Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wananchi wa Manonga kwa kutuombea dua familia yetu na hatimaye jana kuweza kufanikiwa kupata mtoto wa kiume, nashukuru sana. Hiyo ni taarifa nawaambia wananchi wa Manonga nimepata mtoto wa kiume ambaye sasa atajulikana kwa jina la Salim, ni mtoto wangu wa kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye hoja husika katika Wizara hii ya Nishati na Madini, kwanza nimpongeze Waziri aliyepata nafasi ya kuteuliwa na Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Sospeter Muhongo pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Medard Kalemani. Ni viongozi imara, shupavu, wanawajibika na wanafanya kazi kweli. Nawaunga mkono kwa sababu natambua juhudi wanazoendelea kuzifanya na natambua vita kubwa ambayo wanapambana nayo ndani na nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hayo yote nipende kuchangia katika sehemu moja inayohusu vinasaba. Niishauri Wizara ama tushauriane, katika sehemu hii jana liliibuka suala hili la vinasaba katika ajenda zetu humu ndani. Limezungumzwa na kuna mtu mmoja ambaye ame-declare interest kwamba yeye ni mfanyabiashara na masuala haya ya vinasaba yanahusika kwake na ameeleza faida na hasara. Siku ya leo tumepata document inatembea humu ndani ikieleza faida ya vinasaba. Sasa mimi hapa nimepata walakini kidogo, inawezekana, maana kuna Wabunge sasa kama wanafundishwa kusifia na wengine wanafundishwa kukataa, mivutano imekuwa mikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tujadili kwa maslahi ya nchi yetu, tusijadili kwa maslahi ya mfanyabiashara au ya Serikali au ya kukandamiza watu au watu wapate mlungula, kwa sababu inaonekana kuna watu humu wanajadili huku hata document yenyewe tunayoisoma mpaka tuisome, ueleweshwe, uanze kuja kusifia, hii document inatoka wapi ya kufundisha watu jinsi gani ya kuzungumza humu ndani?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri kwa sababu yeye ni makini sana document hii inazungumzia faida ya vinasaba, umepatikana msukumo kutoka wapi kuja kuwafundisha Wabunge kuzungumza faida ya vinasaba? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuombe sasa Wizara hii husika, Mheshimiwa Sospeter Muhongo ni mtu makini, isije kuwa hapa kuna watu wanapokea hela kuja kusifia ama kuja kuponda. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, Wizara yake iende ikayafanyie kazi, ajue kwenye vinasaba kumejificha nini? Inawezekana tunapata faida lakini kuna watu wanapata faida kwa kupokea rushwa. Haiwezekani hapa watu wanazungumzia vinasaba, wengine hata biashara hawaijui wala hawajawahi kuifanya!
Mheshimiwa Naibu Spika, tuombe Mheshimiwa Waziri, hili suala la vinasaba, nimepata wasiwasi kuona document hii imekuja humu, Wabunge wanafundishwa jinsi ya kuchangia, hii hapa ninayo. Kwa hiyo, naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri waende wakaliangalie vizuri hili suala zima. Inawezekana tunawakandamiza wafanyabiashara ama tunawa-favour wafanyabiashara. Kwa hiyo tukaangalie, tusije tukawa tunawaumiza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine hata hii EWURA sijaielewa vizuri, hizi Kanuni za uanzishwaji wa petrol stations sheria ziko Dar es Salaam, zinatakiwa zisambazwe kwenye Halmashauri zetu kule. Maana unakuta wafanyabiashara wana vituo vyao vya mafuta wanaambiwa hana hiki, hana hiki, ukiuliza sheria hana sheria, sheria ziko wapi, wanazo ofisini kwao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Sheria hizi zisambazwe ili wananchi wawe wanafahamu, wawe na uelewa wa jinsi gani ya kuendesha biashara hizi kuliko kukaa tunawabambikiza kesi milioni tano faini, tunawaumiza. Lazima tuangalie pande zote mbili, upande wa Serikali lakini pia tuangalie upande wa wafanyabiashara.
T A A R I F A...
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, dakika zangu zilindwe. Nafikiri hapo sasa Wizara itaangalia jinsi gani ya ku-handle hiki kitu, kwa sababu tayari imeshaanza kuingia migongano ya mawazo, kuna wengine wanasifia na wengine wanaponda.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze pia katika matatizo ambayo nilikuwa nazungumzia EWURA kusambaza hizi sheria katika Halmashauri zote nchini ili wananchi wanaotaka kufungua hivi vituo vya mafuta watambue ili kuweza kuhakikisha kwamba wanafanya biashara zao wakiwa salama badala ya baadaye kuwatwisha mizigo na kuleta hasara kwa wananchi hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo niiombe Wizara hii ya Nishati ikae chini iangalie kwa kina, fedha za mafuta zinakusanywa na EWURA, Wizara ya Nishati na madini haiwezi ikajitengenezea utaratibu au tukatengeneza sheria hapa ambayo itawasukuma wao ingawa chombo hiki kiko chini yao. Maana EWURA wanasimamia maji, sijui mafuta, na vitu vingine vya kupanga bei. Sasa niiombe Wizara iliangalie kwa kina jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuchangia hayo nijielekeze kwenye Jimbo langu la Manonga. Nipende kumpongeza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, alikuja Jimboni kwetu akaangalia maeneo yetu, tuna maeneo ya uchimbaji wa dhahabu. Pamoja na kuona changamoto mbalimbali alijionea mwenyewe jinsi gani tuna vijiji karibu 40 havina umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijiji vya Mwatinje, Mwashiku, kuna Kata ya Ngulu, Kata ya Ntobo, Kata ya Igoweko, Kata ya Uswaya, Kata ya Utambarale, Kata ya Mwamala, Kata ya Sungwizi, Kata ya Kitangiri, maeneo yote hayo hayana umeme. Naiomba Wizara iangalie, inapogawanya mpango wa REA phase III, basi tuwekwe kwenye program hii tupate umeme. Tunahitaji umeme kama vile ambavyo maeneo mengine yanavyohitaji kupewa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo alikuja Naibu Waziri, Mheshimiwa Kalemani alizungumzia ufutaji wa leseni kwa baadhi ya waliomiliki maeneo makubwa ya ardhi ambayo yana rasilimali ndani yake hayaendelezwi kwa miaka mingi sana. Akatoa tamko akasema kuanzia leo nimefuta leseni ya haya maeneo na aliitaja kampuni moja ya Kilimanjaro.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachoshangaza mpaka leo wale wananchi aliowapa maelekezo waende wakafuatilie wapate haki ya kumiliki ardhi ili waweze kufanya kazi ya uchimbaji mdogo mdogo pale, walikwenda pale ofisini Tabora, wakaambiwa process hii bado, hatujapata tamko kutoka Wizarani, hatujapewa maandiko, hao wahusika alikuwa nao, mgongano huu wa kauli mbili tofauti umetoka wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, Wizara yake iangalie vizuri ili kuangalia huu mgongano wa kimaslahi usiweze kujitokeza. Leo tunaambiwa kwamba huyu aliyepewa lile eneo la ardhi leseni yake itakwisha mwezi wa tisa, lakini hapo hapo siku ile alifuta ile leseni yake, hapa mgongano unatokea wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri wachukue hatua, kama wamefuta leseni maana yake wamefuta from the sport na hapo wanaanza kutoa maeneo kwa wadau wa maeneo husika, mwisho wa siku itakuja tarehe hiyo ya kufuta watatuambia ameomba Mwekezaji mwingine kutoka nje ya maeneo yetu. Naomba sana Wizara iliangalie hili la mgawanyo wa rasilimali hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutatua mgogoro alikuja Kamishna wa Madini, alikutana na watu kutoka Nzega wakizungumzia mgogoro wa Resolute. Likatoka agizo, amemwondoa yule mtu aliyekuwa kwenye lile eneo la Resolute, aliyekuwa Mwekezaji amekaa kinyume na utaratibu. Akasema from the sport aondoke, lakini mpaka tunavyoongea dakika hii yule bwana anaendelea kufanya kazi zake katika lile eneo la Resolute Nzega.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba hii Wizara ya Nishati, haya matamko yetu ambayo yanatoka Wizarani hawa walioko chini wanayachukuliaje na wanayafuatilia kwa namna gani, ili tunapotengeneza mazingira tutengeneze mazingira ya uaminifu. Siyo tu uaminifu kwa Wabunge, tutengeneze uaminifu pia kwa Serikali yetu ili tuaminiwe. Serikali iaminiwe, Wabunge waaminiwe na wananchi wafanye kazi zao kwa usalama. Hizi kauli mbili zitapelekea kuleta mgongano wa kimaslahi kati ya yule mwekezaji na wananchi ambao wanataka kuwekeza katika lile eneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuondoa mgogoro ambao utakuja kujitokeza katika eneo la Resolute Nzega, tulitatue haraka iwezekanavyo kutokana na kauli ambayo Mheshimiwa Waziri alishaitoa ya kwamba hawa watu waondoke, wawaachie hawa wananchi na waweze kujipatia kipato chao cha chini, waweze kuhangaikia kupata vitu viwili vitatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri kwa sababu nimezungumza kuhusiana na matatizo haya ya umeme, hayapo tu katika Jimbo la Manonga, yapo pia katika eneo letu la Wilaya yetu ya Igunga. Mgogoro upo wa madini katika Kata ya Nanga. Kuna mwekezaji Mchina alikuja pale, akasema anataka lile eneo, akataka kuingia contract ya kulimiliki eneo lile, akawaambia shilingi ngapi wakakubaliana milioni mia tano. Wale wananchi wakakubali wakaandikishana mikataba, wakapewa milioni mia mbili za kianzio.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha ajabu baadaye tena anakuja anataka sasa awe mbia, waendelee na yeye kama mzawa. Ukienda ukifuatilia Mchina yule amepewa sijui kibali cha uraia cha muda gani. Niombe hata watu wa Uhamiaji wanapotoa vibali vya uraia waangalie, mtu anakaa, ameshaanza kutengeneza mazingira ya mwezi mmoja, miezi miwili, anakwenda Immigration anaomba uraia, anapewa uraia anaanza kuja na documents za kusema nipewe sasa kama mzawa. Wizara hizi ziangaliwe kwa umakini. Tuna mgogoro pale Nanga kati ya Mwekezaji huyo ambaye ni Mchina ili tuutatue.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naunga mkono hoja. Ahsante.