Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante, nashukuru kunipa nafasi na mimi kuwa mmojawapo wa wachangiaji katika hotuba hii ya Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Ndugu yangu Mheshimiwa Waziri wetu Profesa Sospeter Muhongo pamoja na Naibu wake. Pamoja na kuwa ni mgeni lakini tunaona ana nia njema katika Wizara hii na Taifa hili. Vilevile nimpongeze Katibu Mkuu wa Wizara hii pamoja na wote katika Wizara ya Nishati na Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitaanza na REA, cha kwanza nitapingana kidogo kuunga mkono juu ya hoja ya ndugu yangu Mheshimiwa Ally Mohamed Keissy, kwamba REA wanafanya vizuri kwa sababu moja. REA katika mipango yao ya kugawa umeme vijijini wana upendeleo, hili liko wazi, kwa wale Wabunge waliopita, Bunge lililopita wameona, katika ile miradi ya awamu ya pili. Kuna baadhi ya wilaya na majimbo yana vijiji mpaka sitini; kwa mfano Majimbo ya Karagwe na Bunda.
Mheshimiwa Spika, ukija Jimbo la Gairo lina vijiji vinne na havijawaka umeme hata kimoja. Karagwe kuna vijiji 110, ukija Bahi kuna vijiji viwili, hapa Dodoma hakijawaka hata kimoja, sasa nataka kujua, hawa REA wanafuata vigezo gani? Wanataka sisi Wabunge tukashinde ofisini pale kwa Meneja au kwa ndugu yangu yule Msofe tuanze kuomba umeme, tusifanye kazi nyingine? Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri ameliona hili ndiyo maana safari hii hata vijiji hajavitaja humu kwa sababu nafikiri nia yake labda ni kwenda kugawa keki hii kwa kila mwananchi na kila Wilaya au kila Jimbo wapate sawa, wasirudie yale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka jana wameandika Gairo vijiji 27 ndani ya kitabu cha Wizara, nimekwenda kule na Waziri aliyepita, Mheshimiwa Charles John Mwijage, nimekwenda na Mheshimiwa Simbachawene, hawaelewi, wala watu wa REA hawajui wakati wapo Wizara ya Nishati wanaishia vijiji vinne. Kwa kweli mwaka huu ndio utakuwa wa mwisho wangu kuunga mkono hii habari ya REA.
Mheshimiwa Spika, REA hawana maana kabisa katika ugawaji wa umeme vijijini. Hata kama pesa hawapewi basi tupewe hata maneno kwamba utawekewa kijiji hiki, kijiji hiki, tubaki tunadai, sasa hata pa kudai hakuna. REA ni tatizo kubwa na ninyi Wabunge wageni mtaliona tatizo hilo, bado hamjaliona. Mwaka huu nasubiri kwa sababu nimeangalia sana kwenye hotuba ya Waziri hivi vijiji sijaviona humu mwaka huu tumetajiwa tu idadi ya pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitu kingine, mimi ni mfanyabiashara na katika biashara zangu nafanya biashara nyingi mojawapo ikiwa ya mafuta. Na-declare interest na humu ndani kuna watu wengi kuna Walimu, wakulima, wafugaji, kila mtu ana fani yake. Kwa hiyo nisipozungumzia habari ya biashara ya mafuta wakati najua na na-declare interest nitakuwa sijajitendea haki. Kwa wale waliopita Bunge lililopita wanajua kabisa vituko vya EWURA, wanavifahamu, na ndiyo maana hata Mbunge, Mheshimiwa David Silinde nafikiri alikuwa anataka kuizungumzia lakini muda ulikwisha.
Mheshimiwa Spika, kwanza lazima tukumbuke hata neno chakachua aliyelileta Bungeni na Tanzania nzima ni mimi hapa wakati nazungumzia habari ya kuchakachua mafuta ya taa, diesel na petrol ndiyo hilo likaingia chakachua matokeo, sijui chakachua kitu gani, chakachua kitu gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, EWURA ilianzishwa wakati ule mafuta ya taa yalikuwa hayana kodi, petroli na diesel zilikuwa na kodi ziliyazidi mafuta ya taa karibu shilingi mia sita. Kwa hiyo, wafanyabiashara wengi wakawa wanachukua mafuta ya taa wanayafanya malighafi wanachanganya na diesel au na petroli kwa ajili ya kujipatia kipato. Tukaanzisha mfumo wa kuweka vinasaba kwenye mafuta ili mtu akichanganya mafuta ya taa na petroli au na diesel anaona kwamba amechanganya na mafuta ya taa.
Mheshimiwa Spika, baadaye EWURA walishindwa kabisa kuondoa ule uchakachuaji kwa vinasaba vyao kwa ajili ya rushwa iliyoko EWURA. Kwa hiyo, Bunge hili likaamua kupandisha mafuta ya taa kwa kuweka kodi kwa sababu EWURA walishindwa kufanya kazi yao. Lakini cha ajabu EWURA wakahamia sasa wakawa wanaendelea kuweka vinasaba kwenye petroli na diesel. Sasa wakija kwenye petrol station wanakwambia vinasaba vimepungua, kwa hiyo, umeshusha mafuta yanakwenda mgodini au yanakwenda transit. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini vinasaba wanawekaje? ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge nataka niwaeleze. Mtu yuko Dodoma ananunua mafuta anapiga simu BP, nataka kununua mafuta, BP anamwambia bei yangu hii, anamwambia nimekubali, anamwambia weka hela Dodoma kwenye benki nitaziona kwa internet hapa Dar es Salaam. Unaweka hela Dodoma benki mtu wa BP anakwambia lete gari, nampigia simu nikiwa Dodoma Transporter peleka gari yangu BP kanipakilie mafuta.
Mheshimiwa Spika, Transporter anamtuma dereva wake nenda kapakie mafuta labda ya Shabiby BP, dereva akifika pale yuko mtu aliyepewa tenda na EWURA wanaitwa GFI, mtu wa GFI anakuja anamwambia dereva, wakati huo dereva hana elimu yoyote wala hajui vinasaba au anawekewa mkojo wa punda au anawekewa juice, anaambiwa umeona hii hivi ndiyo vinasaba hivi usinuse, nakuwekea hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kumbuka vile vinasaba havibadilishi mafuta rangi wala nini, unaletewa Dodoma. Siku ya pili anakuja mtu na gari la EWURA na havionekani kwa macho ameshaambiwa na yule mwenzie kwamba kule nilikoweka nimeweka kidogo nenda kapime. Anakuja anapima kwako, kwanza anakwambia kabisa nipe milioni tatu kama hutaki napima, usipotoa hiyo pesa na sisi Wabunge wabishi kutoa rushwa anapima, anakwambia vinasaba vipo lakini vimepungua kidogo wakati huvioni kwa macho, hujahusishwa kwenye kuviweka, wala havikuhusu; sasa huu ni wizi.
Mheshimiwa Spika, nikwambie kwa Tanzania kwa mwezi inaingiza meter tones laki mbili na elfu hamsini, sawasawa na lita mia tatu na vinasaba mtu wa mwisho anayeweka mwenye gari anachajiwa shilingi kumi na mbili na senti themanini na nane, kila lita moja unayoweka wewe mafuta. Kwa mwezi yule aliyepewa tenda analipwa bilioni tatu na milioni mia nane, kwa mwaka bilioni arobaini na sita, umenielewa.
Mheshimiwa Spika, hii kampuni ya GFI imepewa tenda bila kutangazwa kwenye magazeti na mpaka leo tenda hiyo inaendelea. Tafuteni GFI imepewa wapi hiyo tenda, haijawahi kutangazwa na imepewa tenda mpaka leo hii. Tusizungumze hapa tunasema sijui hii kampuni ya nani, hii kampuni ni ya wao wenyewe na ukimchukua leo Kalamagozi wa EWURA na yule Kaguo utaona anavyojieleza, wanajieleza kuliko hata waandishi wa habari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baadhi ya magazeti hayawezi kuandika EWURA vibaya, baadhi yao, yanayopewa matangazo, kwa sababu ukiandika vibaya tangazo hupewi. Ukiandika vibaya habari ya EWURA, hupati tangazo. Hivi leo bilioni arobaini na sita hii ukiigawanya hata kama tununue madawati tu tunapata madawati laki saba.
Mheshimiwa Spika, siungi mkono hoja hii mpaka nipate jibu sahihi la hawa watu wa EWURA. Ahsante sana.