Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Catherine Valentine Magige

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa naomba niwashukuru akinamama wa Mkoa wa Arusha kwa kuniamini na kunipa kura kwa ajili ya kuwawakilisha Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba nzuri aliyoileta wakati wa ufunguzi wa Bunge la Kumi na Moja. Hotuba hiyo iligusa maeneo mengi katika nchi yetu. Vilevile ilitupa mwelekeo na
dira ya Serikali ya Awama ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze moja kwa moja katika mchango wangu, nimefarijika sana Mheshimiwa Rais aliposema kuwa Tanzania itakuwa nchi ya viwanda. Katika Mkoa wangu wa Arusha, miaka ya 1970 na 1980 kulikuwa na viwanda vingi sana vya Serikali
pamoja na watu binafsi kama vile Kiwanda cha Tanelec, Kiwanda cha Biskuti na cha Matairi cha General Tyre. Viwanda hivi vyote kwa sasa hivi havifanyi kazi, hali iliyopelekea madhara makubwa sana kwa wakazi wa Arusha na maeneo jirani na Mkoa wetu wa Arusha.
Mheshimwa Naibu Spika, Kiwanda cha Matairi cha General Tyre kilikuwa kiwanda kikubwa sana cha kuzalisha matairi Afrika Mashariki. Kiwanda hiki kilikuwa kimeajiri watu zaidi ya 400, kiwanda hiki kilikuwa kinaingiza mapato shilingi bilioni 100 kila mwaka na takwimu hizi ni kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2008. Kiwanda hiki kilifikia stage kikawa kinaajiri watu hadi milioni moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1971, Kiwanda cha General Tyre kilikuwa kiwanda namba moja Afrika Mashariki kwa kuzalisha matairi 1,200 kwa siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama kipindi hicho kiliweza kuzalisha matairi 1,200 kwa siku, sasa hivi tunashindwa kitu gani? Kwa sasa hivi soko la matairi lipo kubwa sana, kwa sababu tukianza kukitumia Kiwanda cha Matairi cha General Tyre, tutaanza na Serikali na taasisi zake zote kununua matairi ya General Tyre pamoja na mashirika ya Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile soko la matairi bado kubwa sana, watu wengi sasa hivi wanatumia magari, magari yote hayo yanahitaji matairi. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali ikianzishe upya Kiwanda cha General Tyre ili kiendelee kuleta mapato katika nchi yetu.
Kiwanda cha General Tyre kimepunguza ajira kwa vijana wa Arusha, wananchi wa Arusha, vijana wa Arusha, wanahitaji ajira, ajira hii itapatikanaje? Itapatikana kwa kurudisha viwanda vyetu ambavyo vilikuwa havipo tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Arusha hawaamini kama Serikali imeshindwa kufungua kiwanda kile. Wananchi wa Arusha tunaamini kuna hujuma za baadhi ya wafanyabiashara ambao wana-import matairi kutoka nje kwa ajili ya faida zao wenyewe hali ambayo inapelekea sisi kukosa uwezo wa kufungua kiwanda kile cha General Tyre.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa taarifa nyingi za kipolisi zinaonyesha ajali nyingi zinatokea kutokana na matairi yasiyokuwa na ubora ambayo tunayaagiza kutoka nje.
Tumekuwa tunapoteza ndugu zetu katika ajali kwa sababu ya matairi. Sasa naona ni wakati muafaka kwa Serikali kukifungua upya Kiwanda cha Matairi cha Arusha (General Tyre) ili tuweze kutumia matairi yale ambayo yana ubora. (Makofi)
Naomba niende moja kwa moja katika suala la maji. Tatizo la maji limekuwa kubwa sana kabla ya uhuru na baada ya uhuru. Kina mama wa Mkoa wa Arusha wamechoka kuhangaika na tatizo la maji. Kuna maji Ngorongoro, Monduli na Longido. Wamenituma niombe
Serikali yao, wanamwamini Mheshimiwa Magufuli, wanaimani kubwa na Serikali ya Mapinduzi.
Tunaomba sana kina mama hawa wa Arusha wasahau shida hii ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi wa maji wa West Kilimanjaro. Serikali ikitusaidia kuanzisha mradi ule vijiji kadhaa vitapata maji. Mradi ule tunaomba upelekwe mpaka Longido ambapo vijijini vya njiani kama Tingatinga, Singa, Kerenyai, Engiraret, Orbebe, Orpesi, Ranchi
mpaka Longido navyo vipate maji. Vilevile Monduli, Monduli kulikuwa na mabwawa matatu na yenyewe yamepasuka. Wananchi wa Monduli wanakunywa maji ya mabwawani pamoja na mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana Serikali iangalie suala hili la tatizo la maji katika Mkoa wa Arusha. Naomba sana Waziri wa Maji unisaidie sana kutatua tatizo hili. Nakuamini najua ndiyo maana Mheshimiwa Rais wetu tunayemuamini akakuchagua, tunaomba utusaidie.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na migogoro ya wakulima na wafugaji. Kila siku wananchi wamekuwa wakiuwawa, mifugo imekuwa ikiuwawa lakini migogoro hii imekuwa haishi, nenda rudi migogoro hii inaendelea na wananchi wanazidi kuisha kwa ajili ya kufa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini sana wateuzi wa Rais, namwamini sana Mheshimiwa Lukuvi. Mheshimiwa Lukuvi nakuomba baada ya Bunge hili uje Mkoa wa Arusha kuna matatizo mengi ya ardhi, kuna tatizo la ardhi Loliondo, wananchi wamekuwa wakipata shida
hawajielewi, hatujui Serikali inataka nini, hatujui wanavijiji wanataka nini, hatujui wafugaji wanataka nini? Tunaomba sana Serikali iliangalie suala hili. Wananchi wamekuwa wanachomewa nyumba zao, mifugo yao inauliwa lakini sasa hivi Awamu ya Tano, tuna imani kubwa sana na Serikali na ukizingatia hotuba ya Rais wetu imeeleza kila kitu, tunaimani hawatatuangusha watatusaidia sana. (Makofi)
Naomba niongelee pia suala zima la Polisi. Polisi tumekuwa tukiwalaumu sana lakini vilevile Polisi wanaishi katika mazingira magumu sana. Nikitolea mfano Arusha Mjini kuna zile nyumba za Fire, ukipita pale ni aibu. Nyumba za Polisi ni chafu sana, ni nyumba ndogo na mnajua familia zetu za Kiafrika tunavyoishi. Polisi wale wanaishi katika mazingira ya shida sana na hata kwa kupita tu kwa mbali nyumba ni chafu sana. Tunaomba sana Serikali iangalie jinsi gani ya kuwasaidia Polisi katika suala zima la nyumba.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mabadiliko ya tabia nchi limekuwa linasababisha matatizo makubwa sana ya malisho ya mifugo pamoja na maji. Nakumbuka mwaka 2007 kulikuwa na ukame. Wilaya za Monduli, Longido, Ngorongoro, wafugaji walikosa malisho, mifugo
yao ilikuwa inakufa na wenyewe wakawa wanaishi kwa kuhamahama. Tunajua wafugaji wanaishi kwa kuhamahama siyo kwa kupenda bali kutokana na mazingira wanayokuwepo, unakuta mifugo yao haipati maji, haipati huduma kwa hiyo, inabidi wahame. Mheshimiwa
Waziri wa Ardhi, tunaomba sana mliangalie wafugaji wa Mkoa wa Arusha kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana hotuba ya Rais imegusa mambo mengi sana. Nashangaa sana watu wanapokaa na kuikejeli hotuba ya Rais. Mmeona hata juzi Mheshimiwa Magufuli amefika Arusha wananchi walivyomlaki kwa furaha. Mbunge mwenzangu wa Arusha pale awe makini sana, kwa kauli alizozitoa hapa wananchi wa Arusha wanaweza wakampiga mawe na kumzomea kwa sababu wamemkubali Magufuli na Serikali ya Chama cha CCM.
Nilitegemea Mbunge mwenzangu atasimama na kumsifu Mheshimiwa Rais Magufuli na kusifu wananchi wa Tanzania pamoja na wananchi wa Mkoa wa Arusha kwa kumpa kura za kutosha Rais Magufuli. Naomba sana tukubali, upinzani siyo kupinga kila kitu. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)