Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Dua William Nkurua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. WILLIAM D. NKURUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuongea katika Bunge lako Tukufu. Daima nitaendelea kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wa Jimbo la Nanyumbu kwa maamuzi yao ya busara yaliyosababisha mimi kuwa Mbunge wao na hatimaye ndiye mwakilishi wao katika jengo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze kwa kumshukuru sana Mwenyenzi Mungu kwa kuzaliwa nchi hii ya Tanzania, ninamshukuru sana Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ni nchi ambayo Mungu aliipendelea na bado natafiti kwa nini tumependelewa hivi sijapata jibu. Nchi hii ina vivutio vikubwa duniani, sisi ni miongoni mwa watu tunaomiliki Mlima Kilimanjaro, unasifiwa kwamba ni wa pili duniani au wa kwanza Afrika, upo Tanzania lakini Tanzania hii ndio nchi ya pili duniani kuwa na vivutio vingi sana, lakini pamoja na hayo yote tukiacha mambo mengine kama Tanzanite na mambo mengine ambayo Tanzania anamiliki peke yake, dunia nzima anayo Tanzania peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mpaka sasa kwa kweli lazima tukiri hatujajipanga vizuri kutumia vitu hivi ambavyo Mungu ametupatia. Pamoja na hayo ambayo yanatajwa Wizara hii ndio ambayo kama tungeitumia vizuri, wataalam wetu wangejipanga vizuri ni Wizara ambayo ingeweza kupatia nchi hii fedha nyingi ambazo malalamiko mbalimbali ya barabara, hospitali na mambo mengine, tungeweza kutumia Wizara hii kutafuta hizo fedha na hatimaye Watanzania wakanufaika na huduma mbalimbali katika ukusanyaji wa fedha kupita Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukizungumza ukweli bado hatujakaa vizuri. Sasa kama walivyotangulia wengine kwamba Mheshimiwa Maghembe ndiyo ameanza kubeba huu mzigo, lakini hapa tutazungumza mapungufu mengi ambayo tumeona yamejitokeza kule nyuma. Mimi ni miongoni mwa watu wanaosema tunakushauri, tutakuangalia baadaye, lakini tunakushauri na utusikilize vizuri, kwa sababu kama hutatuelewa sisi nafikiri na sisi hatutakuelewa mbele ya safari, itatulazimu tuwe hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitaanza kushauri Wizara hii katika eneo la kutengeneza Watanzania kupenda mazingira hasa ya hifadhi na mbuga za wanyama. Wizara yako ina jukumu kubwa la kuwafanya watu wapende mbuga za wanyama, wapende hifadhi. Watapenda baada ya kuona matunda mazuri yanayotokana na hilo. Binadamu ameumbwa kupenda mazuri na kuchukia mabaya, ukimfanyia jambo zuri mwanadamu anafurahi, ukimfanyia vibaya anakasirika ndio binadamu wa kawaida, na Watanzania wengi wako hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa watu wote ambao wamezunguka hifadhi kwa kweli wao wanajiona wako katika eneo la balaa sana. Kwa sababu mateso wanayopata wale ambao wamezunguka hifadhi ni makubwa mno utafikiri Serikali haipo. Kwa mfano, kwenye Jimbo langu na Nanyumbu tuna hifadhi tunaita Lukwika – Lumesule. Hifadhi ile kila siku inakuwa yaani mipaka tunayoifahamu sisi inaongezeka. Wananchi wamepanda mazao yao lakini unashangaa unaambiwa hifadhi sasa inafika hapa. Sasa wananchi automatically wanaichukia hifadhi hata kama utawaambia kitu gani wanaichukia kwa sababu hifadhi inaongezeka siku hadi siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri akitembelea kwenye Jimbo langu kwenye Kata ya Lumesule, Kata ya Napacho kwenye vijiji vya Napacho vyenyewe, Kijiji cha Mitonga na kwa ujumla ile Kata vijiji vyake wao wamezunguka hifadhi, lakini hifadhi imekwenda kukata mikorosho na kuwaambia kwamba ninyi mpo ndani ya hifadhi. Wananchi wale wanaichukia hifadhi na wanaona kwamba kuwa karibu na hifadhi ni kero. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri, hakikisha kwamba mgogoro huu ambao upo kwenye Kata ya Napacho unaondolewa ili wananchi wapende hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye Kata ya Mkonona, kijiji cha Marumba na vitongoji vyake vya Namunda na Namaromba, kijiji kimesajiliwa, kina shule ya msingi, kina zahanati, kina barabara, kijiji kipo tangu Uhuru, leo wanaambiwa wapo ndani ya hifadhi. Sasa kama Serikali watu hawa imewapa miundombinu hii wamekaa hapo, watu wamehamia pale wamejenga majumba yao wanaambiwa leo wapo ndani ya hifadhi, wananchi hao wanaishi kwa mashaka. Tunawafanya watu wajisikie vibaya ndani ya nchi yao, unategemea wananchi watapenda hifadhi? Nakuomba sana Waziri, mimi nina matumaini makubwa unaweza kubadilisha hii hali. Twendeni tuwaache hawa watu waishi katika nchi yao vizuri, kama tulizubaa sisi Serikali tukawaachia watu wakae mudu mrefu ni kosa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kama tuna uwezo tutume watu wakatathimini pale walipwe fedha waondoke kama tuna uwezo, kwa sababu wananchi wako pale hawakuambiwa chochote, wamepewa Hati, kupewa Hati maana yake ni sehemu sahihi na salama kuishi. Leo unawaambiwa iko ndani ya hifadhi, huu ni unyanyasaji, kwa hiyo lazima tutengeneze mazingira rafiki na wanachi. Hilo Mheshimiwa Waziri ni eneo la kwanza ambalo nimetaka nishauri na naomba tulizingatie.
Mheshimiwa Menyekiti, eneo la pili tuwe na utaratibu mzuri wa kutoa ahadi zinazotekelezeka. Kwa mfano Wilaya ya Nanyumbu kwenye Kata hii ya Napacho kipindi hiki tarehe 8/08/2011 alitembelea Waziri wa Maliasili na Utalii kipindi hicho Mheshimiwa Ezekiel Maige. Alikwenda kijiji cha Chimika na Masuguru, alikuta pale wananchi wana shida kubwa ya maji, na shida aliyoiona kipindi kile mwenyewe akaahidi kutoa shilingi milioni sita Chimika na kutoa shilingi milioni sita Masuguru ili Halmashauri iongeze fedha nyingine wananchi wale wapatiwe maji kwa sababu na wao wamezunguka hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea Mpaka leo fedha hiyo haijalipwa, Halmashauri imeandika barua nyingi hazina majibu. Sasa wananchi unapowaambia kuwa karibu na hifadhi kuna manufaa ya kuweza kupatia miradi mbalimbali na kutatua kero hawaoni.Yote haya yanasababisha wananchi wachukie hifadhi.
Ninaamini uongozi mpya wa Mheshimiwa Profesa Maghembe tutaondoa tatizo hili na hatimaye wananchi wataona faida ya kuzunguka hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuchangia eneo la utoaji wa adhabu kali kwa watu ambao wanapatikana katika maeneo ya hifadhi. Kwanza na mimi nataka niwe mmojawapo ninayekiri kwamba sipendi watu waingilie maeneo ya hifadhi, maeneo haya tumeyatunza kwa ajili yetu sisi na vizazi vinavyokuja ili Watanzania baadaye waweze kurithi huu utajiri ambao Tanzania tunao. Lakini wale watu ambao wamepata haya matatizo wameingia kule na wakaweza kushikwa wakadhibitiwa basi wapelekwe kwenye vyombo vya sheria wakapate hukumu stahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotokea wananchi wanapigwa afadhali nyoka, yaani nyoka huyu mnayemfahamu ananafuu anavyopigwa kuliko anayeshikwa kule. Lakini siku zote Serikali inatangaza kwamba tuwaambie wananchi wasichukue sheria mkononi, wale wanaopigwa njiani, barabarani? Mtu anashikwa ndani ya hifadhi analetwa mpaka kijijini anapigwa anaburuzwa, hii sio sheria mkononi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mimi napowakemea wananchi jamani acheni tabia, mkimkamata mwizi msimpige, mpelekeni mahakama. Wanauliza Maliasili wakitukamata sisi mbona wanatupiga hovyo mbona hawatupeleki mahakamani? Unajibu kitu gani hapo? Mheshimiwa Waziri, una uwezo wa kuthibiti hili ondoa, askari wetu wasitumie sheria mkononi, tunajenga tabia mbaya kwa Watanzania na wao watatumia sheria mkononi, tusiwalaumu kama sisi wenyewe tunawafundisha hii tabia.
Naomba sana Mheshimiwa Waziri hii mizigo ambayo imeikuta jaribu kuiondoa na nina uhakika utakuwa na uwezo wa kuiondoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa mwisho nilitaka nijielekeze katika kuiomba Serikali kutotumia nguvu za ziada hasa kwa maeneo mengine ambayo inatia aibu. Wilaya yangu sio ya ufugaji, kwa hiyo tatizo langu tu kidogo lipo la migogoro ya wafugaji wachache waliokuja kwenye Wilaya yangu hasa kwenye Kata ya Masuguru, lakini maeneo mengi Waheshimiwa Wabunge wamelalamika humu kwamba askari wanapiga risasi ng‟ombe. Hii inaleta aibu kwa nchi yetu….
MWENYEKITI: Ahsante