ya kumaliza mwaka, wanapata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hali ambayo inapelekea hata wao wenyewe Halmashauri kushindwa kutimiza ama kutokukamilisha ile miradi ambayo wamejiwekea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na shida hiyo, unaikuta Halmashauri inaingia kwenye mgogoro aidha na wananchi ama inaingia mgogoro na Serikali ama inapokuja kukaguliwa na CAG wanajikuta wapo kwenye matatizo ya kwamba aidha zile fedha walikuwa nazo wameshindwa kuzitumia na baadaye zinakuwa ni bakaa na wakati mwingine zile fedha wanaambiwa wazirudishe Hazina, kwa hiyo, mwisho wa siku ile miradi iliyokuwepo iliyotengewa zile fedha miradi haifanyiki kwa wakati na zile fedha zimerudi Hazina.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hali hii kwa utaratibu huu tukiendelea nao kwa namna moja ama nyingine miradi mingi sana itakwama kwa sababu nachukulia mfano hata pale katika Wilaya yetu ya Igunga katika Jimbo la Manonga, yako majengo ambayo wananchi wametoa fedha zao za kuanzisha mfano ujenzi wa zahanati, ujenzi wa nyumba za walimu, ujenzi wa madarasa ya shule, maabara lakini unakuta support wanayotakiwa wapate kutoka kwenye Halmashauri, Halmashauri inaweza ikaandika fedha kuomba kwa ajili ya kumalizia, zile fedha hawapati kwa wakati mwisho wa siku wananchi wanalalamika na sisi Wabunge tukija Bungeni tunalalamika, hali hii inapelekea miradi mingi kukwama na Serikali inapokuja mwaka mwingine wa fedha tunakuja tunaanzisha miradi mipya na tunaenda kuwaambia tena wananchi waanze kuchangia wakati miradi mingine haijafika mwisho, tunaanza kuwaambia wananchi waanze kuchanga tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ukianza kumwambia mwananchi achange nyumba ya mwalimu wakati anaona maabara ile pale haijafika mwisho anaanza kukwambia mfano, mbona maabara ile haijamaliziwa na Serikali ilituambia tuchange fedha ili zile fedha wenyewe watamalizia hawajamalizia, leo tujenge nyumba za walimu. Kwa hiyo, hii inaleta mgongano wa kimaslahi kati ya Halmashauri na wananchi lakini pia Halmashauri na Serikali kuu na wakati mwingine hii miradi ambayo inakuwa inaanza haifiki mwisho hivyo basi niiombe sasa na kuishauri Serikali katika suala zima la upelekaji wa fedha, fedha hizi ziende mapema na haraka zaidi ili kuweza kuonyesha kwamba miradi tuliyokuwa tumeipanga katika Halmashauri inatekelezwa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo tumebaini, Halmashauri nyingi zinakusanya fedha kiholela tu hawatumii EFD machine. Kwa hiyo, kutokana na kutokutumia hizi mashine za EFD inapelekea kukosa mapato makubwa zaidi. Kwa hiyo, niishauri Wizara husika itoe maelekezo kwa Halmashauri zote nchini kwamba watumie EFD machine katika kukusanya mapato yao ya ndani, hiyo yote mpaka katika minada sijui mambo yote wanayofanya vijijini kule. Hii itatupelekea kuongeza mapato yetu katika Halmashauri, lakini itaongeza mapato katika Serikali kuu tukiacha kutumia EFD machine, mapato mengi yatapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tuombe sasa Wizara ilichukulie hili na itoe maelekezo na isiwe ombi kwamba toeni maelekezo muda fulani kuhakikisha kwamba Halmashauri zote nchini mpaka kufikia muda fulani sehemu zote za mapato yenu mtumie EFD machine. Hii itasaidia sana kuhakikisha kwamba Halmashauri zinakuwa na hela, Serikali inakuwa na hela, lakini hata ile miradi tuliyokuwa tumejipangia inaweza kutimizwa kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nipende kuishauri Serikali. Serikali Kuu imetenga fedha mwaka huu asilimia 40 za fedha ziende katika miradi ya maendeleo. Sasa hizi fedha zitakwenda ndiyo lakini huku chini usimamizi wake kama ambavyo tumezungumza, wakati mwingine usimamizi mbovu sasa lazima kuwepo na chombo imara ambacho kitakuwa kinasimamia na kufuatilia na chombo hicho ni chombo ambacho tumekiweka wenyewe kisheria ambayo ni Ofisi ya CAG na kupitia Kamati zetu za LAAC na PAC. Hizi Kamati ndizo jicho la Serikali, lakini ndiyo jicho la Bunge, ndiyo jicho la wananchi kuhakikisha kwamba zile fedha zinazokwenda kwenye Halmashauri zetu zinafanyakazi lazima ukaguzi uwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa zikienda na Ofisi ya CAG ikaenda kukagua, Kamati zikaenda kujiridhisha kuangalia maana yake hata tutakaporudisha Serikalini taarifa maana yake Serikali ichukue taarifa yetu sasa ianze kuifanyia kazi kwamba sehemu fulani wamefanya madudu, sehemu fulani wamefanya madudu. Sasa zinapokosa Kamati hizi fedha kwa ajili ya kufanya shughuli hii ya ukaguzi ama Ofisi ya CAG inapokosa fedha maana yake hata tukipeleka mabilioni ya shilingi kama hamna anayefuatilia maana yake na yenyewe yatapotea, mwisho wa siku maana yake hata yale malengo tuliyokuwa tumejiwekea tutafika 2020 yale malengo yatakuwa hatujayafikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niiombe sana Serikali ihakikishe inawezesha Ofisi ya CAG ipate fedha za kutosha za kukagua. Pia Kamati za PAC na LAAC zipate fedha kwa ajili ya kutembelea miradi, hii itaisadia Serikali ya Magufuli kufikia malengo yake iliyojiwekea kufikia mwaka 2020 kwa sababu itakuwa inajua wapi Halmashauri gani imeharibu, taasisi gani imeharibu na hapo hapo inachukua hatua kuhakikisha kwamba zile fedha wanazozitoa zinafanyiwa kazi ili isiwe kwamba vile maana yake Ofisi ya CAG fedha ilizotengewa ni ndogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama fedha ikiwa ndogo Halmashauri mwaka huu Ofisi ya CAG inafikiria kwamba inaweza isikague hata Manispaa kumi. Sasa kama itashindwa, maana yake taarifa ya mwakani tutakuwa hatuna hapa na kama Ofisi ya CAG ikikosa kufanyakazi maana yake Kamati hizi za PAC, Kamati ya LAAC itakuwa haina cha kufanya, kwa hiyo, mwisho wa siku niishauri Serikali kwamba hizi ofisi zipewe fedha mapema na waharakishe na washirikiane nao bega kwa bega kuhakikisha kwamba tunafanyakazi kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nilikuwa nataka tu kuishauri Serikali hasa kupitia Wizara husika ya TAMISEMI wafuatilie sana hizi Halmashauri. Kuna hizi asilimia kumi ambazo wenzangu wamezungumza za vijana na akina mama. Hizi fedha ni muhimu sana Halmashauri ikatoa, ziko Halmashauri naona zinafanya vizuri, zinatoa fedha kwa ajili ya kutoa kwa vijana na makundi mbalimbali ya kina mama. Hizi fedha zikitoka kwa mfano, kwenye Halmashauri mapato yetu yawe shilingi bilioni mbili maana yake fedha makundi haya iko zaidi ya milioni 200. Milioni 200 ukazichukua milioni 100 ukapeleka vijana, milioni 100 ukapeleka kwa akina mama, hizi fedha zikaenda kwenye makundi haya na kwenye kata husika maana yake mwisho wa siku…
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana muda wangu umekwisha napenda kuunga mkono hoja, ahsante.