Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nimshukuru Mungu kwa kunipa afya ya kusimama hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia, naomba kwanza niipongeze Wizara hii hasa Mawaziri hawa Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa kufanya kazi hii kubwa na pia nimpongeze Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Labda niseme pia kwa nini natoa pongezi hizi, Makatibu hawa kweli wapo wawili lakini naamini wanafanya kazi kwa umoja wao. Wizara hii imefika kule kwetu ambako kimsingi ni Mbulu Vijijini, wamefika kwenye hospitali ambayo kwa muda mrefu tumekuwa tukiiomba ipandishwe hadhi kuwa hospitali ya Kanda, Hospitali ya Rufaa ya Lutheran ya Haydom. Kwa sababu hii basi kwa kweli napenda kuwashukuru na wananchi wangu waliniambia nikifika hapa cha kwanza niishukuru Wizara hii kwa kufika pale na kuangalia changamoto za Hospitali ya Haydom. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema haya? Nasema haya pia kwa sababu nataka kuleta ombi kwenye Wizara hii tena kwa ajili ya wananchi hawa wa Wilaya ya Mbulu ambao pia Hospitali ya Haydom inazungukwa na inatoa huduma kwa maeneo mengi na mikoa mingi ambayo kimsingi inategemea hospitali hiyo. Kwa hiyo, kwa kuwa hospitali hii inategemewa na mikoa mingi hasa Mkoa wa Singida wanaitegemea Hospitali ya Haydom, Mkoa wa Arusha, Mkoa huu wa Dodoma, Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Mara, niiombe Wizara iendelee kufanya process ya kutosha ili kwa haraka na wakati ufaao tuweze kuipandisha hadhi Hospitali ya Haydom iwe Hospitali ya Kikanda ili iweze kupata msaada kutoka Serikalini wa kuweza kuhudumia maeneo haya yote niliyoyataja. Wako Wabunge hapa wanasikia ninayoyasema, naamini wanakubaliana nami hospitali hii inatibu wananchi wetu wa maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye hotuba ya Waziri ameitaja Hospitali ya Haydom katika ukurasa ule wa 19 kwamba iko kwenye ngazi ya Mkoa, ni kweli. Kwa nini nazungumzia sana hospitali hii? Tatizo lililopo pale katika mkoa wetu, tunayo pia Hospitali ya Mkoa wa Manyara ambayo kimsingi RAS anapoomba maduhuli kwa sababu ya kuisaidia hospitali hii, hawezi kuomba bajeti mbili na kuiombea Hospitali ya Haydom ambayo kimsingi ipo kwenye level moja na hospitali hiyo ya mkoa na hii ya Haydom bado ipo kwenye level ya mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri tunasubiri ujio wake Haydom na watu wanakusikia na ameniahidi atafika Haydom. Namkaribisha sana ili aone juhudi za wale watu wa Haydom tunavyofanya kazi ya kuisaidia hospitali hiyo, karibu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, lipo tatizo ambalo naamini wengi wetu tumesema, tatizo la watumishi. Hili nafikiri ni tatizo la kimfumo hasa kwenye suala la ajira na nani wa kuwasimamia. Wako watumishi wengine wanasimamiwa na halmashauri, wako wengine wanaajiriwa na RAS na wako wengine wanaajiriwa na Wizara. Sasa tuombe itafutwe namna rahisi na nzuri ya kuweza kufanya watumishi hawa wawe na mtu mmoja anayeweza kuwasimamia kwa sababu umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sikufichi, ukitaka kumtuma mbwa muache aende na awe na mtu mmoja wa kumpigia miruzi. Ukimtuma mbwa akatafute mawindo huo ni mfano tu, ukishampigia miruzi na miruzi mingi humpoteza mbwa. Sifananishi hawa wataalam wetu kama mbwa hapana, nina maana kwamba anayepokea order apokee kwa mtu mmoja na hali hii itakuwa nzuri na Wizara yetu ya Afya itaweza kuwa na miguu na watakuwa na ari ya kufanya kazi na kazi hiyo wataifanya kwa uaminifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo lingine la kusema kuhusu call allowance za hawa watumishi wa Wizara ya Afya. Ukiangalia sasa hivi inavyosadikika na inavyosemekana watumishi hawa wanakatwa kodi kwenye call allowance hasa hawa wa private sectors. Kwa hiyo, niombe kama kuna namna yoyote iangaliwe vizuri na kwa sababu sasa hivi Mheshimiwa Rais ameshaamua kuteremsha kiwango kile cha kodi katika mshahara basi tuangalie kwa kina namna gani ya kupunguza basi tozo linalokatwa katika call allowance hasa kwa hizi sekta binafsi. Naomba sana Wizara iangalie sehemu hizi, hizi allowance wanazopewa kwanza ni kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye bajeti mwaka huu inaonekana hapatakuwa na hizi call allowance za kutosha. Kwa hiyo, niombe basi kwa hizi sekta binafsi ambazo zinawapa wale watumishi wao zile call allowance tuangalie vizuri namna ya kuzikatia kodi. Kwa sasa hivi takwimu zinaonesha wanakatiwa kodi kwa asilimia 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tuone namna ya kupunguza zile asilimia ili ile call allowance yule mtu anapomuacha mke wake, kwa mfano Nesi au Daktari anapoitwa usiku, anaacha familia yake, anakwenda kumtibu mgonjwa. Sasa anapopewa zile fedha hizo allowance halafu baadaye inakatwa kodi kubwa kwa asilimia 30, nafikiri siyo sahihi. Tuone ni namna gani ya kuwa-encourage hawa watu hasa wanaohusika na kuzihudumia roho zetu. Kwa hiyo, naomba Wizara iangalie pia sehemu hii kwa umakini na kwa jicho kali kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea kuhusu bima ya afya. Mimi ni mdau mzuri na napenda sana bima ya afya kwa sababu inasaidia wale wanyonge kupata matibabu kwa urahisi. Hata hivyo, bima ya afya iendane pia na upatikanaji wa dawa. Yupo mzungumzaji mmoja amesema kwamba bajeti ya dawa ni ndogo, nimetazama Fungu 52 na nakiri kwa kweli ni ndogo. Nawashawishi Wabunge wenzangu na nawahamasisha tufanye namna yoyote ile, piga ua galagaza, tuisaidie Wizara hii ipate fungu lingine au sijui tufanyaje, tu re-budget ili tuone kwamba tunalipangia hili eneo la dawa pesa zaidi maana uhai ndiyo unaotakiwa katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla muda wangu haujakwisha, nimeona pia Wizara hii inakwenda na Wizara ya Maendeleo ya Jamii. Maendeleo ya Jamii ni Wizara pekee, sisi tumesomea huko, tumechukua digrii zetu huko na wengine tunaendelea kusoma huko. Tukiangalia miundombinu ya hivi Vyuo vya Maendeleo ya Jamii ni mibaya, haifai na ukiangalia kwenye bajeti yetu hapa hasa bajeti ya maendeleo ina zero. Hakika kama tumeshindwa kuvifanya vyuo hivi vikawa ndani ya Wizara hii ya Afya basi tuitengee Wizara! Maana maendeleo ya jamii ndiyo community base ya kuwasaidia watu wetu, wanapomaliza hivi vyuo wanakwenda kuwasaidia wananchi wetu kuwajengea uwezo, kubuni miradi, kuendeleza miradi iwe sustainable.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Chuo cha TICD - Tengeru kimekuwa pale tangu mwaka 1963 kabla ya Muungano, leo hii kuna lami tangu mkoloni pale haijawahi kufanyiwa rebuilding yoyote, hakina maabara, maabara imeanza kujengwa pale miaka tisa haijawahi kumalizika. Mheshimiwa Waziri wa Afya alishakuwa Naibu Waziri wa Wizara hii. Kwa hiyo, niwaombe kabisa mtembelee chuo kile, mkisaidie na muone namna gani special ya kusaidia vyuo hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye vyuo hivi vya FDC wako walimu wanafundisha lakini mishahara yao ni midogo wakati wana elimu sawasawa na walimu wa vyuo vikuu. Kwa hiyo, naomba muangalie walipwe kutokana na elimu zao maana sasa hivi wanalipwa sawasawa na walimu wa sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda wangu umekwisha, basi niombe kabisa kabisa, Mheshimiwa Waziri FDC ndiyo ngome, hawa ndiyo CDO wa kutosha katika nchi hii, ni viraka maana yake anaweza kufanya kazi yoyote, uwasaidie kwa namna yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, lakini kwa consideration ya haya niliyoyasema. Ahsante sana.