Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Maryam Omar Said

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Pandani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. MARIAM OMAR SAID: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia muda ili kuweza kuchangia hoja iliyopo mbele jioni hii. Moja kwa moja nitajikita katika suala la Muungano, sote wakati tukiwa tunachangia bajeti hii ya Muungano tunachangia kwa maslahi mapana ya kuwa tunaupenda na kuuenzi Muungano. Hata hivyo, tukumbuke na tukubaliane tu na matokeo kwamba, ni kweli zipo changamoto ambazo kwamba zimepatiwa ufumbuzi lakini bado hazijafanyiwa kazi na zipo zile ambazo hazijapatiwa ufumbuzi na hazijafanyiwa kazi na hizi ndiyo changamoto kubwa zaidi ambazo kwamba zinawaumiza wananchi hususan kwa upande wa Zanzibar. Hapo sitaki niendelee sana, niishauri tu Wizara, tuweze kuzifanyia kazi zile changamoto ambazo tayari zimeshapatiwa ufumbuzi, lakini pia na zile ambazo hazijapatiwa ufumbuzi, basi twende kwa haraka zaidi ili kuhakikisha tunauweka Muungano wetu katika sehemu salama.

Mheshimiwa Spika, nikija kwenye masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, kiuhalisia mabadiliko ya tabia nchi hakuna ambaye kwamba hayamgusi, hapa ndani na hata huko nje. Ukisema suala la mabadiliko ya tabia nchi kila mtu linamgusa, hakuna mtu ambaye yatamwacha salama pindi yanapotokea. Sasa basi niishauri Wizara kwenda kwa kasi katika ile miradi ya mabadiliko ya tabia nchi, hususan kama kwa upande wa Zanzibar tukiangalia muunganiko wetu wa nchi ya Zanzibar ni visiwa na kawaida visiwa vinapata mabadiliko ya tabia nchi katika sehemu zote, mvua ikiwa kubwa tumo kule Zanzibar, jua likiwa kali tumo, bahari ikipata tetesi kidogo tu tumo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sisi tunaathirika zaidi katika pande zote, tunaiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu ndiyo wahusika wakuu kwenye masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, kwa kupitia miradi ya mabadiliko ya tabia nchi, watuangalie kwa jicho la huruma zaidi Zanzibar. Hivi sasa Zanzibar kuna visiwa hususan kule kaskazini Pemba kuna kisiwa cha Mtambwe Kuu ni kisiwa cha Jimbo la Mtambwe la Mheshimiwa Khalifa. Hiki kisiwa tupo karibu kukipoteza kabisa, ni miaka mingi sasa, hii ni changamoto kubwa na haijafanyiwa kazi. Si hicho tu kuna kisiwa cha Kojani, kisiwa cha Fundo, visiwa vyote hivi vina hali mbaya sana. Tukiangalia Kisiwa cha Kojani tuna Naibu Waziri wa Fedha jamani ni aibu, hebu tufanyeni basi twende kwa kasi angalau hizi kero za mabadiliko ya tabia nchi ikifika 2025 tuwe angalau kwenye 85% basi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikija kwenye suala la mwisho ambalo nataka nilichangie, nimemsikia Mheshimiwa Jafo hapa kawazungumzia sana mabalozi, lakini ni watu ambao tupo katika hali ngumu kiutendaji wa kazi, nazungumza hivyo mimi ni Mbunge lakini pia ni Mwanakamati ya Muungano na Mazingira lakini pia ni balozi. Juzi tu kaka yangu Mheshimiwa kanipita jina lake Mheshimiwa Msukuma alijiuzulu ubalozi baada ya kuona kwamba hauna faida. Mheshimiwa Jafo atuangalie kwa jicho la huruma mabalozi, mabalozi wanajituma sana na kazi zao unazijua, mabalozi ili apate fursa ya kufanya kazi akialikwa kwenye shughuli ya mtu ndiyo anaenda kuhamasisha huko. Msanii akialikwa kwenda kutumbuiza ndiyo anapata kwenda kuhamasisha huko, kinyume na hapo hatuwezi kufanya kazi zetu ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, balozi kama balozi mimi ananijua Waziri tu, nitakapokwenda popote pale nikijitambulisha naambiwa toa kitambulisho hakuna anayenielewa balozi mimi. Hivyo sasa ushauri wangu, tunataka Mheshimiwa Jafo atuwezesha mabalozi kutenda kazi. Anatuona na tunajitolea kwa hali na mali kwa nguvu zetu zote atushirikishe katika kila sehemu ili mradi mabalozi tuweze kufanya kazi zetu kiufanisi. Kama Waziri ameutambua mchango wetu na kuweza kuuelezea hapa, isiishie hapo tu. Mimi Mariam naweza kukimu baadhi ya nini ndogo ndogo, lakini kuna mabalozi ambao wana hali mbaya, mtu hawezi hata kutoa nauli na bodaboda kwenda sehemu nyingine, ukifika kule bado unakumbana na changamoto, unaanza kuulizwa wewe ni balozi? Ndiyo. Kakuteua nani? Nipe kitambulisho, tayari unaanza kutoka kwenye mood, hata lile ulilolikusudia kwenda kulifanya, linakushinda kufanya.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)