Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. STANSLAUS S. MABULA – MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, na mimi nitumie nafasi hii kwanza kukushukuru sana kwa uamuzi wako uliopelekea Bunge lako kuifanya kazi hii kwa siku takribani nne ambazo hakika Wabunge wameisaidia sana Seriakli kuonesha namna ambavyo usimamizi, changamoto na mapungufu yaliyopo katika utendaji wa halmashauri zetu nchini. Ni mategemeo yetu kwamba mambo mengi yatazingatiwa leo baada tu ya maazimio haya ili yakaweze kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kabla sijaenda kwenye maazimio ya Bunge lako, yako mambo mawili ambayo nilitamani niyaseme. Moja ni lile la asilimia 10 ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamelizungumza, na wamelizungumza kwa sababu wanaamini kwamba fedha hizi ni nyingi sana; zingeweza kulisaidia sana Taifa kama malengo yake yalivyo.

Mheshimiwa Spika, msingi mmoja ambao umetushangaza sana Kamati, kwa sababu, ipo Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, katika Sura 209 imeeleza wazi, na bahati nzuri sana imeitaja Kamati ya Huduma za Mikopo. Kamati hii kwenye kanuni ya 14 (1) inaundwa na Mkurugenzi mwenyewe wa Halmashauri, Muweka hazina wa halmashauri, Afisa Mipango, Afisa Ushirika, Afisa Ustawi na Afisa Maendeleo. Maana yake ni nini? Watu wote hao ni Wakuu wa Idara wenye weledi na wenye sifa za kusimamia kazi hii. Kwa hiyo tulitegemea sana kuona kwamba tunapozungumzia mapungufu kwenye eneo la asilimia kumi ambayo tunatarajia iende kwenye jamii na ikalete matokeo chanya haifanyi kazi yake sawa sawa. Tafsiri yake ni kwamba, inawezekana tuna watu ambao hawana uwezo wa kusimamia majukumu waliopewa.

Mheshimiwa Spika, suala la pili ambalo lilitutafakarisha sana ni suala la matumizi ya POS. Hizi POS zililetwa ili zisaidie, na mfumo huu umeletwa ili uisaidie Serikali katika ukusanyaji wa mapato na uirahisishie, lakini kumekuwa na mchezo ambao unaendelea kwenye matumizi ya POS, unakuta POS imezimwa kati ya siku 1000 mpaka 4,000. Maana yake ni kwamba, ikizimwa POS kwa siku 4,000 unazungumzia miaka zaidi ya mitatu mbele. Nyingine imezimwa zaidi ya siku 1,000 nyuma. Yaani hata kabla ya mfumo wa POS haujaanzishwa, POS imeshakuwepo na imezimwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tafsiri yake ni kwamba watu wanazima mashine na kurudisha mfumo nyuma wakati hela inayokusanywa haitoonekana popote pale. Na ile iliyopelekwa mbele maana yake ni kwamba ile fedha hautaiona wewe ambaye ni msimamizi pale. Kwa hiyo tunadhani yapo majukumu na ulazima kabisa wa Serikali kusimamia hili jambo na kuweka mifumo ambayo itatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kabla sijasoma maazimio ya Bunge lako, nijielekeze kwenye maelezo mafupi sana ya utangulizi. Kifungu cha 10 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya Mwaka 2008 kinatamka bayana kwamba ukaguzi unaotekelezwa na CAG ni kwa niaba ya Bunge. Naomba kuliarifu Bunge lako kwamba LAAC imejiridhisha kwamba kuwa ukaguzi wa hesabu za mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2021 ulizingatia misingi ya Katiba na Sheria za nchi na viwango vya Kimataifa na Kitaifa. Katika kufikia hoja za ukaguzi zilizojadiliwa na Kamati. Aidha, kifungu cha 16 cha nyongeza ya nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Juni 2020 kimeweka Sharti la kwamba msingi wa kazi za LAAC ni taarifa ya ukaguzi uliotekelezwa na CAG.

Mheshimiwa Spika, Kwa sababu hizo, mapendekezo ya maazimio ambayo nitayawasilisha hivi punde yanatokana na uchambuzi wa Kamati kuhusi ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali wa Hesabu za Serikali kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa Fedha ulioishia Juni 2021. Aidha, maazimio haya pia yamezingatia michango ya Waheshimiwa Wabunge mbali mbali ambayo imetolewa hapa Bungeni kwa kujadili taarifa hii ya Kamati.

Mheshimiwa Spika, Wabunge zaidi ya 82, miongoni mwao Wabunge 71 wamechangia juu ya taarifa ya Kamati ya LAAC, na uchangiaji wao umetusaidia sana kuboresha maazimio yetu tuliokuwa tumeyatengeneza na kuyatoa awali. Ni matumaini ya Kamati ya kwamba maazimio haya yatasaidia katika kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha za umma katika kuimarisha uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba uniruhusu nijielekeze kuwasilisha mapendekezo, hasa nijielekeze kuwasilisha maazimio kumi na moja kama ifuatavyo: -

(1) Mheshimiwa Spika, azimio la kwanza ni kuhusu mfuko wa mikopo kwa vikundi vya kina mama, vijana na wenye ulemavu. Ukaguzi uliofanywa na CAG umeonyesha kasoro mbalimbali za uendeshaji wa mfuko huu ikiwemo: -

(a) Halmashauri 155 kushindwa kukusanya shilingi bilioni 47.01 zilizotolewa kwa vikundi mbali mbali.

(b) Halmashauri 11 kushindwa kuhamisha shilingi bilioni 1.24 kutoka Akaunti ya Amana kwenda akaunti ya mifuko.

(c) Halmashauri 17 zilitoa mikopo ya shilingi bilioni 3.26 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu bila kuzungatia uwiano ulioanishwa.

(d) Halmashauri 83 kutokuchangia jumla ya shilingi bilioni 6.68 kwenye mfuko kutoka kwenye mapatao yake ya ndani.

Mheshimiwa Spika, hivyo basi, Bunge linaazimia ya kwamba, Mamlaka ya nidhamu ya Wakurugenzi ichukue hatua dhidi ya Wakurugenzi wote waliobanika kushindwa kwa uzembe kusimamia kikamilifu utoaji na usimamizi wa mikopo hii kama ilivyoelekezwa kwenye kanuni ya 24(2) ya Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. (Makofi)

(2) Mheshimiwa Spika, kuhusu upatikanaji wa ruzuku ya maendeleo katika mamlaka za Serikali za Mitaa. Bunge linaitaka Serikali kutekeleza yatuatayo: -

(a) Kuzingatia matakwa ya sharia ya matumizi ya fedha zinazopitishwa na Bunge katika kila Mwaka wa Bajeti ili kuendelea kujijengea imani Bungeni na kwa wananchi.

(b) Kuweka angalau karibio kwa kiasi cha ruzuku endapo itabidi baadhi ya halmashauri kuzidishiwa kuliko vile inavyotokea kwamba halmashauri zingine hupewa kiasi kidogo mno wakati zingine hupewa zaidi ya asilimia hamsini.

(c) Kutorejesha Hazina fedha zinazokuwa zimepelekwa katika halmashauri kwa madai kuwa mwaka husika wa fedha umeisha ili kukamilisha miradi inayohusika.

(3) Mheshimiwa Spika, kuhusu uwekezaji wa tija, kuhusu uwekevu na tija katika uwekezaji wa mitaji ya umma. Ukaguzi umebainisha dosari zinazohusu uwekezaji wa mitaji ya umma katika baadhi ya halmashauri nchini.

Mheshimiwa Spika, dosari hizo ni pamoja na uwekezaji unaofanyika bila upembuzi yakinifu wala andiko la biashara. Bunge linaitaka Serikali, kuhakikisha kuwa halmashauri zote zinazofanya uwekezaji, unazingatia fursa za uwekezaji na tija katika maeneo mbalimbali ya halmashauri kuliko hali ilivyo sasa ambapo kila halmashauri inataka kuwekeza kwenye soko na kituo cha mabasi tu. Aidha, Serikali iandae muongozo na kanuni inayoelekeza namna bora ya uwekezaji kwa ngazi za halmashauri na kuzingatia umuhimu wa maandiko miradi kabla ya kuanza miradi husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nne, kuhusu manunuzi na mikataba ya upatikanaji wa huduma na bidhaa. Ukaguzi umebaini udhaifu katika ununuzi na upatikanaji wa huduma na bidhaa katika halmashauri bila kufuata taratibu zinazohusika. Hali hiyo inaweka mwanya wa upotevu wa fedha za Umma. Hivyo basi, Bunge linaiagiza Serikali kusimamia ipasavyo manunuzi yote ya Umma kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na kwa kuridhiwa na Bunge. Aidha, Maafisa Masuuli wote watakaobainika kutosimamia ipasavyo agizo hili, wachukuliwe hatua kali za kisheria kwa nia ya kukomesha ubadhirifu na kuliletea Taifa manufaa stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tano, kuhusu upatikanaji wa stahiki za watumishi kwa mujibu wa sheria. Bunge linaitaka Serikali kushughulikia mara moja madai yote ya stahiki za watumishi wa halmashauri kwa mujibu wa sheria ambazo hazijatolewa na kuchukua hatua kali kwa waajiri wasiozingatia matakwa ya sheria zinazohusika na stahili za watumishi.

Mheshimiwa Spika, sita, kuhusu ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri. Imebainika kwamba halmashauri zilizo nyingi zina udhaifu katika eneo la ukusanyaji wa mapato ya ndani kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo upotevu wa mapato kwenye mifumo ya kielektroniki, rushwa na kutosimamia ipasavyo sheria, kanuni na taratibu za kifedha; hivyo basi, Bunge linaitaka Serikali kutekeleza yafuatayo: -

(a) Kuhakikisha kuwa mfumo mpya wa ukusanyaji wa mapato, yaani TAUSI, unaanza kutumika katika halmashauri zote za Serikali nchini ndani ya mwaka wa fedha wa 2022/2023;

(b) Kuchukua hatua kali za kisheria kwa watendaji wote ambao wanakusanya mapato nje ya utaratibu wa kisheria na ambao hawapeleki makusanyo hayo benki kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, saba, kuhusu matumizi yasiyofaa ya fedha katika Akaunti za Amana. Imebainika ya kwamba katika halmashauri mbalimbali fedha zilizomo katika Akaunti za Amana zinatumika kwa shughuli ambazo hazikutarajiwa. Ripoti ya CAG ilibainisha matumizi mabaya ya Shilingi bilioni 9.74 kutoka katika Akaunti za Amana kutokana na kutosimamiwa ipasavyo. Matumizi hayo yalibainika katika halmashauri 81 nchini na hivyo basi, Bunge linaitaka Serikali kuhakikisha kuwa fedha zinazowekwa katika Akaunti za Amana zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa kuliko hali ilivyo sasa ambapo akaunti hizo zinaonekana kutumika kama maficho ya fedha ambazo baadaye hutumika kibadhirifu.

Mheshimiwa Spika, aidha, Maafisa Masuuli wote waliotumia fedha hizi kinyume na uataratibu wachukuliwe hatua kali za kinidhamu. Mifano ipo kama ambavyo tuliitaja, kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa ilitumia zaidi ya Shilingi milioni 90 bila utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, azimio la nane, kuhusu upotevu wa mapato katika mifumo ya kielektroniki ya kukusanyia mapato. Imebainika kuwepo kwa upotevu wa mapato kupitia katika mifumo ya kielektroniki katika halmashauri zetu. Katika mwaka wa fedha 2021, halmashauri 27 zilifanya marekebisho ya miamala yenye jumla ya Shilingi bilioni 1.6 kwenye mfumo bila uthibitisho wa ulazima na uhalali wa marekebisho hayo kufanyika. Hivyo basi, Bunge linaitaka Serikali kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa watumishi wote waliohusika na upotevu, mathalan watumishi walio katika halmashauri ambazo miamala ya mapato ilibadilishwa au kufutwa bila uthibitisho wa ulazima wa kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tisa, kuhusu hasara ya kifedha kutokana na vitendo vya taasisi za Serikali dhidi ya halmashauri. Imebainika kuwa, jumla ya Shilingi bilioni 2.34 hazijalipwa katika mamlaka mbalimbali za Serikali za Mitaa nchini kutokana na huduma za tiba zilizotolewa kwa wanufaika wa mfuko huo. Hivyo basi, Bunge linaitaka Serikali kushughulikia mara moja suala la NHIF kutorejesha gharama za matibabu na vifaatiba vinavyotolewa na halmashauri kwa wanufaika wa bima ya afya chini ya mfuko huo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.

Mheshimiwa Spika, Bohari ya Madawa (MSD); Halmashauri nyingi zimekuwa zikilipa fedha kwa bohari ya madawa nchini (MSD) pasipo kupelekewa dawa na vifaatiba kwa wakati. Zaidi ya Shilingi bilioni 1.17 hazijawahi kupelekwa kwenye vituo dawa za gharama hiyo. Hivyo Bunge linaitaka Serikali kuisimamia ipasavyo MSD ili iwe inapeleka dawa na vifaatiba katika halmashauri kwa muda usiozidi mwezi mmoja kulingana na mahitaji ya halmashauri husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA). Imebainika kuwa halmashauri mbalimbali zimekuwa zikiamrishwa au zikihimizwa kupeleka fedha kabla ya kupata huduma au bidhaa husika kwa upande wa uagizaji na manunuzi ya magari. Wameshindwa kufanya vizuri kwani wamekuwa na tabia ya kurudisha fedha kwa wateja pasipo kukamilisha manunuzi ya magari hayo kwa muda uliopangwa. Hivyo basi, Bunge linaitaka Serikali kuisimamia GPSA ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kazi zao ili kuzisaidia halmashauri katika utekelezaji wa mipango yao kuliko hali ilivyo sasa ambapo GPSA huchangia kuzizorotesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA). Bunge linaitaka Serikali kuimarisha TEMESA ili iweze kuzisaidia halmashauri na taasisi nyingine za Serikali ili kupunguza malalamiko ya udhaifu wake katika eneo la ukaguzi na utengenezaji wa magari na mitambo katika halmashauri.

Mheshimiwa Spika, azimio la kumi, kuhusu uteketezaji wa dawa za binadamu katika halmashauri na vituo vya afya. Taarifa ya CAG ya mwaka wa fedha 2021 inaonesha kuwepo kwa wimbi kubwa la uteketezaji wa dawa za binadamu zenye thamani kubwa ya fedha. Kwa miaka mitatu tuliyotolea mfano, zaidi ya Shilingi bilioni 12.3 katika halmashauri 91 dawa zake ziliteketezwa. Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa hazipokei dawa zilizobakiza muda wa matumizi unaopungua miezi sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, azimio la 11, upungufu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Uchambuzi wa Kamati kutokana na taarifa ya CAG umebainisha kuwa, baadhi ya halmashauri hazina watumishi wenye taaluma unaohitajika na kulazimika kutumia watumishi wasio na sifa kwa kazi zinazohitaji utaalamu. Kitendo hiki kinasababisha kufanyika kwa maamuzi yanayosababisha hasara kubwa katika halmashauri zetu. Hivyo basi, Bunge linaitaka Serikali kupeleka katika kila halmashauri wataalamu wa kutosha kwenye sekta zote muhimu zinazohitajika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwatumia ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kukushukuru wewe na Waheshimiwa Wabunge wote kwa mijadala mizuri.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, naafiki.