Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, nianze kutoa mchango wangu kwanza kabisa kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa namna ambavyo ameendelea kujitoa na kwa namna ambavyo ameendelea kuhakikisha anawafikishia Watanzania huduma mahali popote pale walipo. Lakini pia niendelee kuendelea kuwaomba wale ambao Mheshimiwa Rais amewaamini kama wasaidizi wake, Baraza la Mawaziri Wasaidizi mikoani na wilaya wahakikishe angalau wanakwenda na speed ya mama ili wasiendelee kumwangusha ili Watanzania wapate kile ambacho mama amekusudia kiweze kuwafikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mchango wangu katika maeneo matatu kama muda utakuwa rafiki, nichangie kwenye eneo la Kilimo, Nishati lakini kwenye eneo la Teknolojia namna ambavyo tukitumia teknolojia vizuri inaweza kutusaidia ku-speed up maendeleo lakini pia ambavyo inaweza kusaidia kutoa ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kwenye eneo la kilimo, nitachangia katika maeneo mawili. Suala la kwanza ni kwenye pembejeo kama ambavyo waliotangulia wamesema. Kwa kuwa sisi Tanzania siyo kisiwa, tulipopata janga la Corona Nchi nyingine zilipokuwa zimeathirika automatically na sisi Tanzania tuliathirika hata kama sisi hatukujifungia ndani tuliendelea kufanya kazi. Nchi nyingi ambazo zinazalisha mbolea pamoja na pembejeo zingine zilipata changamoto hizo, kwa ambazo zimepata changamoto hizo imesababisha hata vitendea kazi vya kilimo huko especially mbolea imekuwa ni changamoto. Kwa hiyo, tuiombe sana Serikali ambayo ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali Sikivu sana. Kwa sababu tuna wiki mbili tu tayari tumeshafika kwenye msimu wa kilimo, tunaomba Serikali itoe fedha ya dharula kwa ajili ya ruzuku ya mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili tunaomba kwenye Mpango ambao utakuja baada ya kutoa mawazo yetu 2022/2023, tunaomba viwanda vyetu vya ndani ambavyo vinazalisha mbolea viwezeshwe. Viwanda hivi vikiwezeshwa vitakuja kutusaidia kwenye nyakati kama hivi, hakuna mahali panapoonesha kwenye mpango kwamba baadhi ya viwanda vyetu vitaweza kuwezeshwa ili mbolea ambayo itatoka na kuzalishwa ndani Nchi yetu iweze kuwasaidia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jambo la pili kwenye kilimo nichangie kuhusiana na masoko na hapa naomba niende kabisa soko la DRC Congo. Kwa kuwa mama ameonekana kuwa ni Mwanadiplomasia mzuri na katika kipindi kifupi hiki ameonesha namna ambayo ameionesha dunia kwamba tunaweza tukashirikiana na mataifa mengine. Tumuombe sana Mheshimiwa Rais, atusaidie kukaa na Nchi ya Zambia waweze kutuondolea vile vikwazo ambavyo wafanyabiashara ambao wanategemea soko la Congo wanavipitia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitaka kutoa takwimu ya namna ambavyo soko la Congo linaitegemea Nchi ya Tanzania kwa ajili ya kuwasambazia chakula, unaweza kuona hata zile bilioni 50 ambazo tulipoiomba Serikali tulipoleta hoja hapa waliweza kutusaidia, tusingeweza kwenda kuitumia kwa ajili ya kununua mahindi kwa Watanzania, soko la Congo peke yake lilikuwa linatosha wafanyabiashara kununua mahindi ya kutosha na kupeleka Congo au kusindika unga wa mahindi na kusambaza kule. Soko la Congo linatamani Watanzania sisi tuwa-supply tani za unga kuanzia laki moja na hamsini mpaka laki nne. Na inaweze hapo tunaongelea Congo Lubumbashi peke yake labda Katanga na Kolowezi lakini hapo hatuongelei Congo Kinshasa, hatuongelei Goma ni hiyo Congo Lubumbashi peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa vikwazo hivi vitaendelea, vinaendela kuwanyima nguvu wananchi ambao wanazalisha mazao ya nafaka especially wale ambao wanatokea Nyanda za Juu Kusini mikoa yote saba. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali itafuta namna nzuri ambayo itakaa na Nchi ya Zambia waelewane vile vikwazo ambavyo wafanyabiashara wanapata na kwenye biashara nyingine viweze kuondoka ili tuweze kutumia kwa sababu mizigo mingi ambayo inatoka Tanzania inakwenda kama transit. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa kumalizia niongelee suala la teknolojia. Suala la teknolojia, teknolojia ni kama muda hauwezi kushindana na muda, wewe unapotaka kushindana na muda wewe utapitwa na wakati. Unaweza ukaona, sasa hivi hata Bunge letu vitu vingi tunaendesha kwa kutumia kishkwambi, lakini unaweza ukaona Nchi ambazo zimeendelea teknolojia hii ilipaswa itumike kwenye Bunge la Nane, Bunge la Tisa au Bunge la Kumi. Lakini tupo Bunge la Kumi na Mbili mwaka 2021 ndiyo tunatumia teknolojia hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa kwenye teknolojia nataka niongelee kuna kitu kinaitwa Block Chain Technology na kwenye Block Chain Technology nataka nitoe takwimu ndogo tu ikiwa kama Nchi zetu zitatamani kuendana na kasi ya teknolojia iliyopo duniani, tusiwe tunachelewa kupokea teknolojia, mambo ambayo tunapaswa kuyafanya sasa hivi tunakuja kuyafanya baada ya miaka kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu turudi miaka kumi iliyopita nyuma mwaka 2010. Mwaka 2010 wakati teknolojia ya Block Chain Technology inakuja, ndani ya Block Chain Technology kuna vitu vingi, watu wa kada mbalimbali wanaweze wakatumia Block Chain Technology lakini hapa niongelee suala la fedha ambalo naamini kila mtanzania tunafanya kazi ili tuweze kupata fedha. Ndani ya Block Chain Technology kuna kitu kinaitwa Digital Currency, Crypto Currency yaani BitCoin. Mwaka 2010 bitcoin ilikuwa inauzwa chini ya dola 5, ilikuwa inauzwa 0.5 USD ambapo mwaka 2010 dola ya Kimarekani ukilinganisha na fedha yetu ya Tanzania ilikuwa inakwenda kwenye 1,490 – 1500.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa tafsiri yake kama Serikali ingesema sisi tumeilewa hii idea hebu tujaribu tu tuchukue bilioni 1 tuwekeze hapa kama vile ambavyo wananunua hisa na nimegundua inawezekana hata IMF hizi Benki za Dunia wanavyotukopesha wao wanawekeza kwenye vitu kama hivi halafu sisi ndiyo wanakuja kutukopesha tunabaki tunalipa madeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali ingeamua kuchukua bilioni moja ikanunua bitcoin ambayo ilikuwa ni Dola 0.5 ya Kimarekani ukizidisha na thamani ya dola kipindi kile unapata kama 750 maana yake bilioni 1 ukigawanya kwa hiyo fedha unakuja kupata bitcoin laki moja ama elfu thelathini na tano hivi. Ukizidisha na bei ya sasa ya bitcoin, bei ya bitcoin ya sasa ni dola za Kimarekani 66,000 ambapo almost na fedha ya Kitanzania kama Milioni mia moja na hamsini na.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani tafsiri yake kama Serikali sasa hivi ingeamua kuziuza hizo bitcoin laki moja na thelathini na tano n.k. tungekuwa na uwezo wa kulipa hilo deni la Taifa ambalo tunadaiwa sasa hivi hizo trilioni 70 na. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu bei ya bitcoin sasa hivi ukizidisha na kama Serikali ingenunua bitcoin kipindi hicho inakuja karibu trilion 90. Kwa hiyo, unaweza kuona namna gani hatuwekezi kwenye teknolojia tunapitwa, 2010 na sasa tulipo siyo muda mrefu. Unaopomuongelea Mwekezaji kama Mark Zuckerberg’s ambaye ndiyo mwanzilishi wa Facebook na sasa hivi hi WhatsApp kama kuna Watanzania 10 tu wangekwenda kununua hiza kwenye kampuni yake hata wakawa na share mojamoja sasa hivi ndiyo trillionaire.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuangalie namna gani tunaweza tukawekeza kwenye teknolojia na ni maombi yangu na mapendekezo yangu, vijana wengi wa Kitanzania waliopo huko na nilipata nafasi kufanya research kwenye nchi za West Africa mwaka 2016/2017. Kipindi kile Nchi za Nigeria zilikuwa zina burn sana mambo haya ya cryptocurrency lakini sasa hivi tunavyoongea muda huu hata ukiongea na Ubalozi wa Tanzania nchini Nigeria. Nigeria wamepitisha cryptocurrency bitcoin ni miongoni mwa fedha ambayo inatumika na wameweka katika mfumo mzuri hata kwa kutumia local network za Nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hata Mnigeria asiyejua kusoma ambaye hana uwezo hawezi kutumia internet anaweza akafanya, kwa hiyo ni kitu ambacho katika mpango huu tunaomba kuona Tanzania waisome teknolojia ya Block Chain Technology ili waweze kuiwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kwenye nishati. Kwa kweli sisi Wabunge ambao tunatokea vijijini kwenye umeme, kwa kweli kauli hii ambayo Serikali inasema sana umeme mpaka kwenye vitongoji inatutesa huko vijijini. Sera ya Serikali inasema kwenye kila Kijiji kilometa moja ya nguzo ambazo ziweze kupita. Lakini unagundua...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. CONDESTER M. SICHWALE: Dakika moja tu.

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. CONDESTER M. SICHWALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini unagundua kwamba umeme haupiti kwenye nyumba kama inavyotakikana kwa hiyo wananchi wanajiulia hiyo umeme kwa kila Kitongoji imekuwaje? Na vijiji vingine ni vikubwa ina vitongoji vikubwa kwa hiyo, bado hii kauli inatupa mkanganyiko wananchi wakisikia umeme kwa kila Kitongoji lakini ukienda uhalisia kule umeme kwa kila Kitongoji hakuna.

Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali iliangalie jambo hili ikiwezekana umeme kwenye kila Kijiji angalau nguzo kilometa tatu. Ahsante sana. (Makofi)