Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hotuba hii ya Waziri wa TAMISEMI pamoja na Waziri wa Utumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunijalia kuwepo katika siku hii njema ya leo. Pia naungana na wasemaji wenzangu kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri pamoja na Baraza lake la Mawaziri. Unajua wanasema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Sisi wanadamu wengi tuna ile hali ya kutoridhika na kwa bahati mbaya sana wenzetu tukishukuru huwa wanakereka hivi lakini huo ndiyo ukweli wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme machache ambayo yananifanya niendelee kuishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Mimi nakumbuka wakati amekuja Musoma wakati ule anatafuta ridhaa, alipofika nilimuomba mambo matatu ya muhimu kwa niaba ya wananchi wa Musoma. Nilimwambia kati ya kero kubwa ya watu wa Musoma tuliyonayo ni kwamba maji ya Ziwa Victoria yako hapa na kuna huu mradi ambao niliuanzisha kabla sijaondoka, lakini mradi huu umeendelea kusuasua kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, alichosema akishakuwa Rais, Waziri atakayemteua asipoleta hayo maji, huyo Waziri atageuka kuwa maji. Leo nashukuru kuliambia Bunge hili kwamba Mheshimiwa Dkt. Magufuli alipokuwa Rais mwaka jana, moja kwa moja zoezi lile la uwekaji wa maji lilienda kwa speed. Hivi leo ninavyozungumza mwezi huu wa sita karibu Musoma nzima itapata maji safi na salama. Kwa hiyo, ndiyo maana nasema nina kila aina ya sababu kushukuru katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi, sababu nyingine au jambo lingine nililomuomba, nilimwambia tuna Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Hospitali ile inahitaji zaidi ya shilingi bilioni 50 lakini kila mwaka inatengewa shilingi bilioni moja. Nikamwambia Mheshimiwa hii hospitali itatengamaa lini? Kwa mwaka huu peke yake nimeangalia kwenye bajeti tumetengewa toka shilingi bilioni 1 mpaka shilingi bilioni 5.5. Ndiyo maana tunasema wakati mwingine lazima tuwe na ule moyo wa kusema ahsante na ndiyo maana naposimama nasema naunga mkono hoja asilimia mia kwa mia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiendelea kuangalia hata kwenye sekta zingine, maana wakati ule Rais anasema elimu sasa ni bure kuna baadhi ya watu walibeza lakini nitoe tu mfano halisi ulioonyesha umuhimu wa ile bure aliyoisema Mheshimiwa Rais. Kwenye ile kata yangu ninayoishi peke yake, ambayo ni Kata ya Nyakato, darasa la kwanza walioandikishwa ni watoto wasiopungua 800, tafsiri yake ni baada ya kuona kwamba ile elimu sasa inatolewa bure. Kwa hiyo, ndiyo maana nasema nina kila sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya lakini tunaendelea kusema na hii ni kawaida yetu sisi wanadamu kwamba lazima ushukuru lakini haikumaanishi kwamba uache kuomba maana yeyote aliyeko hapa hata kama angekuwa na fedha kiasi gani bado kesho anahitaji na mahitaji yake hayaishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwetu kuna vitu ambavyo Mheshimiwa Waziri lazima tuviangalie sana. Moja, ni vyumba vya madarasa lakini pili ni madawati. Pamoja na kwamba yapo madawati ambayo Wabunge tutapewa kwa ajili ya kupeleka majimboni lakini bado tuna upungufu mkubwa. Kwa hiyo, naiomba kabisa Wizara na Serikali kwa ujumla iendelee kuangalia na kutathmini itafanyaje ipunguze tatizo la madawati pamoja na vyumba vya madarasa. Maana kama leo kweli shule moja ina wanafunzi wasiopungua 800, hilo ni darasa la kwanza, tafsiri yake ni kwamba darasa hilo tu ni shule. Kwa hiyo, kutokana na hali hiyo na kwa sababu kwenye bajeti hapa hatujaona kama kuna fedha za kutosha kwa ajili ya vyumba vya madarasa pamoja na madawati tujue kwamba hiyo ni changamoto ambayo tunahitaji kuifanyia kazi na tuone ni kwa kiasi gani Serikali itajipanga kulitatua tatizo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo bado tuna tatizo la upungufu wa dawa katika zahanati na vituo vyetu vya afya. Wakati mwingine inatia aibu, watu wetu ambao wana uwezo wa chini anapokwenda hospitalini anakuta hakuna dawa za kutosha. Nadhani Serikali yetu ina kila sababu kuendelea kuhakikisha kwamba tunakuwa na hizi zahanati katika maeneo yetu yote sambamba na vituo vya afya kwa ajili ya kuboresha huduma za wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kuendelea kuiomba Serikali, pamoja na kwamba jana nililiuliza katika swali la nyongeza, kusema kweli naomba Mheshimiwa Waziri alitilie maanani maana nayo ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais kwamba zile shule zetu zote za sekondari tumeziweka pembezoni mwa kata zetu, upande mmoja. Mfano kutoka pale kwenye Kata ya Bweli mpaka Kata ya Makoko zipo sekondari zisizopungua 14, zile sekondari zote barabara hazipitiki. Kwa hiyo, tukaomba barabara moja ya lami ikaziunganisha hizo shule zote ili turahisishe hata usafiri wa wanafunzi kwenda shuleni kwa maana kwamba tutaruhusu daladala kupita huko. Kwa hiyo, tunadhani kwamba barabara hiyo ikipewa kipaumbele basi itaweza kutusaidia sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo naiomba Serikali ni kutokana na zile fedha ambazo tunataraji kuzipata, shilingi milioni 50 kwa kila kijiji lakini kwetu sisi mjini tunahesabu ni shilingi milioni 50 kwa kila mtaa. Kama kuna kazi kubwa tuliyonayo ambayo tunahitaji kuifanya sasa ni kujenga uchumi wa vijana, ni kujenga uchumi wa akina mama kwa maana kwamba akina mama ndiyo wenye jukumu kubwa la kulea familia zetu. Kama hivyo ndivyo hebu tuhakikishe kwamba wale watu wetu wamepata elimu nzuri, wamepata mafunzo mazuri maana tulijifunza kidogo kwenye yale mabilioni ya JK na sasa tunadhani kwamba kwa yale tuliyojifunza kule tuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi katika hizi milioni 50 zinazokuja kwa ajili ya kila kijiji na kila mtaa. Nadhani fedha hizi zikisimamiwa vizuri kwa ajili ya vijana na akina mama, zitaleta impact kubwa na zitajenga uchumi wa watu wetu kwa maana ya mtu mmoja mmoja na maisha yao yatakuwa mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nalisema hili kutokana na uzoefu wangu baada ya kuwa nimelijaribu maana nilichukua kama pilot study, nikajaribu kwa vijana tukawaanzishia mradi wa kujitegemea. Naomba kulihakikishia Bunge hili kwamba zoezi lile linakwenda vizuri na wale vijana ambao hawapungui 200 wanafanya kazi zao za kulima vizuri na tunataraji kwamba baada ya mwaka mmoja watakuwa model wa vijana wengine kujifunza. Nadhani kwa utaratibu huo sasa wale vijana watakuwa wamepata ajira na maisha yao yatakua yamekwenda vizuri. Nazungumzia uzoefu nilionao ikiwa ni pamoja na kwasaidia akina mama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasiā€¦
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja, ahsante sana.