Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Stephen Hillary Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kupitia Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ambayo ameionesha kwa muda mfupi ambao ameingia madarakani. Nataka tuwaambie kwamba hatutawaangusha, tutawaunga mkono kwa dhati.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa mambo ambayo yameongelewa juzi pamoja na Waziri, ameongelea sana kwamba ataimarisha Bandari na Viwanja vya Ndege na ataimarisha Reli. Nimeshangaa sana katika mambo ya kuimarisha reli yeye anaizungumzia tu reli ya kutoka Dar es Salaam mpaka nyumbani kwake Kigoma, hajawahi kuitaja reli ya Tanga – Moshi - Arusha mpaka Musoma. Hapa pana tatizo gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati uliopita nilizungumzia sana suala la reli, nikazungumzia suna kama tunataka kuimarisha biashara ni lazima muiangalie reli ya Tanga. Reli ya Tanga kutoka Tanga kupitia Moshi kwenda Arusha mpaka Musoma ingesaidia sana katika uchumi wa nchi yetu. Nashangaa rafiki yangu ambaye ni Dkt. wangu Mpango, ameangalia sana reli inayokwenda nyumbani kwake ameisahahu ile ya Tanga. Naomba atakapojumuisha aiangalie hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, ni suala la Mkaguzi Mkuu. Kiwango cha pesa ambacho amemtengea, Serikali hapa hamuwezi kwenda kila mahali kukagua na mkapata wale mafisadi, lazima Mkaguzi Mkuu wa Serikali awakagulie, awaambie huyu ndiye fisadi, anatakiwa kupelekwa Mahakamani, leo mnapowapunguzia pesa watakwenda kukagua hiyo miradi na nini? Naomba Serikali iliangalie sana suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, wamepunguza bei ya mafuta ya petroli kwamba bei ya mafuta ya petroli imeachwa kama ilivyo, naomba Serikali ipandishe kwa sababu bei ya petroli haimsaidii Mtanzania, maana kupunguza bei ya mafuta maana yake ni kwamba wasafiri wapunguziwe gharama, lakini toka wamepunguza bei ya petroli hakuna Mtanzania yeyote ambaye anapanda nauli kwenye gari kwa kupunguziwa gharama.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa waiongeze, tujue kabisa kwamba kwa sababu hatufaidiki lolote Watanzania wa hali ya chini. Kwa hiyo, kwa sababu ni kitu muhimu na wameona kwamba ni vizuri, basi tunaomba wapandishe petroli, watupunguzie sukari. Sukari hawajaiongelea hapa, lakini sukari ni kitu muhimu sana kwa Watanzania. Naomba hiyo Mheshimiwa rafiki yangu Waziri wa Mipango, Mpango yeye ni rafiki yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maji ni muhimu sana na barabara; wamezungumzia masuala ya barabara kuna mikoa wameshaanza kuionesha kwamba ni mikoa matajiri sana, lakini mbona wanashindwa kuwaambia hii mikoa maskini kama mikoa ambayo wamenyima hata kuwatengenezea Bandari, mtawapa kiwango kiasi gani kwa sababu tuna bandari ya Tanga pale, tuna Bandari ya Mtwara pale, tuna Bandari ya Bagamoyo, katika Mpango walisema hizi Bandari wataziongeza lakini hatuoni chochote kinachoendelea eti Tanga kwa sababu kunajengwa bomba la mafuta kutoka Uganda ndiyo isahaulike? Haikubaliki!
Hili bomba la mafuta linakuja kwa ajili ya nchi mbili! Haliji kwa ajili ya Tanga! Kama Tanga linakuja ni kama bandari nyingine. Naomba hapa iongezewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Kambi ya Mbadala, tunazungumzia suala hili kwa masikitiko makubwa. Kwa niaba ya Kambi Mbadala, wenzetu wa Kambi ya Upinzani walisema kwamba sitting za Wabunge zifutwe, nasi tunasema hata per diem pia zifutwe kama tunataka kuisaidia Serikali, si Waheshimiwa Wabunge wote tulikuja kwa ajili ya kuwatetea wanyonge? Kama tumekuja kwa ajili ya kuwatetea wanyonge, wenzetu wamesema sitting mwondoe, sisi Kambi Mbadala tunasema hivi, hata ile per diem inayotegemewa na hawa, kama kweli tumekuja kuwasaidia watu, zote ziondolewe ziende kwa maendeleo ya wananchi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo ni uti wa mgongo sana, lakini kwangu kulitakiwa kujengwe bwawa la maji toka miaka ya nyuma sana. Bwawa hili lilikuwa linagharimu shilingi bilioni 13, lakini fedha zile ziliondoka zikaenda Kilimanjaro. Sasa hii bwawa ambalo lilikuwa lijengwe katika Jimbo langu; mmesema safari hii ni wakati wa kilimo, naomba hili bwawa liendelee kujengwa pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni viwanda. Katika Tanzania, mikoa ambayo ilikuwa inaongoza kwa kuwa na viwanda vingi ni mikoa mitatu au minne. Ni Mkoa wa Dar es Salaam, Morogoro, Tanga na Arusha. Hebu niambieni leo, tunazungumzia viwanda. Rafiki yangu Waziri wa Viwanda, best wangu hapa ana hakika kabisa kwamba atafanya; hela za kuanzia hivyo viwanda zitapatikana wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, Serikali yangu sikivu, nampenda sana Mheshimiwa Dkt. Pombe Magufuli na Mawaziri mlioko hapa, mnafanya kazi kubwa sana kwa kujituma na hata leo tutamwombea dua Naibu Spika ili aendelee kukaa mpaka Bunge la mwaka 2020 kwenye jukwaa lile pale. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema haya kwa sababu tuna uchungu. Sisi tunaotoka kule Majimbo tunapokuja hapa, tunaonekana kama Waswahili. Mnaposema kwamba maendeleo yanakwenda vijijini, mtuambie maendeleo haya ni ya namna gani, siyo kusoma vitabu. Leo hii hakuna dawa mahospitalini, hakuna elimu ya kutosha, Walimu wanadai haki zao hawapewi, Madaktari hospitalini hawaongezewi posho; leo tunasema kwamba tunataka kufanya mambo, hebu tumalize haya madeni tunayodaiwa na watu ambao tunawatumia muda mwingi mpaka wakati wa uchaguzi hawa ndiyo tunaowatumia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama tunawatumia watu mpaka wakati wa uchaguzi tunawapenda, leo hii madeni yao hatuwalipi, eti tunategemea tu kukaa; inakuwa siyo nzuri. Naomba kabisa Mheshimiwa tuanze na madeni ya ndani. Tukishamaliza madeni ya ndani tutakuwa tumefanya kazi za msingi sana kwa wananchi, Watanzania ambao wanaipenda sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Ukimwona mtu anaipinga Serikali ya Chama cha Mapinduzi, basi ujue ni fisadi. Ukimwona mtu yeyote leo anakuja kulalamika kwa bajeti yenu, ni fisadi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii Mahakama naomba muianzishe mapema, kwa sababu tumechoka kuonekana Wabunge…
TAARIFA.......
MHE. STEVEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei, mimi sio Kambi ya Upinzani. Mimi ni mmoja kati ya Wabunge wa CCM ambao tumekuja hapa kuweka chachu ya michango yetu kufuatana na hawa wenzetu waliokimbia eneo hili. Kwa hiyo, mimi bado ni Mbunge wa CCM, hiyo taarifa yake siisikii. Ninaposema Kambi Mbadala ni kambi ambayo imekamilika kwa ajili ya kujenga hoja za msingi ya kuisaidia Serikali yetu. Sisi sio Upinzani, kwa hiyo taarifa yake siikubali.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya haya, nimeipenda sana bajeti hii, naiunga mkono kwa asilimia mia moja, siungi mkono taarifa yake huyo.