Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara hii, Sekta hii ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuwashukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri sana anayoifanya kwa nchi yetu katika maendeleo. Pili, nakushukuru na kukupongeza wewe kwa jinsi ambavyo unatuongoza humu Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze ndugu yangu Waziri Bashungwa, kwa kweli tunamtegemea anafanya kazi nzuri pamoja na Manaibu wake na Makatibu wake wazuri. Nikianzia hapo hapo nakuja kwa Manaibu Katibu Wakuu. Kuna Naibu Katibu Mkuu kwenye Afya anafanya vizuri sana, Naibu Katibu Mkuu kwenye mambo ya Elimu anafanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye mambo ya uzalishaji ambayo wananchi wengi wanategemea sana, haionekani wazi wazi Katibu Mkuu yuko wapi? Ambaye anaweza akasimamia wazi wazi kwa kusaidiana na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwenye mambo ya kilimo ambayo wananchi wengi wanakitegemea na mifugo ambayo watu wengi wanaitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini kuwa tungekuwa na Naibu Katibu Mkuu ambaye yuko assigned kwenye mambo ya kilimo, mifugo na uvuvi, sekta hii ya uzalishaji ingefanya mambo mazuri sana. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri akija kuainisha hapa ni vizuri atueleze vizuri Serikali imejipangaje kama tunaweza tukapata Naibu Katibu Mkuu ambaye anashughulikia mambo ya Sekta ya Uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kwa kusema kuwa Wabunge tuko humu ndani kuwawakilisha wananchi waliotutuma. Nimetumwa na Waheshimiwa Madiwani, Madiwani hasa wakiwakilishwa na Madiwani wa Mkoa wa Morogoro. Madiwani hasa wakiliwakilishwa na Madiwani wa Manispaa ya Morogoro. Madiwani wanafanya kazi kubwa sana na wewe mwenyewe na Wabunge wote tunaamini kuwa wanafanya kazi kubwa. Wanachoomba posho yao ni ndogo na maslahi yao, waongezewe kiasi na wenyewe waweze kufanya kazi vizuri. Tuko humu Bungeni lakini wenyewe ndiyo wanalinda majimbo yote. Tuko humu Bungeni ndiyo wanaofanya kazi zote za kijamii, za Serikali na za kichama. Kwa hiyo naomba sana tuwaangalie Waheshimiwa Madiwani kwa upande wa elimu na kwenye maslahi yao. Hapo hapo na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Wenyeviti wa Vijiji na wenyewe waangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siko mbali sana, naongelea asilimia 10. Asilimia 10 hiyo mahali inatumika vizuri, mahali pengine siyo vizuri. Ni kweli haitoshi vikundi ni vingi sana, lakini ingeweza kutosha kama ingesimamiwa vizuri sana. Kwa mfano miradi ya maendeleo kwa upande wa akinamama asilimia nne hiyo, miradi ya kimaendeleo kwa upande wa vijana asilimia nne hiyo na miradi ya kimaendeleo kwa watu wenye ulemavu ingeweza kuwanufaisha wanufaika hao.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano hela zinazorejeshwa hazina mpangilio mzuri wa marejesho. Halmashauri zingine hawajui jinsi ya kuzipangilia. Kwa hiyo naishauri Serikali iangalie jinsi ya kuwanufaisha walengwa kusudi waweze kunufaika na hizi asilimia 10. Pia uwepo ufuatiaji, ufuatiliaji mahususi wa kuona hizi fedha zinatumikaje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu TARURA. Kwa upande wa TARURA wanafanya vizuri sana. Wameongezewa hela naamini kuwa watafanya vizuri hasa kwenye barabara za vijijini na hata kwenye barabara za mijini pembezoni. Nikichukua barabara ya Mjini Morogoro ambayo inaanzia Mziga mpaka Mgambazi ni mbaya sana. Nikichukua ya Fokoland ni mbaya sana na barabara zingine za pembezoni. Vijijini Bwakila Juu ni mbaya sana, Kweuma ni mbaya sana. Kwa hiyo, hiyo ni mifano midogo ambayo TARURA naamini wanafanya vizuri lakini kwa kuongezewa hela naamini watafanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa makandarasi wanaofanya miradi ya barabara na wanaofanya miradi ya maji, naomba waangaliwe vigezo vyao kama wametimiza? Wakimaliza kazi zao walipwe kwa wakati wasiwacheleweshe kuwalipa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo ninaloongelea sasa ni upande wa elimu. Hapa elimu namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi aliyoifanya kwa hiyo hela ya trilioni 1.3. Kwa kweli kila mmoja anayaona mambo mazuri anayoyafanya Mheshimiwa Rais kwa upande wa kujenga shule, madarasa na upande wa matundu ya vyoo, lakini kuna shule zingine za sekondari, kuna shule zingine za msingi kama SUA Sekondari bado hawana maabara, bado hawana matundu ya vyoo. Kwa hiyo ningeomba kuwa na wenyewe waangaliwe.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la elimu ambalo natoa ushauri ni kwa upande wa chakula cha mchana. Chakula cha mchana hasa kwenye shule za kutwa bado ni changamoto kwenye baadhi ya shule. Kwa hiyo naomba waweke mkakati, waandike barua au mwongozo kwa shule zote za sekondari za kutwa na kwa shule zote za msingi waweze kupata chakula cha mchana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Walimu, ni kweli mgawanyo wa Walimu bado hauendi vizuri hasa kwa shule za pembezoni. Naomba waweze kupata Walimu wa kutosha hasa wa sayansi pamoja na sanaa tunaajiri. Pongezi sana Serikali kwa kuajiri, kuomba vibali, lakini mgawanyo uangaliwe.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa afya, tumejenga vituo vingi vya afya, tunamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais na hata Mkoa wetu wa Morogoro tumejenga vituo vya afya zaidi ya vitatu. Tumejenga hospitali zaidi ya sita. Kwa hiyo tunampongeza Mheshimiwa Rais lakini tatizo bado ni wafanyakazi, wataalam wa afya. Tatizo unakuta kuwa hospitali au zahanati moja kwa mfano, Zahanati ya Mvuha. Zahanati ya Mvuha kuna Daktari mmoja na Nurse mmoja, siku Daktari akiumwa au Nurse akiumwa hakuna kazi siku hiyo. Kwa hiyo tunaomba waongezwe wataalam wa afya pamoja na dawa na vifaa tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikija kwa upande wa afya hiyo hiyo, naomba waangaliwe hasa kinamama kwenye maternity zao. Kuna maternity ward nzuri sana ambazo zimejengwa, lakini wataalam na madawa hakuna. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)