Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Sophia Mattayo Simba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SOPHIA M. SIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kukushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia mchana huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya ya kuweza kuwa mmojawapo wa kuchangia bajeti hii ya mwanzo kabisa, bajeti ambayo inakwenda kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 mpaka 2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa jinsi anavyofanya kazi nzuri katika kutekeleza hii Ilani, lakini katika kutekeleza yale aliyosema mabadiliko ya kweli. Ni kweli, Mheshimiwa Rais tunaona katika bajeti hii ni vipi mabadiliko ya kweli yanaweza yakapatikana. Hongera sana Mheshimiwa wetu, tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu uendelee kuwa na nguvu ya kutusimamia na hivyo kuleta maisha bora kwa Watanzania wengi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nachukua nafasi hii pia, kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi nzuri waliyoifanya. Pia nakupongeza wewe Mheshimiwa Naibu Spika kwa jinsi unavyoendesha Bunge lako kwa busara, kwa umakini na kwa jinsi unavyohakikisha unaleta nidhamu ndani ya Bunge hili, ukitumia weledi wako mkubwa wa kutafsiri Kanuni za Bunge tulizojiwekea wenyewe. Hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla bajeti ni nzuri, lakini inahitaji sana Watanzania tubadilike, tunahitaji discipline ya hali ya juu katika ukusanyaji na katika utumiaji wa fedha hizo. Sisi kama Waheshimiwa Wabunge, tupo pamoja na Rais wetu, tunakubalina naye kwamba tutabana matumizi kama tulivyoanza na pia tutahakikisha huko Majimboni kwetu kila mtu anafanya kazi. Kabla sijaendelea naomba niunge mkono hoja mia kwa mia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niwapongeze sana Kamati ya Bunge ya Bajeti kwa kazi nzuri waliyofanya. Nawapongeza sana wadau wangu akinamama nadhani wanne au watano, wamefanya kazi kwa umahiri mkubwa sana. Pia nawapongeza na akinababa ambao walikuwanao, lakini walionesha umahiri wao kwa vile wamesheheni weledi katika taaluma zao na wanazielewa vizuri, kwa hiyo, nawapongeza sana. Kwangu mimi nikiwa Mwenyekiti wao, I am proud of them, wamefanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kazi hiyo, moja ambalo limenifanya niwapongeze ni pale walipogundua lile tatizo kubwa ambalo wameliona na wamepeleka mapendekezo, ingawa sijui kama yamechukuliwa katika ukurasa wa 11. Moja ya pendekezo lao ni lile walilosema, ziongezwe shilingi bilioni 30 kwenye bajeti ili kumaliza zile Zahanati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo zahanati ambazo wananchi wamejitolea kujenga. Nilipokuwa nikitembea mikoani wakati wa kampeni kilio kikubwa walichonacho akinamama, walikuwa wanasema, unaona boma lile, ndiyo Zahanati yetu, haijakwisha. Hivyo basi, kama hatukuwasaidia hawa katika hizi zahanati, kwanza tunawavunja moyo wa kujitolea, lakini kubwa zaidi akinamama wanaendelea kufa kutokana na kukosa huduma za afya. Baya zaidi, vipo pia Vituo vya Afya ambavyo vimejengwa vizuri, lakini havina vyumba vya upasuaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbona saa inaenda upesi! (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini fedha hizi zingesaidia sana katika kutengeneza hizo theater ili tupunguze vifo vya akinamama. Pia, waliozungumzia kuongeza tozo ile ya senti 50 kuwa sh. 100/= kwa ajili ya Mfuko wa Maji. Nawaunga mkono mia kwa mia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naona muda wenyewe siyo rafiki, lakini napenda niwapongeze sana kwa jinsi walivyotenga pesa ya kutosha kwenye miradi ya maji. Nashukuru sana kama pia wangetenga pesa ya kutosha kwenye miradi ya mazingira. Kazi yote tunayoifanya kwenye maji haitakuwa na maana kama mazingira yetu yanaendelea kama yalivyo. Tunahitaji kuwe na Mfuko wa Mazingira uweze kupanda miti mingi sana. Kwa hiyo, hilo naomba liishie hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia Mheshimiwa Waziri afafanue, kuna uwoga ndani ya jamii kuhusu huu ushuru wa simu pamoja na benki; hizi ada. Wananchi na sisi wenyewe tuna wasiwasi; mzigo usije ukarudi kwa wananchi. Hali siyo nzuri. Wananchi hawana hali nzuri ya kifedha, pesa imepotea; sasa tusiwaongezee tena matatizo katika masuala ya simu. Hata mkisema watakaolipa ni wale wenye Makampuni ya Simu, lakini mwisho wa siku hawa ni wafanyabiashara, watatafuta ujanja zitarudi kwetu tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kuhusu shilingi milioni 50. Mimi na wenzangu ambao wako humu tulikuwemo katika kutengeneza ile Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Nataka nitanabahishe, tuelewe. Tuliposema vijiji 50 tulikuwa na maana ya Vijiji, Mitaa na Shehia. Kwa hiyo, kwa sababu kila mtu anazungumzia vijiji, wale kule mitaani wanaweza kudhania hawamo. Wamo! Hata hivyo, nawapongeza sana kwa utaratibu mliouchukua wa kufanya kwanza pilot project ya mikoa 10. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi shilingi milioni 50 tulisema zitakuwa revolving fund katika kile kijiji, hazitoki. Kwa hiyo, leo wanapata hawa, kesho wale, ni za kijiji, hazi-revolve kutoka nje. Kwa hiyo, hilo likumbukwe, nia yetu ilikuwa hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, gratuity kwa Waheshimiwa Wabunge kutozwa kodi siyo sahihi. Zile sababu zilizosababisha kusamehewa, bado zipo mpaka leo. Warudi kwenye makabrasha yao wasome, zile sababu zimekwisha? Ahsante.