Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kutuwasilishia Mpango ambao sisi kama Wabunge tuna wajibu wa Kikatiba wa kutoa maoni yetu ili kuuboresha ili uweze kuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla Mpango ni mzuri sana na kwa kweli nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa sababu yako baadhi ya maeneo ambayo tumekuwa tukiyazungumza sana ameyataja japo si kwa kiwango kikubwa ambacho tungetarajia lakini walau yamezungumzwa. Mojawapo ni suala la uboreshaji na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka kwenye Bunge lililopita tulizungumza sana eneo hili, tulikasirishana sana na moja ya eneo tulilokuwa na wasiwasi ni ujenzi wa reli hii kwa kiwango cha standard gauge kwenye matawi yake yote. Nashukuru kwenye Mpango liko wazi, matawi yote yametajwa Kaliua - Mpanda - Karema - Uvinza - Msongati - Isaka - Keza na sehemu zingine. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, eneo hili ni la muhimu sana, tunakubaliana na yeye na yako maeneo mengi ambayo tunakubaliana. Naamini kwamba tukienda kutekeleza matokeo makubwa tutayapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama taratibu zinavyotaka nifanye, naomba nizungumzie baadhi ya maeneo ambayo naamini yanaweza yakasaidia zaidi kufanya Mpango uweze kuwa na manufaa makubwa kwa wananchi lakini lengo kuu likiwa ni kutusaidia katika kufikisha au kutekeleza ahadi tulizozitoa. Kwenye kitabu cha Mapendekezo ya Mpango ukurasa wa 62 Mheshimwa Waziri ameeleza maeneo ya kipaumbele kwa mwaka 2017/2018. Kwenye maeneo hayo yako baadhi ya maeneo ambayo mimi naamini yalitakiwa yaingizwe na yangefaa yatizamwe kwa upana mkubwa sana. Eneo moja ambalo mimi naona halijaelezwa kwa upana unaostahili ni mchango wa sekta ya kilimo kwa upana wake kama engine ya raw material inayotakiwa kwa ajili ya uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba hauwezi ukajenga viwanda bila malighafi na asilimia zaidi ya 80 ya malighafi zinazohitajika kwenye viwanda zinatoka kwenye sekta ya kilimo. Ili kweli kupata uchumi wa viwanda ni lazima tuangalie maeneo ya sekta ya kilimo na hasa mazao ambayo kwanza yanaajiri watu wengi lakini pili yana multiplier effect kubwa mfano ni zao la pamba. Zao la pamba mwaka 2000 tulizalisha marobota kama milioni moja na laki mbili hivi, uzalishaji wa mwaka jana ilikuwa ni chini ya marobota laki mbili. Kuzalishwa kwa pamba kwa kiwango kidogo namna hiyo kwa lugha rahisi maana yake ni kwamba zao la pamba limeanguka. Kuanguka kwa zao la pamba kunamaanisha wananchi wanaofikia zaidi ya milioni 14, wananchi wanaotoka kwenye Wilaya zaidi ya 42 ambao kwa kiasi kikubwa shughuli zao za kiuchumi zimekuwa zikitegemea pamba hawana shughuli ya kufanya. Iko Mikoa ambayo hauwezi ukapambana na umaskini kwenye mikoa hiyo bila kugusa pamba, mojawapo ni Mkoa wa Shinyanga na Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwenye mpango huu, mkakati maalum wa kufufua sekta ya kilimo utajwe, acha tu kutaja kwa ujumla jumla kwamba kuongeza pembejeo, lakini uwepo mkakati maalum wa kufufua zao la pamba, kujenga viwanda vya mafuta yanayotokana na mbegu za pamba vilevile viwanda vya kusokota nyuzi za pamba na hatimaye kupata nguo. Tukifanya hivyo, tutatoa ajira kwa Watanzania zaidi ya milioni 14 lakini pia tutaondoa umaskini kwa mikoa zaidi na nane ambayo inaishi kwa kutegemea zao la pamba. Kwa hiyo, eneo hili nilidhani ni muhimu Mheshimiwa Waziri akalitizama kwa umakini unaostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni zao la mifugo na hapa kuna tatizo kubwa sana. Hivi sasa tunakisiwa kuwa na ng‟ombe, mbuzi na kondoo zaidi ya milioni 26. Mifugo hii wote tunajua ambavyo imekuwa ni kero kati ya wahifadhi na wakulima kwa upande mmoja pamoja na mifugo yenyewe. Ukiangalia kinachopatikana kutoka kwenye mifugo hii kimsingi ni kama hakihesabiki (negligible). Naiomba sana Wizara hasa Wizara ya Fedha pamoja na Wizara ya Kilimo mkae pamoja muwe na mpango mkubwa pia wa ujenzi wa viwanda vya nyama, ujenzi wa viwanda vya maziwa, ujenzi wa viwanda vya ngozi, tuache hivi viwanda vidogo vidogo ambavyo vimekuwa vikisemwa na rafiki yangu mmoja ametajwa hata hapa Waziri wa Viwanda kwamba anachukulia suala la viwanda ni suala rahisi, ni suala ambalo ni complicated sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani ng‟ombe hawa zaidi ya milioni 25 ambao kwa wastani wa bei ya soko ya shilingi 300,000 kwa ng‟ombe mmoja unazungumzia utajiri wa zaidi ya shilingi trilioni 7.5, ambayo ni karibia theluthi moja ya bajeti yetu ya Serikali, utajiri wa namna hiyo tunauona hauna thamani, wafugaji tunawafukuza kila mahali na kuwaambia warudi walikotoka. Mimi nimekuwa nikihoji sana hiyo lugha ya kusema watoke kwenye hifadhi warudi walikotoka, nikawa najiuliza hivi sisi Watanzania tukiambiwa turudi tulikotoka itakuwaje? Kwa sababu Watanzania tulio wengi wengine wana asili ya Asia, wengine Wabantu wana asili ya Afrika ya Kati na wengine Nilotics wana asili ya Afrika ya Kaskazini, hivi na sisi turudi huko? Ni lazima tujue mifugo ni rasilimali yetu tuiwekee mkakati maaalum mzuri wa kuiendeleza wala si kuiona kwamba ni kero na inawezekana. Kwa hiyo, naomba sana eneo hili la mifugo liweze kutazamwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni la mtawanyiko wa uwekezaji wa kimkakati katika nchi. Kuna eneo ambalo tumezungumzia miradi ya kielelezo na kanda za kiuchumi, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 18. Ukitazama kanda za kiuchumi zilizotajwa za Pwani, Tanga, Dar es Salaam, Mtwara na Kigoma, najiuliza kama kweli tunataka kufanya kanda ya mkakati wa kiuchumi iwe kanda hiyo na huko ndipo pengine tutakoweka uwekezaji mkubwa na biashara kubwa na viwanda, haitawezekana kwa malighafi zitakazotoka katikati ya nchi yetu za mifugo na mazao ya kilimo kuyapeleka kwenda kuchakatwa kwenye viwanda ambavyo vitajengwa maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ukuzaji wa uchumi kwa kanda za kiuchumi za kitaifa ziwe kijiografia kwa kuangalia kila eneo linazalisha nini? Tuwe na makakati maalum wa kuendeleza mifugo kwa hiyo tuwe na kanda maalum ya Dodoma; Kanda ya Mwanza tuwe na mkakati maalum wa kuendeleza madini, kuendeleza kilimo cha pamba na kuendeleza mifugo. Kanda ya Kigoma kule kwa kina Nswazugwako tuwe na mikakati hiyo ya kuendeleza uvuvi wa Lake Tanganyika, mawese na vitu kama hivyo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inatofautiana utajiri wa rasilimali eneo kwa eneo, hauwezi ukategemea chuma cha Liganga kiwe rasilimali kwa kiwanda kitakachojengwa Tanga au kiwanda kitakachojengwa Bagamoyo. Kwa hiyo, ni lazima eneo ambalo rasilimali inapatikana, mifugo inapatika Shinyanga kiwanda cha nyama kijengwe huko na ndiyo huko kuufanya uchumi uweze kugusa Watanzania wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie eneo moja ambalo naona kama linasahaulika la misitu. Uzalishaji wetu na potential yetu kwenye misitu hatuitumii vizuri. Bahati mbaya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili hayupo, nchi ya Finland kwa mfano, uchumi wake zaidi ya Euro bilioni 20 kwa mwaka unatokana na mazao ya misitu. Ardhi wanayolima ni kama hekta milioni mbili, sisi ardhi yetu iliyoko kwenye hifadhi (forest reserves) ni hekta milioni 13 na eneo linalolimwa kwa maana ya forest plantation ni hekta 80,000. Maeneo makubwa ya hizi reserves kwa lugha ambayo anaitumia sasa hivi ndugu yangu Lukuvi kwa wananchi wa kawaida tunaita mashamba pori. Naomba niwafahamishe kama kuna mtu tajiri wa mashamba pori ni Wizara ya Maliasili na Utalii. Maeneo haya yanaitwa hifadhi lakini ukifika ni nyika hakuna miti zilishabaki nyasi na yamebaki maeneo ambayo yanatumika kukusanya rushwa kwa watu wanaokwenda pale kujitafutia riziki, hayana ulinzi wala hayafanyiwi shughuli yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike? Wenzetu wa Finland maeneo haya wametumia PPP, sekta binafsi mnaiita mnaingia concession, wanalima miti kwenye maeneo hayo, Serikali inapata kipato fulani na wale wawekezaji wanapata. Kwa mfano, sisi mahitaji yetu ya mbao ni zaidi ya cubic meter milioni 40. Sasa hivi uzalishaji wetu ni cubic meter 450,000. Soko la mbao la Kenya, soko la mbao la Djibouti, South Sudan, Ethiopia mpaka Muscat wanasomba mbao na wananunua mbao kutoka Tanzania. Uwepo wetu hapa kijiografia na kuzungukwa na nchi ambazo hazina ardhi ya kutosha, Kenya hawana ardhi ya kutosha, Somalia wana vita na maeneo mengine ni jangwa, kwa hiyo tukitumia ardhi yetu ambayo tayari tunayo, naamini tunaweza kabisa kwa export ya mazao ya misitu na revenue ya kutoka kwenye mazao ya misitu kwa commercial plantation kwa kutumia sekta binafsi kuwa zaidi ya dola za Kimarekani angalau bilioni 20 ambayo ni zaidi ya trilioni 40 ambayo ndiyo bajeti ya Serikali. Tukiwa na mkakati wa namna hiyo kwa miaka 20, 25 kule mbele naamini sekta hii inaweza ikatoa mchango mkubwa sana kwa uchumi wa nchi yetu. Naamini kabisa kwamba tukiyatazama mambo haya kwa upana unaostahili kwa kiwango hicho, tunaweza tukaitoa nchi yetu kutoka hapo ilipo kwenda mbali zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kuna eneo ambalo tunazungumzia kuangalia upya mikataba ili iweze kuwa na tija kwenye uchumi na kwa wananchi na hasa mikataba inayohusu kodi. Kwenye sekta ya madini kuna mikataba ambayo ilikwishakuwekwa inayozuia Halmashauri zisitoze ushuru wa huduma na mikataba hiyo imefanya Halmashauri zisiwe zinanufaika pamoja na mabadiliko mazuri sana aliyofanya Mheshimiwa Profesa Muhongo. Kwa mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala inadai zaidi ya shilingi bilioni 14 kutokana na malimbikizo ya ushuru wa huduma ambao imekuwa hailipwi kwa sababu mkataba ulifungwa kwamba ilipwe dola 200,000 wakati proper service levy ya 0.3% ni zaidi ya dola za Kimarekani milioni 1.8 kwa mwaka. Kwa hiyo, mnafungiwa mkataba wa kulipa dola 200,000 wakati sheria inasema mlipwe over and above 1.8 million dollar. Kwa hiyo, naomba mambo tuliyokwisha kuyaanza ya kuzungumza ili kurekebisha…
MWENYEKITI: Ahsante.