Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Dr. Eliezer Mbuki Feleshi

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuweka hai na kutuwezesha kuwepo kwenye majukumu yetu.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru pia wewe binafsi kwa jinsi ambavyo umeendelea kuongoza shughuli za Bunge hili. Aidha, nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kuendelea kusimamia Utawala wa Sheria na vile vile naamini kazi inayofanyika kwenye Mkutano huu hasa kwa hizi siku nne, ni matokeo ambayo ni ya kazi ya Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ambayo kwa mujibu wa Ibara ya 153(4) kila anapokabidhiwa basi inawasilishwa ndani ya Bunge lako Tukufu. Ndio msingi kwa mujibu wa Nyongeza ya Nane ile, Sehemu ya Nne ya Kamati hizi tatu zilizowasilisha taarifa hii kuweza kuwasilisha taarifa zao pamoja na kuwezesha mjadala ambao unaendelea.

Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana Wenyeviti wa Kamati pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao na vilevile niendelee kuwashukuru sana Wabunge kwa yote ambayo wamechangia. Vile vile niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na nikimaanisha Mawaziri kwa maana yangu na kwa maana ya sheria zetu na Katiba hasa kwa mujibu wa ile Ibara ya 54. Wao ni sehemu ya utendaji kazi zinazoongozwa na mamlaka inayotawala chini ya Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo Waheshimiwa Mawaziri nawapongeza sana.

Mheshimiwa Spika, zaidi ya wachangiaji 70 wameshiriki kuchangia hoja ambayo iko mezani na mambo kadhaa wa kadha yamejitokeza. Wapo ambao wameeleza ni vizuri Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aongezewe mamlaka na hata ikiwezekana kuendesha mashtaka ya wale ambao wanabainika kuwa wamekinzana na sheria. Pia wapo wale ambao wameona kwamba sheria zinazotolewa kwa wahusika hazifai kabisa na wengine wamependekeza adhabu za kunyongwa na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, vilevile wako ambao wameshangazwa na kuona watu ambao kwa njia moja au nyingine wameonekana kwenye taarifa kwa kipindi husika wakiwa bado kwenye utumishi wa umma. Pia wapo ambao wameona kipindi kichotolewa kujadili taarifa hizi ni kifupi mno na hakitoshi na muda unastahili kuongezwa. Wapo vile vile ambao wamesema Halmashauri za Wilaya zifutwe na wapo ambo wametaka kuwe na list of shame.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hili la mamlaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ningependa tu kurejea kwamba nchi yetu inaongozwa kwa utawala wa sheria na misingi ya utawala bora, ambapo kunakuwa na mgawanyo wa majukumu, lakini vilevile ni kitu ambacho Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amepungukiwa. Tukiangalia mamlaka aliyonayo chini ya ibara ya 143, bila shaka wengi watakubaliana nami kwamba Katiba imempatia mamlaka yanayojitosheleza kwa sababu hata kama taarifa yake isingeletwa na Serikali, yeye kwa mujibu wa ibara ya 143(4), angekuwa na mamlaka ya kuileta.

Mheshimiwa Spika, vilevile tukisoma Katiba pamoja na ile Sheria anayoifanyia kazi Public Audit Act, kifungu cha 27, 28 na 29 vimempa wigo mpana kufanya Forensic Audit, Performance Audit na other audits. Sasa tunapofika hapa ndipo tunaona uwajibishwaji wa watu wale ambao wamepewa dhamana ya kutekeleza majukumu ya Serikali na mashirika yake wanavyowajibishwa kwa njia mbalimbali kwa kufuata misingi yetu ya utawala bora na vilevile kwa kuzingatia nchi yetu ina mgawanyo wa madaraka. Wapo ambao wanatuhumiwa ambao wamebainika na wakachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi ambapo kifungu cha 6(1) kinagatua mamlaka ya kinidhamu kwa Accounting Officers. Kwa hiyo tunapofika mahali hapa mamlaka haya yako mpaka kwa Wakurugenzi wa Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, yawezekana baadhi ya michango watu wanashangaa kuwaona watu mtaani, lakini yule mtu tayari shauri lake lilishachunguzwa na tayari lilishafanyiwa kazi na mamlaka zinazohusika kwa mujibu wa taarifa ya TAKUKURU, kwa mfano kwa 2020/2021, kati ya taarifa walizopokea wao kufanyia kazi kutoka kwa taarifa ya CAG ni 533, taarifa 110 zilifungwa kwa kukosa mashiko. Hii maana yake ilikuwa ni kutekeleza yale majukumu ambayo yapo kisheria, vyombo chunguzi vinapopokea taarifa vinachunguza.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna hatua za kidhamu katika taarifa 102 zilichukuliwa. Kwa hiyo nalisema hili ili kutuhumiwa ni jambo moja, kuthibitishwa na ukosaji au hatia ni jambo lingine na mchakato wa kusikiliza mashauri yenye tuhuma umegatuliwa kikatiba, mahakama kwa upande mmoja kama chombo na mhimili unaosimamia haki wa ngazi ya juu.

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa mujibu wa Ibara yetu ya 13(6) tunajua kuna vyombo vingi pamoja na hao Accounting Officers, hivyo, ningependa ieleweke kwamba tuhuma ni jambo moja na mchkato wa kuthibitisha ni jambo lingine. Mijadala kama hii inavyoendelea inawezekana watu wakaonekana mitaani na ndiyo hao wanasema kwamba ni vizuri waorodheshwe ikibidi waletwe au wakutwe Gerezani kesho, lakini yule mtu kwa mujibu wa Sheria zetu ameshafikishwa mbele ya Mwajiri ambaye ndiye disciplinary authority, akasomewa mashtaka wakaleta utetezi na akatiwa hatiani kwa mujibu wa zile taratibu zilizopo kwenye Sheria ya Utumishi wa Umma pamoja na Public Finance Act.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ningependa kuchangia ni kuhusu habari ya kuongezewa muda, nafikiri hili ni jambo ambalo mimi sioni kama ni baya, kwa sababu hata kwa mujibu wa Ibara ya 143 (3), CAG anachotakiwa ni kuandaa taarifa walau afanye mara moja na kuwasilisha taarifa sasa akiongezewa inakuwa vizuri zaidi, lakini Kamati hizi nazo zikiongezewa muda ni jambo la heri. Pia kuna jambo lingine ambalo limenivutia sana la wale Wabunge wenye kusema Halmashauri zifutwe, ninatambua Waheshimiwa Wabunge wao ni sehemu ya Mabaraza ya Madiwani na wao wapo kwenye Planning and Finance Committees. Kwa hiyo, ningependa ieleweke kwamba ni vizuri sana chochote kinachoazimiwa hapa, vilevile labda na waliohusika kwenye Halmashauri zile kwa ujumla wao, ni vizuri tusiangalie in isolation.

Mheshimiwa Spika, jambo hili ningetamini ingelikuwa ni mimi, Bunge hili lilivyo - live na yale Mabaraza au ngazi ya chini yangekuwa live. Yawezekana ndugu zangu wengine mmeongea hapa, msingeweza kuyaongea kama mlivyoyaongea. Ninapenda kuomba na kuungana na baadhi ya Wabunge wengi ambao wamesema ni vizuri sheria zetu tuendelee kuzihuisha na nipende tu kutoa taarifa kwamba Sheria ya Public Procurement Act tayari inafanyiwa review na wakati wowote kwa mujibu wa taratibu zetu za mkondo wa kutunga sheria na marekebisho, itawasilishwa kwenye Bunge lako kila kitu kitakapokuwa kimekamilika, ni pamoja na sheria zingine ikiwemo ile ya PPP na zinginezo.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na mikataba, vilevile Serikali imeendelea kuchukua hatua ambazo ni mahsusi na nafikiri tumejitahidi kuwa wawazi sana, mmeona tarehe 29 Mwezi wa Tisa mwaka 2022, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo yake kuhusiana na Watendaji ndani ya Serikali kuhakikisha kwamba mikataba yote iingiwe kwa kufuata miongozo pamoja na taratibu ambazo inatuwezesha kama Taifa kuwa na mikataba bora.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naomba niendelee kupongeza chochote kilichoendelea katika mijadala hii ni ombi langu kwamba nia njema iwepo ili tuweze kufikia maendeleo mazuri. Mheshimiwa Shigongo ameelezea yale mafanikio ambayo nchi yetu inaangaliwa na nchi zingine na inavyopimwa, sasa tukisema kwamba hatuna mchango mzuri kama Serikali, Mawaziri hawa hawachangii chochote kidogo inashangaza! Siyo kutetea kwamba kule ambako kuna udhaifu vilevile ni vizuri ukashughuliwa kwa nafasi ile inayokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, mwisho kwa kumalizia, Bunge hili katika majukumu yale tuliyonayo ile Ibara ya 63, mojawapo ni kutunga sheria. Kwa hiyo, ninaomba sana mijadala yote tunayoitoa humu ambayo imekwenda kinyume na sheria zetu wenyewe tulizotunga, unaposema mtu anyongwe na unajua Bunge hili halijatunga sheria ya kunyonga mtu kwa makosa ambayo yapo humu. Nafikiri iwe ni uamsho kwamba tujitahidi sana kuelewa mipaka ya sheria zetu, inatoa nini. Vilevile kuangalia namna ambavyo tutatekeleza majukumu ambayo tunayo, kila muhimili ukitekeleza majukumu yake ili mwisho wa siku wananchi ambao tunawatumikia basi waweze kunufaika na utumishi wetu. Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)