Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Mendard Lutengano Kigola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru sana kwa kunipa nafasi nichangie. Nami natoa pongezi sana kwa Waziri Muhongo kwa kazi nzuri aliyoifanya mwaka uliopita. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba tena amerudi kwenye Wizara hii muhimu. Wabunge wengi sana wakisimama wanaomba umeme vijijini na tuna matumaini makubwa sana kwenye Awamu hii ya Tatu vijiji vile ambavyo vilikuwa vimebaki kwamba vitapewa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naishukuru Serikali kwa kutoa ile service charge kwa sababu ilikuwa ina-discourage sana wananchi, lakini Serikali ilitangaza kwamba imetoa service charge kwa hiyo, wananchi saa hizi nadhani hata bei ya umeme imeshuka sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nashukuru sana kwa kupunguza gharama za umeme hasa kwenye installation kwenye nyumba zetu. Hii italeta nafuu sana wananchi waweze kuingiza umeme kwa urahisi kwenye nyumba zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni masuala ya gesi. Naiomba Serikali, gesi isiwe mijini tu, hata watu wa vijijini wanahitaji kutumia gesi. Hata mwaka 2015 niliongea kwamba inabidi elimu itolewe kwa wananchi kuhusu matumizi ya gesi. Sasa na gharama kubwa sana; ukienda kununua au kubadilisha mtungi wa gesi unakuwa na gharama kubwa sana. Naomba Serikali ifikirie masuala ya gharama ya gesi. Tunasema kwamba wananchi wasitumie mkaa, mbadala wake watumie gesi, lakini gesi bado vijijini haijafika. Naiomba Serikali iweze kupeleka gesi vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini kuna vijiji vingi havijapata umeme. Ni asilimia 37 tu ambavyo vimepata umeme. Naomba kwenye Kata ya Mtambula, Idunda, Kiyowela, Luhunga, Mninga, Kata zile zote pamoja na vijiji vyake; kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini nina vijiji 88. Kati ya vijiji hivyo kuna vijiji 50 havijapata umeme.
Sasa tunapopeleka umeme vijijini, naiomba Serikali kuwaambia wale Makandarasi, umeme unapelekwa kwenye kaya za watu, siyo kwenye barabara. Unaweza kuona umeme umepelekwa lakini bado haujaenda kwenye Vitongoji. Kwa mfano, mimi kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini, nina vitongoji 365. Kati ya vitongoji hivyo kuna vitongoji karibu 200 havijapata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, umeme upelekwe kwenye vitongoji ili wananchi waweze kupata umeme. Kwa mfano, pale Malangali nashukuru kwanza REA wamepeleka umeme, lakini mpaka leo haujawaka na transformer wameshaweka tayari. Mheshimiwa Naibu Waziri nadhani nilikwambia, kwamba wananchi wa Malangali hata sasa hivi wameniandikia message; Kata ya Malangali, Mbalamaziwa na Kwatwanga kule Kata ya Ihohanza, umeme haujawaka lakini nyaya zipo pale. Kwa hiyo, watu wameangalia nyaya tu, umeme upo pale. Namwomba Naibu Waziri hili alichukulie kiundani zaidi, awashe umeme pale wananchi waanze kufaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine kuna vijiji vingine wanaangalia nguzo za umeme zilipitishwa miaka ya nyuma, kwa mfano Kijiji cha Lugolofu, nyaya zimepita tu juu pale, kwa hiyo, ina-discourage sana, wananchi wanalinda nguzo. Siku moja waliniambia tutashangaa wamekata nguzo zile zimedondoka chini, sasa itakuwa imeleta tatizo kubwa. Kwa hiyo, naiomba Serikali, vile vijiji ambavyo vinalinda nyaya, hebu muwapatie umeme basi na wenyewe wafaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine katika Jimbo langu la Mufindi Kusini, kuna Mto Nyalawa, tulifanya research, kuna maporomoko makubwa sana pale. Tungepata umeme kutoka katika Mto Nyalawa halafu tungeweza kupeleka kwenye vijiji vingi sana kwenye Jimbo langu la Mfindi Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, kwa sababu muda ni mdogo, naunga mkono hoja.