Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Jonas Van Zeeland

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu jioni ya leo. Nianze kwanza kumshukuru Mwenyekiti Mungu kwa kunijalia, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na na Manaibu Mawaziri, Katibu Mkuu na Manaibu wake kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya katika Wizara hii ya TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi kifupi, sisi Mvomero, tumepokea fedha nyingi sana za miradi na kipekee naomba nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, mwaka jana nilisema, niliomba fedha mbalimbali kwa ajili ya miradi na tumepata fedha nyingi na sasa hivi ninavyozungumza hapa miradi mingine inaendelea na utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Bashungwa hivi karibuni alifanya ziara Mvomero na alijionea mwenyewe miradi inavyoendelea. Pia alipata nafasi ya kwenda kuangalia sekondari ya kumbukumbu ya Sokoine, ambayo Serikali imetupatia fedha nyingi sana na hivi juzi juzi wametupa milioni 700 kwa ajili ya kuiendeleza ile sekondari ya Sokoine. Kwa bahati mbaya kulikuwa kuna shida kidogo kwenye milioni 700 na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri alifika akatoa maelekezo, kuna ubadhirifu wa zaidi ya milioni 200 na kitu, akatoa maelekezo watumishi zaidi ya tisa wachukuliwe hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze tena kwa mara nyingine Mheshimiwa Waziri, lakini mpaka sasa hivi ninavyozungumza hapa Bungeni, hakuna mtumishi hata mmoja aliyechukuliwa hatua Mheshimiwa Waziri. Kama watumishi hawa wataendelea kubaki pale bila kuchukuliwa hatua zozote hata za kinidhamu, Mheshimiwa Waziri ataendelea kutupa fedha lakini kuna watu wamejiandaa kuendelea kuzitafuna hizi fedha. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri maelekezo yake yazingatiwe na wale watumishi wachukuliwe hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sisi tumepokea fedha bilioni 2.2 kwa ajili ya madarasa 107 yale ya COVID, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Hapa nimpongeze pia Mkuu wangu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri na Madiwani kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya ya kutekeleza kujenga vyumba hivi 107 katika kipindi cha miezi miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Mvomero tuna maboma mengi sana ya madarasa, tunaomba sana safari hii watutengee fedha katika bajeti kwa ajili ya kumalizia haya maboma, hii ni miradi viporo vya muda mrefu sana. Tunawakatisha tamaa wananchi, wanaanzisha wao wenyewe, lakini mwisho wa siku Serikali inachukua muda mrefu sana kuleta fedha za umaliziaji.

Sisi moja kazi ya mwanasiasa ni kuhamasisha, nikiwa jimboni kule nahamasisha tuanzishe ujenzi wa zahanati, ujenzi wa vyumba vya madarasa, ujenzi wa nyumba za Walimu, lakini tunapofika kwenye hatua ya lenter, Serikali inachukua muda mrefu sana kuleta fedha za umaliziaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao ujenzi wa zahanati iko pale Dakawa, ina zaidi ya miaka kumi ile haijamaliziwa na tumeomba sana, kila bajeti tunaomba fedha kwa ajili ya kuimalizia. Tuna imani sasa hivi watatuletea fedha ili tuweze kumaliza. Pia nimpongeze Waziri, wametupa milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mziha na ujenzi unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda niende moja kwa moja kwenye suala la Madiwani. Mwaka jana nilisimama nikasema suala la Madiwani na wenzangu walizungumza sana masuala ya Madiwani lakini hata bajeti unaona kila Mbunge karibuni anachangia suala la Madiwani. Nimwombe sana Waziri, mwaka jana wamewapa nafuu halmashauri kwa maana Serikali moja kwa moja inakwenda kulipa zile posho za mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Waziri kumlipa moja kwa moja Mkurugenzi ili awalipe Madiwani wamewasaidia watu wa Benki, kwa sababu zile 350,000 asilimia zaidi ya 90 Madiwani wamekopa. Kwa hiyo, zile fedha zikienda kwenye halmashauri zinakwenda benki, Diwani kama Diwani pengine anabakia na 50,000. Kwa hiyo, nimwombe pamoja na jambo nzuri walilolifanya, safari hii Mheshimiwa Waziri aangalie namna ya kuongeza bajeti katika suala zima la Madiwani, angalau hata wakipata kwa kuanza shilingi 500,000, sasa hivi wanalipwa shilingi 350,000 ongeza shilingi 150,000, mpaka 2025 huko angalau watafikia hata kwenye shilingi 700,000 au shilingi 800,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimwombe Mheshimiwa Waziri na hawa wenzetu wapewe kibali cha msamaha wa kodi wawe na exemption upande wa magari. Waheshimiwa Madiwani, wanafanya kazi kubwa sana, wana uwezo wa kununua magari sio wote lakini wakipata msamaha wa kodi watakuwa na uwezo wa kununua magari na wenyewe watafanya kazi kwa urahisi, wataweza kuzunguka kwenye kata zao. Niombe sana suala hili linawezekana. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri angalau wapate msamaha wa kodi ili na wenyewe waweze kununua vyombo vya moto, waweze kufanya kazi usiku na mchana, za kusimamia fedha ambazo unazipeleka kwenye majimbo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa TBA, kama kuna bomu lingine lipo nchi hii ni hawa watu wa TBA, miradi yote ambayo inasimamiwa na TBA, miradi hii ina mambo matatu, moja lazima kutakuwa na ongezeko la mradi, thamani ya mradi ongezeko ni kubwa sana, kama mradi wa bilioni moja, hawa TBA wakisimamia watakwenda mpaka bilioni mbili na kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, muda, miradi hii haitaisha kwa wakati, kama TBA wanasimamia. La tatu, value for money katika miradi hii hakuna. Mheshimiwa Waziri anafanya kazi nzuri, miradi mingi siyo yote ambayo inasimamiwa na TBA kuna shida afuatilie, atupie jicho la tatu huo upande wa TBA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)

Whoops, looks like something went wrong.