Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa na mimi kuwa sehemu ya kutoa mchango kwenye taarifa iliyowalishwa na Mheshimiwa Waziri kuhusu Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza kwanza kwa kuwa taarifa ambayo amewasilisha imefanya tathmini imetutaarifu utekelezaji wa bajeti ya 2021/2022. Napenda niipongeze sana Serikali kwa mafanikio mbalimbali waliopata ikiwemo kwenye ukusanyaji wa mapato na kupeleka pesa nyingi za maendeleo kupitia mapato ya ndani, kwa hiyo naipongeza sana Serikali. Vilevile, kwa kuwa pia taarifa imeonesha utekelezaji wa bajeti wa 2022/2023 robo ya kwanza, kwamba tunaendelea vizuri naomba niipongeze sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mpango huu ambao umewasilishwa wa mapendekezo naomba nipendekeze mpango huo utakapokuja sasa uainishe na uweke bajeti ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Hali ilivyo katika dunia na nchini kwetu si nzuri. Tumeona ukame, tumeona shida ya maji na tumeona namna gani hata hali ambayo inakwenda kuwa tete. Kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Waziri katika hili ni kulizingatia; na kwa kuwa tunajua hata sasa hivi Rais wetu yuko nchini Misri akihudhuria Mkutano wa Nchi kwa ajili ya mabadiliko ya tabianchi, kwa hiyo ninaomba sana jambo hili litiliwe mkazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo nipongeze kazi nzuri inayofanywa kwenye miradi ya kimkakati hususan, ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Katika ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kama ambavyo Kamati tumesema, kwamba kazi inaendelea vizuri na hata taarifa ya leo ambapo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na Mheshimiwa Rais wa Misri inaonekana kazi imefika asilimia 77 na kwamba Maraisi hao wawili wameona kazi nzuri inayofanyika. Na kwa mujibu wa taarifa ya kwenye vyombo vya habari wamekubaliana kwamba bora bwawa lichelewe lakini lijengwe kwa viwango vinavyokusudiwa na ubora wa hali ya juu. Kwa hiyo mimi nadhani kwa kuwa Marais hawa na kwa kuwa kazi inaonekana ni nzuri tuipe nafasi Serikali iendelee kutekeleza ujenzi wa bwawa hili kwa sababu mambo yanaendelea vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwa ile CSR ya bilioni 260, kwa kuwa tangu mkataba umesainiwa tarehe 15 Desemba, 2018 mpaka leo CSR zile hazijatumika kwa kuwa kulikuwa na mabishano. Lakini sasa TANESCO imewasilisha miradi kama minne, ujenzi wa vyuo katika Mkoa wa Lindi, Kigoma, Tanga na Dodoma. Lakini sisi Mkoa wa Pwani na Morogoro tumeomba kwa kuwa kwa mujibu wa mkataba CSR inatumika kwenye maeneo yaliyokusudiwa. Ninaiomba Serikali hili litazamwe kwa jicho la huruma Mkoa wa Pwani na Morogoro maeneo ya Mwaseni na Kisaki tupate miradi kutokana na bilioni 260.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kwa kuwa hata taarifa ya leo imesema Mheshimiwa Rais Samia ameelezea kwamba bwawalinakaribia kuanza kujazwa maji. Vilevile, kwa kuwa kuna hali ya mazingira ya mito inayotiririsha kwenye Mto Rufiji Mito ya Ruegu, Ruaha Mkuu na Mto Kilombero kuwa na hali ya uchafuzi wa mazingira na ukame unaoendelea ninashauri Serikali sehemu ya bilioni 260 zitumike kupambana na mazingira ya maeneo hayo, upandaji wa miti, uondoaji wa mifugo kwenye mito yote hiyo inayopeleka maji Mto Rufiji ili zoezi likianza la kuweka maji kwenye bwawa letu lipate mafanikio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze Wizara ya Nishati kwa Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia. Jambo ambalo kwa mara ya kwanza linaenda kutiliwa mkazo. Baada ya mafanikio ya kumtua mama ndoo kichwani Mheshimiwa Rais amekuja na kampeni hiyo. Sehemu ya bilioni 260 basi zitumike pia kama mchango katika kuhakikisha maeneo yaliyoharibiwa kwa kasi ya ukataji wa miti, zinatumika kurejesha mazingira mazuri katika maeneo hayo ili mradi wetu huu uweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Wilaya ya Rufiji, Wilaya ya Morogoro Vijijini, Wilaya ya Kibiti tukumbukwe kwenye Shilingi bilioni 260, na ni haki yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nipongeze; katika hali ya kupambana na mazingira ya ukame yaliyopelekea hali ya upatikanaji wa maji kuwa ngumu, naipongeza sana Serikali chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza kuanza kwa kutekeleza mradi wa maji wa kuyatoa Mto Rufiji. Jambo hili halikupata kufikiriwa, lakini ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita mmekuja na mradi huo. Maana yake maji yatatoka Mloka, yatapita Vikumbulu, yatakuja Kisarawe na Dar es Salaam. Maji yatatoka Mloka yatapita Mkongo, yatakuja Rufiji, Kibiti, Mkuranga na Dar es Salaam. Kwa hiyo, naishukuru sana Serikali na kuipongeza kwa kuanza ujenzi wa Bwawa la Kidunda. Naomba miradi hii ionekane waziwazi katika mpango unaotarajiwa wa 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wowote unahitaji mapato. Nimeona matarajio ya Mpango wa 2023/2024 wa kukusanya zaidi ya shilingi trilioni 43 na matumizi ya hizo shilingi trilioni 43. Naomba niishauri Serikali kuendelea kutilia mkazo namna ya matumizi sahihi ya mashine za kutolea risiti. Tumeona kwenye ripoti ya CAG kwamba baadhi ya sampling ya watu 3,594, waliyoifanya kwa baadhi ya wafanyabiashara kwenye mikoa 15 ya kikodi, wafanyabiashara 1,794 hawakuwa wanatumia mashine za kutolea risiti. Mheshimiwa Waziri hata kwenye taarifa zako umekuwa ukitoa. Sambamba na hilo, kuna baadhi ya wafanyabiashara sampling zaidi ya 10,000 hawakufikiwa hata kukaguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mamlaka hii Mheshimiwa Rais ameitilia mkazo na kuipa kibali, kwa mara ya kwanza imeajiri watumishi 1,200 kwa mkupuo tangu Mamlaka hii imeanzishwa. Napongeza sana hatua hii. Naiomba Serikali iwatumie kikamilifu kuwafikia wafanyabiashara wengi wakaguliwe, watathminiwe hatua za kikodi, na tutumie takwimu za Sensa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dkt. Albina Chuwa alisema siku ile ya uzinduzi wa matokeo kwamba Sensa hii itabainisha wafanyabiashara wako wangapi na Shughuli zao mbalimbali. Natamani kuona mpango ujao uainishe ongezeko ya walipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, tuna Muswada wa Bima ya Afya unaokuja Ijumaa, lakini kwenye Mpango huu haijaonekana wazi wazi. Kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri, hilo lizingatiwe kwa sababu kwa kuwa wanawake tuko wengi tuna matarajio sana na hii Bima ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja hii. (Makofi)