Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Josephine Tabitha Chagulla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu katika hotuba hii iliyoko mbele yetu. Nianze na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama hapa leo nikiwa mzima wa afya ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza na kumpongeza Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya. Nimpongeze pia Waziri Mkuu, lakini pia nipongeze sana Baraza lote la Mawaziri kwa jinsi walivyojipanga kufanya kazi nzuri, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu sasa na sekta ya afya. Utafiti uliofanyika mwaka 2015, Mkoa wa Geita unaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi sana wa malaria. Katika Hospitali zetu za Wilaya ya Geita zote zimejaa wagonjwa wa malaria. Hii ni kutokana na mashimo mengi yaliyoachwa wazi na wachimbaji wa madini. Akina mama na watoto wadogo wa chini ya umri wa miaka mitano wanakufa sana na ugonjwa wa malaria. Niiombe sana Serikali iweze kuona ni namna gani itaweza kumaliza tatizo hili, tatizo hili ni kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, naomba nitoe ushauri, niiombe sana Serikali iweze kuja na sheria ambayo itawataka pia wachimbaji hawa wa madini waweze kufukia mashimo kabla ya kuanza tena kuchimba mashimo mengine ili tuweze kunusuru maisha ya wananchi wa Mkoa wa Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa ujenzi wa vituo vya afya katika kila kata na ujenzi wa zahanati katika kila kijiji utapunguza sana msongamano katika Hospitali zetu za Wilaya. Hivi sasa Hospitali zetu za Wilaya zimejaa wagonjwa wengi sana lakini niiombe sana Serikali iweze kujitahidi kila kata iweze kuwa na kituo cha afya na kila kijiji kiweze kuwa na zahanati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi wa afya katika vituo vyetu vya afya na zahanati. Unakuta katika kituo cha afya kimoja kina daktari mmoja na muuguzi mmoja, hii kwa kweli sio sawa, huyu mtu atafanyaje kazi? Kazi hii ni ngumu inahitaji angalau watu wawe na shift. Niombe Serikali iweze kuajiri watumishi wengi katika sekta hii ya afya ili vituo vyetu viweze kuwa na watumishi wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sasa kuongelea kuhusu kauli mbovu na chafu kwa baadhi ya watumishi wa afya. Hivi karibuni tumeshuhudia vitendo vya kinyama vilivyofanywa na baadhi ya wauguzi hadi kusababisha vifo vya watoto mapacha na mama yao. Hii kwa kweli inauma, Serikali ijipange na kukemea kabisa kwa nguvu vitendo hivi visijirudie tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye sekta ya maji. Nianze mchango wangu wa sekta ya maji na tatizo kubwa la maji katika Mkoa wa Geita. Mkoa wa Geita umezungukwa na Ziwa Viktoria lakini tatizo la maji ni kubwa mno huwezi kuamini. Bado akinamama ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa hili wanahangaika kutwa nzima kutafuta maji tu. Bado wanatembea kilometa nane mpaka kumi kutafuta maji tu.
Mheshimiwa Spika, niiombe sana Serikali iweze kutatua tatizo hili ili akinamama hawa waweze kushiriki vizuri katika ujenzi wa Taifa lao. Ipo haja sasa ya Serikali kutoa kipaumbele kwa wawekezaji binafsi kama ilivyo katika sekta ya elimu ili tuweze kutatua kabisa tatizo hili la upungufu wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile miradi ielekezwe vizuri kuliko sasa hivi, kuna miradi mingi inaanzishwa lakini inasuasua na mingine haiishi kabisa. Kuna mradi wa maji katika Wilaya ya Nyang‟hwale. Hivi sasa ni mwaka wa tano lakini haijulikani kama mradi huu utakwisha au la! Kutokamilika kwa miradi kama hii kunasababisha sehemu kama vituo vya afya, zahanati, hospitali, kukosa maji safi na salama hivyo kuwa na mazingira hatarishi kwa mlipuko wa magonjwa kama kipindupindu. Niombe sana Serikali ijipange vizuri katika kutatua tatizo hili la ukosefu wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la elimu, nimpongeze tena Rais wetu mpendwa na kumshukuru sana kwa kutuletea elimu bure kutoka Chekechea mpaka Kidato cha IV. Pia niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kujenga shule za Sekondari za Kata nchi nzima. Sasa hivi tuna uhakika watoto wetu watafika angalau Kidato cha IV.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, changamoto iliyopo sasa ni upungufu wa vyuo vya ufundi pamoja na VETA. Mkoa wa Geita ni mpya, tunahitaji kupata chuo cha ufundi na chuo cha VETA, lakini siyo Mkoa wa Geita tu bali ni mikoa yote. Naomba Serikali ijipange ili tuweze kuwa na vyuo vya ufundi nchi nzima ili watoto wetu hawa wanavyomaliza Form Four waweze kuingia vyuo vya ufundi na vyuo vya VETA.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.