Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nianze kwa kumwombea msanii Kinyambe ambaye masaa machache yaliyopita ameingia kaburini. Mwenyezi Mungu amrehemu, ampeleke peponi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisikitishwa wakati Mheshimiwa Waziri anawasilisha hapa, nilidhani angeweza kumtaja msanii huyu. Ni miongoni mwa wasanii maarufu kwa vicheko waliokuwa wanakonga nyoyo za Watanzania, lakini kwa masikitiko Mheshimiwa Waziri amemsahau. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kuipongeza sana tena sana timu yangu niipendayo Dar es Salaam Young African kwa kutangazwa kuwa mabigwa wa kihistoria wa mpira wa miguu wa Tanzania kwa mara ya 26. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwombe Mheshimiwa Waziri, najua fedha hakuna, najua bajeti yake fedha hamna, Mheshimiwa leo hapa sigongi, leo nakushauri tu brother, tunatoka Halmashauri moja. Mimi na wewe ni Wabunge wa Halmashauri moja. Mheshimiwa Waziri angalau kesho tu, Yanga watakuwa wanakabidhiwa kombe lao, TBC iwe live Watanzania waone. Angalau kesho tu, yes! Yanga watakuwa wanacheza pale Dar es Salaam na Ndanda, baadaye siku inayofuatia wataruka ndege kwenda Angola kuliwakilisha Taifa hili kwenye mashindano ya Kimataifa kwa kuwa wao ni wa Kimataifa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana juzi yalipokuwa yanaulizwa maswali hapa kuhusu bei ya ndege hapa jana, mimi nilikuwa naumia sana kwa sababu timu yangu ya Yanga inaumia sana. Ndani ya nchi inasafiri kwa ndege, nje ya nchi kwa ndege, sasa bei za ndege mkishusha zitatupa ahueni watu wa Yanga. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo machache ya utangulizi, nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri juu ya mambo machache yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mwaka 1992 mwandishi mashuhuri wa vitabu, Mohamed Said Abdulla, ni Mtanzania mwenye asili ya Zanzibar aliandika kitabu kimoja kinaitwa duniani kuna watu. Angalau nisome tu aya moja ya ukurasa wa kwanza wa kitabu chake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitabu kinaanza; “Ilikuwa kiasi cha saa moja unusu usiku, Kassim alipanda ngazi pana zilizotandikwa zulia au blanketi nene zinazoongoza kufikia ghorofa akaayo baba yake Hakimu Marijani.”
Mheshimiwa Nape, wewe ni sawa na Kassim. Tumekutandikia zulia upande uende kwa Mheshimiwa Magufuli, Baba Marijani ukamweleze shida zetu. Shida ya Watanzania, wanataka kuwaona Wabunge wao wakijenga hoja, wakiwasilisha hoja zao, nenda kamweleze Baba Marijani. Umri wako ni kijana sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Abdulla anaendelea, anawataja watu maarufu, watu wanaopata umaarufu, kuna wengine wanapata umaarufu kwa kupongezwa, wengine wanapata umaarufu kwa kuzomewa, wengine wanapata umaarufu kwa watu tu kuwachukiza, brother hili jambo limewachukiza sana Watanzania. Miongoni mwa watu wanaochukiwa, mimi inaniuma, wewe ni kaka yangu, Wabunge wawili wa Halmashuri ya Wilaya ya Lindi, tunakaa kiti hiki na hiki, nikiona unaandikwa vibaya brother inaniuma. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili nenda kamwambie baba, pita kwenye zulia kamwambie Marijani, Watanzania wanataka kuona Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naombe tena nimshauri brother, miaka ya nyuma aliyekuwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kipenzi chetu, Mzee wetu Mwinyi, aliwahi kuita timu ya Taifa sawa na kichwa cha mwendawazimu. Mheshimiwa Waziri naomba, Mzee Mwinyi bado yuko hai, twende tukampigie magoti, ile kauli aitengue. Ile kauli Mzee wetu ajirudi, inawezekana ikawa ndiyo sababu ya timu yetu ya Taifa haifanyi vizuri. Kwa nini timu yetu kila ikijaribu inapigwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nadhani siyo tu ile kauli ya Mheshimiwa Rais, pamoja na kwamba ilikuwa inatupa changamoto, leo mmeelezwa hapa, tumebakiwa na mechi mbili za timu ya Taifa, Mheshimiwa Waziri ulipokuwa unasoma hapa, nilifikiri angalau utaitaja timu ya Taifa. Tukiwafunga Misri brother, tuna-qualify. Tukiwafunga Misri tukienda Nigeria kule, tukienda kutoa sare, tuna-qualify.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mkakati gani wa kuisaidia timu ya Taifa? Vijana wetu wanapenda sana mpira. Na wewe mwenyewe Mheshimiwa Waziri nakupongeza, kila nikienda pale Taifa tunakutana, Chamazi pale tunakutana. Nakupongeza sana, unajaribu sana kwenda uwanjani. Hivi huoni kwamba Watanzania wanapenda sana soka? Kama wanapenda soka hivi jiulize kwa mapenzi yale waliyonayo, timu ikifungwa inakuwaje? Wanaumia sana.
Mheshimiwa Waziri katika hili nakuomba sana, isaidieni timu ya Taifa ivuke hapa, tumechoka kuwa kichwa cha mwendawazimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie masafa ya TBC. Kama bahati mbaya vile, Lindi inapatikana hii redio ya TBC. Maana ni bahati mbaya, lakini mmezima mitambo ya analog. Lindi leo tupo kwenye digital, hiyo Star Media Lindi haipatikani. Kama sijui unajua ama hujui! Na wewe ni Mbunge kutoka Lindi. King‟amuzi cha Startimes Lindi hakifanyi kazi; ni ving‟amuzi vya Azam na Zuku ndiyo vinafanya kazi. Hawa watu wote wana uwezo wa kulipia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini msipeleke hiyo Star Media angalau mtu akiwa na kantena kake na kadhalika, analipia shilingi 5,000 mambo yanakwenda? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni masikitiko makubwa. Mkoa kama wa Lindi ni wa siku nyingi, una mitambo ya TBC pale ipo, lakini hawapati, Star Media haipatikani Lindi, watu wanaangalia Azam na Zuku tu. Watu wale wa vijijini kule Jimboni kwangu Mchinga huyu bwana ananikumbusha hapa, Liwale ndiyo kabisa. Lindi yote brother.Wewe wa Liwale kule ndiyo pole yako kabisa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie suala la wasanii. Brother watu wanakusema sana kuwa unampenda sana Diamond. Aah, mimi si nakueleza! Nilikwambia leo nakushauri tu brother. Wasanii wetu ni kweli wana changamoto nyingi, lakini pia kuna haja ya kuangalia maadili ya kazi zao kabla hazijatoka. Leo tunakuja kuzuia chura, tayari ameshaingia mtaani. Chura yupo mtaani anarukaruka kwenye maji, anazuiwa chura, mimi nina kijana wangu pale ana miaka mitano, ukifika tu anakwambia baba chura anarukaruka. Tayari wameshamwona chura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tengenezeni mechanism ya kuhakikisha kwamba hizi kazi za wasanii haziingii mtaani bila kupitia kwenu. Leo mpaka jamii imeanza kulalamika ndio chura kaanza kuzuiwa. Sasa ndugu yangu, kuna akina chura wengi, maadili yetu yanamomonyoka na jamii inaharibika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala la ngoma za asili, sijui mnalipa kipaumbele kwa namna gani? Sisi kwetu kule kuna Sindimba. Muda siyo mrefu tutaanza kuagiza watu waje kucheza kule, maana vijana wale wadogo wadogo hawajui kabisa. Ngoma zile za asili, jadi zile mmezisahau kabisa. Nikiangalia bajeti hii uliyopewa brother, huwezi ku-function. Naona dhamira yako ya kutaka kusaidia, wewe ni kijana, una dhamira nzuri, lakini shida yangu ni bajeti. Pita kwenye zulia alilolisema Mohamed Abdulla, ukamshauri Rais akuongezee bajeti hii. Hali ni mbaya Mheshimiwa. Hayo tu leo brother!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.