Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, na kabla sijafika mbali Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango naomba masuala mawili haya ambayo kwenye hotuba yako hujayazingatia nipate ufafanuzi; sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, kuna ushuru na tozo mbalimbali ambazo toka Bunge lililopita tunapiga kelele kwamba wakulima katika sekta hiyo hawatafika mbali kwa sababu ya ushuru na tozo ambazo hazina tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, na kwenye hotuba yako hapa umebaki tu kutaja kwamba kuna hizo changamoto, lakini hujatuletea hizo sheria mbalimbali kwa ajili ya kuzifuta ili wakulima waweze kuifanya Tanzania yetu kuwa nchi ya viwanda. Na wewe Mheshimiwa Mwijage hivyo viwanda unavyovihubiri havitakuwepo kama sekta hii ya kilimo tunafanya nayo mzaha wa namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni suala la maji. Maji vijijini tulitenga Shilingi 50 kila lita ya mafuta ya petrol na diesel kuanzia Bunge lililopita kuwekwa kwenye mfuko wa maji, lakini zile fedha zikapelekwa maji mjini matokeo yake mpaka leo vijijini bado kunashida ya maji. Wabunge hapa tulisema na tukashauri tuongeze kutoka shilingi 50 kwenda shilingi 100, lakini kwenye hotuba yako ya bajeti unasema itabaki hivyo hivyo shilingi 50. Tunaomba tuweke shilingi 50 kwenye mafuta ili tuweze kuwa na mfuko mzuri wa maji vijijini; na hakutakuwa na mfumuko wa bei. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, John Pombe Maghufuli, kwa juhudi zake anazozifanya za kutumbua majipu katika nchi yetu na nimshukuru kwamba analeta Mahakama ya Mafisadi na zile rushwa kubwa za manyangumi. Lakini juhudi hizi za Mheshimiwa Rais, hatazifikisha mwakani endapo atabaki peke yake mtumbua majibu wakati mtambua na mbaini majipu ambaye ni CAG ataendelea kuwa na fedha shilingi bilioni nne katika bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo cha kupunguza bajeti ya CAG ambapo mwaka jana alikuwa na shilingi bilioni 74; wakati fedha za miradi ya maendeleo zilikuwa ni kidogo kuliko mwaka huu, tuna trilioni 11 halafu ndipo mnampa shilingi bilioni 44. Hii ni dalili kwamba bajeti hii inataka kukumbatia mafisadi kwa sababu CAG ndiye anayekagua miradi na mikataba ambayo ni ya kifisadi. Kitendo cha kuminya Ofisi ya CAG, nakuambia Mheshimiwa Waziri Mpango, utumbuaji wa majibu utaishia mwaka huu; Rais hatakuwa na majipu ya kutumbua tena kama bajeti ya CAG haitaongezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi niseme bayana, hata hawa watumishi hewa ambao sasa wanatumbuliwa, juhudi kubwa zilifanywa na CAG Bunge lililopita akawa anabaini watumishi hewa, miradi hii ambayo mingine tunapigwa kwenye barabara na sasa tunapeleka asilimia 40 kwenye miradi ya maendeleo, kama CAG ofisi yake itaminywa haya majipu yakifisadi nani atayabaini na hizi fedha mnazosema mnawezesha TAKUKURU; TAKUKURU atawachunguza mafisadi gani ambao hawajabainiwa na CAG?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwangu mimi bila kumwongeza fedha CAG ambaye ndio jicho, ambaye ndiye ameikomboa nchi hii kwa kubaini mafisadi, nakuhakikishia Mheshimiwa Rais wetu, mwakani hatakuwa hata na kijipu uchungu; hata kipele cha kuweze kutumbua, kwa sababu CAG atakuwa hajafanya kazi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye hii hoja iliyowasilishwa na Mheshimiwa Mpango ya kuondoa msamaha kwenye mafao ya Wabunge. Mheshimiwa Mpango naomba nikuulize, hawa Wabunge ambao unaondoa msamaha kwenye mafao yao unajua kwamba hawana pensheni? Unajua kwamba Wabunge hawa sio pensionable?
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge sisi hufanya kazi yetu miaka mitano tu hapa, hatuna pension, matokeo yake tunaambulia hicho kidogo; fedha nyingine ni nauli, mizigo, vifedha vingine ndio vile ambavyo tumevidunduliza kwenye mshahara tunawekewa kila mwezi. Sasa wewe unataka kuondoa msamaha. Nataka nikuhakikishie kuanzia utawala Mkapa, Wabunge walikuwa wanaomba hata watumishi wengine mafao yao yasije yakakatwa kodi kwa sababu wamefanya kazi miaka 30, 40 watumishi wanakatwa fedha, wanaenda wengine wanakufa kesho yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tumefika pazuri baada ya kuondoa kundi la Wabunge. Tulitarajia katika Bajeti hii sasa unatuletea sheria ya kwenda hata kufuta hizo kodi za mafao ya watumishi wengine Serikalini, sasa matokeo yake unatuletea tena kufuta za Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge ninyi ni mashahidi, akiwepo Mheshimiwa Makinda hapa alisema amechoka kusumbuliwa Wabunge ambao walishastaafu wamekuwa wakija ofisini wanamwomba hela, wamekuwa ombaomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge leo maslahi yetu tumedunduliziwa na kila mwezi tunakatwa kodi ya mapato halafu tena mafao yetu ambayo yamelimbikizwa na yenyewe yakakatwe kodi mnataka turudi mtaani halafu muanze tena kutucheka. Lazima Wabunge tulinde maslahi yetu, Mheshimiwa Waziri usicheze na maslahi yetu, lazima tulinde maslahi yetu. Hatuwezi kukubali fedha ambazo sisi kila mwezi tunakatwa kodi Pay as You Earn na nyingine ile tunawekewa pale halafu baada ya kutoka hapa uanze tena kututoza kodi. Waheshimiwa Wabunge tusikubali sisi hatuna pensheni lazima kodi hii isiwekwe kwenye fedha za Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nimwambie Mheshimiwa Waziri Mpango, sisi Wabunge mshahara wetu ni mdogo sana kuliko wa kwako, wewe mshahara wako ni mkubwa. Sisi Wabunge kule mtaani ndio ATM hata sasa hivi humu kila simu ya Mbunge sijui kuna msiba wapi, kuna kisima kimeharibika, kuna darasa upepo umeezua, ndipo hapo hapo tunapotoa pesa. Halafu Mheshimiwa Mpango unataka kucheza na maslahi ya Mbunge na wewe hapo ulipo wewe Jimbo lako ni Mheshimiwa Rais, sisi Jimbo letu ni wananchi kule. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukiomba fedha hata za kukarabati chuma kidogo tu kwenye pampu ya maji kutoka Halmashauri unaambiwa wewe Mbunge saidia. Tunaomba Halmashauri kuna kadaraja pale kamekatika kidogo pelekeni fedha wanasema kazi ya Mbunge, kazi ya mwenge. Halafu leo hata hicho kidogo na ndiyo maana unanikumbusha lile tangazo kwenye TV walikuwa wameweka kakuku pale linakuja lile kama fisadi mara ya kwanza likakata robo tatu ya kuku haaam! Halafu kakabaki karobo likamalizia tena haamm! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mpango asitupeleke huko, fedha zetu ni kidogo sana matokeo yake unaanza kuzikwangua tena, je, tutakapofika mwakani utakuja tena na ajenda gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtu wa CHADEMA hapa alikuwa anawasilisha bajeti hapa nikaona mhh! Huyu ndiye Silinde kweli? Anashabikia kwamba eti na sisi tunaunga mkono hii kodi wakatwe.
Mheshimiwa Mpango wewe ni mchumi kuna kitu kinaitwa free rider problem, huyu pamoja na kuipiga panga kwamba haitaki wanajua sisi tukiitetea na wao pia watapata free rider problem. Asidanganye wananchi hapa UKAWA wata-enjoy free rider problem baada ya sisi kuitetea na wewe ni mchumi unajua maana ya free rider problem, hatutakubali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, anazungumzia masuala ya sitting allowance, leo, mimi nadhani alikuwa anachomekea tu kwa sababu wana ugomvi na mama yetu pale wanachomekea chomekea vitu na sisi hivi vitu vya kuchomekea hivi mama wala usiwe na wasi wasi wewe ndiye Naibu Spika na wao walikuchagua na sisi tumekuchagua hicho kiti utakikalia mpaka wewe mwenyewe utakaposema sasa basi. (Makofi)
Mheshimiwa Mpango utakapokuja kutoa majumuisho fedha hizi za CAG bila kupanda na bila kutoa kauli hapa kwamba hicho ulichojaribu cha kutu-beep juu ya maslahi yetu hatutaelewana. Na ninashukuru umetu-beep na sisi tumeamua kukupigia. Tunakwenda wapi? Na watumishi wengine wote wale tulishasema fedha zao zile msizikate kodi zile.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.