Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Rose Kamili Sukum

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Naomba na mimi niwe mmojawapo wa kujadili hotuba na mpango wa bajeti wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na Tawala za Mikoa na Utawala Bora, kinachonisikitisha ni kwamba kabla sijajadili kwanza habari ya bajeti, suala la utawala bora haupo kabisa kwa TAMISEMI. Upo kwa maandishi tu kusema kwamba wanaridhika na kuhakikisha kwamba kwa wakati muafaka wananchi wanapata taarifa zao kwa ubora zaidi na pia kusimamia vyema utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, simlaumu sana Waziri wa TAMISEMI, bali namwambia kwamba watendaji wako au Maafisa Masuuli katika Halmashauri mbalimbali hawako vizuri. Wao hawatekelezi ipasavyo suala la utawala bora. Wananchi katika Halmashauri mbalimbali hawana taarifa kabisa hata ya miradi yao ya maendeleo; hawana taarifa ya fedha ambazo zinafikishwa huko, je, utawala bora hapo uko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine pia kwenye suala la utawala bora inatugusa sisi Wabunge wote wa Viti Maalum. Ninashindwa kuelewa huo waraka uliotolewa na Waziri wa wakati huo ambao siujui kwamba Wabunge wa Viti Maalum hawaruhusiwi kuingia kwenye Kamati ya Fedha ndani ya Halmashauri zao ambazo wanahudhuria. Hii inawagusa Wabunge wote, sio mimi peke yangu. Ni kwa nini hatuhudhurii hizo Kamati za Fedha? Naomba kutambua hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kairuki uko hapo, wewe ni mwanamke na ni Viti Maalum, umeteuliwa kuwa Waziri, kwanini sisi kama Wabunge hatuhudhurii kwenye Kamati za Fedha ambazo ziko kwenye Halmashauri zetu? Napenda kujua kwanini msibadilishe utaratibu huo ambao haufuati utawala bora?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imesababisha katika Halmashauri nyingi, saa nyingine Waheshimiwa Wabunge hawaingii. Mbunge wa Viti Maalum angekuwepo maeneo hayo, ni wazi kabisa angekuwa mdhibiti wa fedha na mali ya Halmashauri yetu husika au mali ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la utawala bora pia naomba sana TAMISEMI kubadilisha taratibu kuhusu Wenyeviti wa Vijiji na Serikali yao kuweza kupewa posho au angalau hata msharaha kidogo ili waweze kufanya kazi vizuri kusimamia miradi ya maendeleo kwenye vijiji vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye suala la Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuhusu kuomba tuidhinishe makadirio ya shilingi trilioni 6.023 kwa ajili ya mpango wa maendeleo na makadirio ya fedha kwa mwaka huu wa 2016/2017. Mishahara tu pamoja na matumizi mengineyo imekwenda kiasi cha shilingi trilioni 4.4 lakini fedha za maendeleo ni shilingi trilioni 1.6 tu! Ukigawanya hizi fedha za maendeleo kwa Mikoa 26, kwa Wilaya 139, kwa Tarafa 562, kwa Kata 3,963, kwa Mitaa 4,037 kwa vijiji 12,545 na Vitongoji 64,677 maana yake wastani wake kwa ujumla, kila timu itapata shilingi 18,663,609.95 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu mwangalie kwenye suala la maendeleo kama hizi fedha zinakidhi haja. Kwenye taarifa yao ya fedha wameonesha kwamba wamepewa mikoa kadhaa, wamepewa vijiji kadhaa au wamepewa Wilaya kadhaa. Ina maana fedha za maendeleo hazitoshi hata kidogo! Mimi nadhani ifikie mahali sasa kwamba sisi kama Wabunge waangalie TAMISEMI waweze kupata fedha za kutosha. Ili waweze kukidhi haja ya wananchi kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilienda mbali kidogo kuhakikisha kwamba hebu hata hizi fedha za maendeleo zimekwendaje? Nikachambua programu za maendeleo kadhaa. Nikaenda kwenye programu ya maendeleo ya barabara vijijini, kasma ya 4,170. Unakuta kwamba wameomba fedha shilingi bilioni 224.7, hizi hela ukiangalia kazi yake ni kuratibu na kutekeleza mpango, kufungua barabara za vijijini ambazo hazipitiki ambayo hela yake sasa ukiangalia kwenye mchanguo huoni ni vijiji gani ambavyo wanastahili kufungua hizo barabara na ni hela kiasi gani haikuoneshwa?
Pia kwenye matengenezo ya barabara maeneo ambayo ni korofi kwenye barabara za Halmashuri, haioneshi ni barabara za Halmashauri gani, ni barabara ya wapi ni ya kijiji gani, haioneshwi kabisa. Sasa sisi kama Wabunge tunaidhinisha nini? Tunatakiwa tujue, tuidhinishe kitu ambacho tunajua, kama inaenda kwenye Wilaya ile au kama inaenda kwenye Halmashauri fulani, basi ifahamike kwamba ni Halmashauri kadhaa safari hii wamepata, labda ninyi mkapate mwaka 2018. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuangalie kwa undani. Pia nilienda moja kwa moja kwenye programu nyingine ambayo ni kasma ya 3,280, programu ya maji safi na usafi wa mazingira vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiit, fedha zimeombwa kuidhinishwa, ni shilingi milioni 412 tu! Hatuna maji, hatuna fedha za kutosha kwenye Halmashauri zetu, hatuna visima. Leo ni shilingi milioni 412, ni kufanya ufuatiliaji wa miradi, tathmini, kuratibu shughuli na kuratibu vikao vya kitaalam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunahitaji vikao vya kitaalam au tunataka visima vya maji? Sasa tunapitisha nini? Naomba mkarekebishe hapa! Tena fedha zenyewe zinatoka nje, fedha za ndani hazipo. Tunafanyaje? Miradi itaendeleaje? Ina maana kwamba Watanzania bado wataendelea kukosa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natokea Hanang. Wana-Hanang tuna upungufu mkubwa sana wa maji. Hata fedha ulizozipeleka Mheshimiwa Waziri safari iliyopita, hakuna maji. Unaenda Gehandu, hakuna maji; sijui Galangala, hakuna maji na fedha nyingi zimeenda; unaenda Garoji, hakuna maji. Hata Mjini Katesh yale maji ambayo yametengenezwa na Mfuko wa Rais nayo hayapo saa hizi. Visima vipo tu kama sanamu. Kwa hiyo, watu wanaenda kuabudu sanamu, hakuna maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri lazima hilo mliangalie pia kwa upande wa TAMISEMI, mtafanya nini kuhusu masuala ya maji na fedha hizi tunazoziidhinisha sasa hivi, shilingi milioni 412, kweli ni za kufuatilia au tunahitaji visima vya kutosha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitishwa na suala la elimu. Ukiangalia, tunasema kwamba tunapata elimu bure, kupunguza tu ile ada, lakini michango ni mikubwa sana. Nafikiri ifikie mahali sasa TAMISEMI tuangalie suala la michango ile ya ziada ambayo itawasaidia wanafunzi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mbunge amesema watu walikuwa wanakwenda na maakuli, chakula cha nyumbani. Kipindi hiki magonjwa yako mengi, mwanafunzi hawezi kwenda na chakula kutoka nyumbani kwao. Kitakuwepo kipindupindu, sijui na ugonjwa gani sijui na kitu gani; inatakiwa wanafunzi wale mahali pamoja. Mimi nadhani sasa Serikali ifikie mahali kwamba muangalie suala la chakula shuleni, itolewe na Serikali. Hiyo ndiyo kupunguza adha kwa wazazi kwa ajili ya wanafunzi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kikubwa zaidi ni hela za MMES. Huu mpango wa hela za MMES na MMEM, tunaomba mwangalie utaratibu wa hela za MMEM na MMES. Siyo kupitia tena kwa Wakurugenzi, halafu eti Mtendaji wa Kata ndio anasimamia hizo hela. Ziende moja kwa moja kwenye shule. Sasa zinavyoacha kwenda kwenye shule, wengine wanaanza kumega kidogo kidogo ambapo ukifika, hazipo shuleni tena kwa walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia suala la afya. Hospitali zetu hazina dawa, uchakachuaji umekuwa mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kutumbua majipu, lakini nashindwa kuelewa, mnasema kwamba tusimtaje Mheshimiwa Rais hapa, huyu Mheshimiwa Rais anachelewa kutumbua Wakurugenzi kwenye Halmashauri zetu na wengine wanaokula fedha. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.