Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya TAMISEMI. Awali ya yote tumshukuru Waziri wa Wizara hii, Mheshimiwa Rais ambaye anafanya kazi nzuri sana katika Tanzania hii, nami namwombea kwa Mungu aendelee kumtunza. Watanzania wamwache Rais afanye kazi yake kadri anavyoona yeye, kwa sababu ni muda wake wa kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishukuru Wizara hii kwa sababu inafanya kazi vizuri. Wapo Mawaziri vijana kabisa hapa. Yupo Katibu Mkuu, tunamfahamu Profesa, amefanya kazi mpaka kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri mbalimbali, ana uwezo huo. Makatibu wake wapo vizuri sana na wanafanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa la TAMISEMI ni coordination. Bahati nzuri ukurasa wa 90 mpaka 93 wameongelea ubadhirifu wa mali ya Umma TAMISEMI. Watumishi wazembe; mahusiano yao na Halmashauri ni kidogo sana.

Mheshimiwa Spika, kuna kitu kimenishangaza sana juzi hapa. Tarehe 07 Aprili, 2022 Mheshimiwa Rais alikuja Bunda, tukaongea, Mheshimiwa Bashungwa alikuwepo. Kukawepo na fedha ya Sekondari kati ya Tingirima na Kyandege, bahati nzuri Mheshimiwa akazungumza, hela ikaletwa. Hela ya sekondari imekuja toka tarehe 07, vifungu vya kufungua hiyo hela itumike vimefunguliwa tarehe 12 mwezi wa Nne, halafu nimeona hapa wanasema tuna call center, tuna maeneo maalum. Tatizo la TAMISEMI ni coordination. Mahusiano yake na watu wa chini ni shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, viongozi tuliowaweka hapo; Waziri ni kiongozi mzuri sana, bajeti yake tutapitisha, nami naunga mkono hata kabla sijamaliza. Yupo vizuri, tatizo, ashughulike na walaji wa Halmashauri. Halmashauri ya Bunda ni mbaya na imepata hati mbaya. Siyo chafu, ni mbaya. Amekuja Rais amesema, lakini mpaka leo hakuna mtu ametoka kwenye ofisi ya Mheshimiwa Waziri kwenda pale kushughulika na ile Halmashauri. Juzi Mkurugenzi ameulizwa mtu aliyekula hela za Afya; DMO amekula hela za Afya, anaulizwa Mkurugenzi, anakimbia na mafaili. Sasa ni vurugu zinatokea. Kwa hiyo, coordination ni mbaya sana katika Halmashauri zetu. Kwa hiyo, naomba kwenye hilo, mshughulike nalo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jambo limezungumzwa hapa la Utawala Bora na nyie mmelizungumza vizuri hapa. Utawala Bora maana yake Wizara hii ndiyo inatafsiri D by D. Wao ndio wanatakiwa wapeleke maelekezo ya Utawala Bora kwenye Kata, Tarafa, Vijiji na kwenye Vitongoji. Shida iliyopo hapa naona tunazungumzia sana Madiwani, hivi Wenyeviti wa Vijiji wanaishije? Wenyeviti wa Vitongoji wanaishije? Wenyeviti wa Mitaa wanaishije?

Mheshimiwa Spika, hivi kweli leo kijiji kina mnada, kina madini, kina mifugo na kila rasilimali zilizopo hapa, Halmashauri inakusanya zote, inapeleka Halmashauri, Mwenyekiti wa Serikali, Serikali yenyewe haina chochote inachopata. Hata kuwalipa mishahara basi, achieni mapato yao yale ya kisheria ya Na. 7 mpaka Na. 8 wayapate wao. Kama kuna mnada mahali, kijiji kilicho na mnada kipate mapato. Kama kuna mawe wanakusanya, wapewe. Sasa... (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Getere kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe.

T A A R I F A

MHE. ALLY A.J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Getere kwamba hata sasa kwenye zoezi linaloendelea la anuani za makazi, watendaji ndio wanaofanya kazi, lakini Wenyeviti na wale Wenyeviti wa Vitongoji wameachwa pembeni.

SPIKA: Mheshimiwa Getere, unapokea taarifa hiyo?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, naipokea sana, kwa sababu ni mwelewa, naye anayajua haya mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Bunge lako, kama inawezekana, siyo lazima, kama ulivyosema kwa Viti Maalumu wakae, nasi siku moja tukae basi na hii TAMISEMI hata kama ni katika ukumbi wa Pius Msekwa, tulizungumze hili jambo la Utawala Bora. Uchaguzi upo karibu, 2024 nadhani tunaanza uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unakwenda kusimamia watu, unatumia billions of money kusimamia watu; wanapatikana Wenyeviti wa Vijiji, zinapatikana Serikali, wanapatikana Wenyeviti wa Vitongoji, halafu unawa-dump. Hakuna semina, hakuna mafunzo, hakuna vitabu vya kujifunza, hakuna chochote. Haiwezekani! Sasa tunakuwaje na Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huku juu sisi tunatembelea magari, wao hata kuwasimamia basi wapate chochote. Halmashauri inakusanya chochote; mchanga inakusanya, mawe inakusanya, minada ni yao, kila kitu inabeba. Inawaacha wamekaa pale bure. Sasa Utawala Bora huu utakuwaje jamani? Haiwezekani. Kwa hiyo, nafikiri kwamba hili nalo tuliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona Wizara imetenga fedha nyingi sana za sekondari; na sera zetu zinasema tujenge Sekondari kwenye Kata, tujenge sijui vituo vya afya kwenye Tarafa, sioni shida. Naomba twende mbali zaidi, tujenge sekondari kwenye maeneo maalum. Inawezekana tukawa na Kata tatu zina sekondari moja. Umbali wa kutoka Kata hiyo mpaka sekondari ni kilomita tatu. Inawezekana kwa mfano Bunda, ukitoka Vijiji vya Mahanga na Machimero kwenda Sekondari ya Mihingo ni kilomita 17, halafu leo unasema huwapi sekondari. Watoto wanaokwenda kujiunga kutoka hivyo vijiji wanaweza kuwa 60, wanamaliza 20.

Mheshimiwa Spika, umbali wa kutoka pale ni mrefu, mvua ikinyesha hakuna mahali pa kujikinga, ni porini. Kwa hiyo, tuwe na dhana ya kujenga sekondari kwenye Kata na kwenye maeneo maalum ili tusiwe na fedha na lengo tu kwamba tunajenga kwenye Kata, hapana, ni maeneo maalum.

Mheshimiwa Spika, leo Sekondari ya Sanzate ambayo wanaiita Mama Samia, inajengwa na hapa tunapozungumza wananchi wanachimba msingi. Naomba Serikali itambue hiyo Sekondari. Wananchi wamechoka, Sekondari ya Mahanga na Machimero wanachimba msingi, Sekondari ya Nyaburundu wanachimba msingi, Sekondari Maliwanda na Kisarakwe wanachimba msingi. Wananchi wamechoka, wanataka kujenga sekondari kwenye maeneo maalum. Umbali wa kutoka kwenye maeneo hayo kwenda hapo, ni suala kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, tumezungumza vituo vya afya, kuna vitu vinashangaza sana. Nami nimekuwa Bungeni hapa wakati fulani najiuliza maswali mengi sana. Tuliomba vituo vya afya vikajengwa 2016, tukaambiwa vituo vya afya vinajengwa kwa shilingi milioni 700. Kwa mfano, Kituo cha Afya Mgeta, shilingi milioni 700, tukaambiwa tutakupa shilingi milioni 400, halafu shilingi milioni 300 itapelekwa MSD kuleta vifaa tiba. Tumepewa shilingi milioni 400 tumejenga Kituo cha Afya Mgeta, kipo mpaka leo, vifaa hakuna. Wameleta vifaa vya shilingi milioni 161, wame-dump hapo ndani. Hata majokofu ya kufanyia mortuary hamna.

Mheshimiwa Spika, nauliza, tuliambiwa hapa zile fedha siyo kwamba zilikuwa za makusanyo, tulikuwa tumepata msaada sijui wa Canada sijui wapi, shilingi milioni 700 kila kituo. Waliopewa shilingi milioni 500, watapewa shilingi milioni 200; waliopewa shilingi milioni 400, watapewa shilingi milioni 300, hizo fedha ziko wapi? Ziko wapi? Tuliambiwa kwamba zimekwenda MSD, ziko wapi? Kwa hiyo, nafikiri Mheshimiwa Waziri akija hapa aje na tafasiri ya kwamba hizi fedha zinapatikana wapi?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba kwamba katika ile haja ya kujenga TAMISEMI, nyie vijana msimwangushe Rais, amewaamini sana. Jamani mimi niseme, Rais Samia amewapa mamlaka yote Mawaziri. Kwa hiyo, kama Waziri anazingua, ni yeye; nasi humu Bungeni tutamzingua.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hatuwezi kusema kwamba mnakosa nini, mnapewa msaada. Juzi Mheshimiwa Bashungwa nimeona Mheshimiwa Rais anakwambia, Inno! Anakuita Inno, take care. Sasa nasi tunakwambia, umepewa hiyo kazi, Rais amekuamini sana. Tutekelezee yale ambayo yanayoitajika.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, tujengewe Sekondari Jimbo la Bunda. (Makofi)