Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na wote walioshiriki katika kusababisha nikawa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kutumia fursa hii adhimu kabisa kuchangia katika mjadala huu na napenda nianze na wenzangu wa TAMISEMI. Nimepitia vitabu vilivyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati lakini kwa masikitiko makubwa ukiangalia vitabu hivi, nyuma kabisa huku vinasomeka Kamati ya Bunge ya Utawala na Sheria za Serikali za Mitaa Aprili, 2015. Kile kingine cha Utawala Bora nacho hivyo hivyo kinasomeka Aprili, 2015. Tunaweza tukasema labda ni makosa ya uandishi lakini kwa mujibu wa taarifa ambazo ninazo bahati mbaya sana hata Kamati yenyewe haikupitia taarifa hii. Kwa hiyo, yawezekana makosa haya yapo wazi ni kwa sababu Kamati nayo kwa bahati mbaya sana haikushirikishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msingi uleule wa Bunge kuishauri na kuisimamia Serikali itategemea zaidi kama Kamati zako zitatimiza wajibu wake na zitafanya kazi kwa mujibu wa Kanuni. Tukiwa na utaratibu huu kwamba zinaletwa taarifa zinasomwa hapa halafu wanakamati hawashirikishwi sidhani kama ni utaratibu mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye mapendekezo ya Kamati, pendekezo namba 13, linasema kwa kuwa ukusanyaji wa ushuru na majengo katika Halmashauri za Manispaaa utatekelezwa na TRA, ni vyema Serikali ikawa makini na uamuzi huo hasa ikizingatiwa kuwa mamlaka hiyo haikupata mafanikio huko nyuma ikilinganishwa na mafanikio yaliyoonyeshwa na Serikali za Mitaa. Naamini kabisa kama Kamati ingekuwa imeipitia taarifa hii naamini wasingekubali kuunga mkono kwa sababu taarifa inaonyesha ufanisi umepatikana kwenye Manispaa lakini vilevile wanakubaliana kupeleka TRA, mantiki haikubali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija katika ukusanyaji wa mapato takwimu zinaonyesha Manispaa wamekusanya vizuri sana na mimi nikiangalia takwimu za Manispaa yangu ya Kinondoni miaka mitatu imekusanya vizuri sana, asilimia 75, asilimia 80, asilimia 116. Sasa leo kuamua kodi hii kurudishwa tena TRA watu ambao watategemea watendaji wale wale wa Manispaa kwa kweli hili ni jambo ambalo linanifanya kwa namna moja ama nyingine nisiunge mkono hoja hii. Nashauri Serikali wafanye marekebisho kodi hii ikusanywe na Manispaa kwa sababu imeonekana bado wanaendelea kukusanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la milioni 50 au tunaweza tukaziita mamilioni ya Mheshimiwa Rais kwa kila kijiji na kwa sisi watu wa mjini kila Manispaa na kila mtaa. Katika Jimbo langu nina mitaa 52, tafsiri yake mapesa haya tunatarajiwa kupewa bilioni 2.6 wakati Mfuko wa Jimbo wa Mheshimiwa Mbunge wengine milioni 70, wengine milioni 50. Mbaya zaidi pesa hizo wakati tunazipeleka tuna historia ya mapesa ya mabilioni ya Kikwete ambapo hakukuwa na utaratibu mzuri wa pesa zile kuwafikia walengwa. Wasiwasi wangu ni kwamba hizi pesa tunazipeleka kisiasa na bahati nzuri nashukuru hatujaona kwenye maandishi hizi pesa zimetengwa wapi. Ni bora sasa kabla pesa hizi hazijapelekwa huko tukaonyeshwa kama Bunge utaratibu gani utatumika kuhakikisha walengwa wanazipata pesa hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la elimu, nimepata tabu sana wakati mwingine tunatamani kupongeza Serikali lakini kwa hali ilivyo tunashindwa. Mfano uhaba wa matundu ya vyoo kwamba mpaka hapa tulipo Serikali yetu haijaweza kumudu kuchimba vyoo kwenye shule zetu. Serikali inatupa taarifa kwamba mwaka 2010 mpaka mwaka 2016 tofauti ya vyoo tulivyochimba ni 57,092 wakati mahitaji ya vyoo ni 464,676. Tunapokuwa na Serikali ambayo ina upungufu wa mashimo ya vyoo katika shule zetu 464,000 unakosa cha kupongeza. Kama tunashindwa kuchimba walau matundu ya choo maana yake tusistaajabu tunapopata kipindupindu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili nitamuomba Waziri ajitahidi tuondokane na aibu hii. Haiwezekani tukaja bajeti ya mwaka ujao tukaendelea kusema tuna matatizo au tuna upungufu wa matundu ya vyoo. Serikali iliyopata uhuru miaka 50 hili ni jambo haliwezekani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukirudi katika elimu, tuna programu ya elimu bure, tunasema alhamdullilah lakini kama mwenzangu alivyosema siyo elimu bure ni elimu kwa kodi. Hata hivyo, tujue kwamba ruzuku ya elimu tunayotoa mashuleni ya mtoto mmoja Sh. 500/=, shule yenye watoto 1,000 mwalimu anapewa Sh. 500,000/= kwa mwezi. Shilingi 500,000 kwa mwezi hata matumizi ya Mbunge ndani ya nyumba yake hayapatikani. Wizara lazima ije na suluhisho na katika nafasi yangu ya kushauri angalau basi tuweke sh. 2,000/=, hii sh. 500/= ni pesa ndogo sana. Leo imefika mtu anaogopa kuwa Mwalimu Mkuu kwa sababu ni mateso, ni presha, turekebishe hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye afya, akina mama wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na wazee hawahudumiwi bure kama tulivyoahidi. Nina ushahidi, mimi katika Jimbo langu tuna Hospitali yetu ya Mwananyamala, kama hiyo haitoshi hospitali zetu tumeweka viingilio kama kwa waganga wa kienyeji kwamba ukitaka kwenda hospitali lazima uwe na sh. 6,000/=. Kwa hiyo, Serikali iondoe hili tozo la kiingilio na kama kuna ulazima wa kuweka basi isizidi sh. 1,000/= ili mwananchi aweze kwenda hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora. Tunaposema utawala bora kwa kweli inatupa tabu sana hasa tukiangalia uchaguzi wa Zanzibar, tunakuwaje na utawala bora katika uchaguzi ule tulioufanya? Uchaguzi ule umetutia aibu, nafikiri Serikali imefika mahali sasa warudi, siyo vibaya mtu kulamba matapishi yako. Uchaguzi ule ulivyofanywa watu wanajua, bahati nzuri niliongea na kaka yangu Mheshimiwa Keissy, msema kweli sana kaka Keissy yeye anajua kabisa kwamba uchaguzi ule wamepiga kura watu 48, hatuwezi kuwa na uchaguzi kama huu, ni aibu. Lazima tujitahidi turudi nyuma tutazame tulipokosea ili tusonge mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la utumbuaji wa majipu. Hatuwezi kwenda kwa mtindo huu Rais ndiyo akawa anatumbua majipu. Rais ana kazi nyingi, vyombo vyake vinafanya kazi gani? Tume ya Maadili inafanya kazi gani? Imetengewa pesa hapa shilingi bilioni 6 sijui bilioni ngapi ya kazi gani, wanashughulikia Maadili gani, kwa nini wasitumbuliwe wao? TAKUKURU hawapewi uwezo na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinafanya kazi gani mpaka Rais leo ndiyo anatumbua majipu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuruka live, kama kuonekana usiku ndiyo watu wanapatikana na siye tubadilishe muda.
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Tubadili Kanuni tufanye kikao usiku.
MWENYEKITI: Muda wako umemalizika.
MHE. MAULID S.A. MTULIA: Ili tuonekane. Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti.