Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Abdullah Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mahonda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Natoa shukrani zangu za dhati kwa kunipatia wasaa kuchangia huu Mpango kwa dakika chache ambazo tunazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na uzima na kuwepo leo hii. Pili, kuwashukuru Kamati kwa uchambuzi wao mzuri na kuainisha yale ambayo sisi kama Wabunge tuyatazame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri au mbaya Mheshimiwa Nape Nnauye na wewe mwenyewe kwa sehemu kubwa mmenifilisi yale ambayo nataka kuyazungumza, lakini nitagusia mambo fulani fulani kuzungumza kiini cha nini tunachotaka kukifanya na katika kilimo tutazame maeneo gani ili tuboreshe Mpango na tuboreshe maisha ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, athari za UVIKO-19 ni mtambuka. UVIKO-19 umetuathiri kiafya, kiuchumi na kijamii. Maisha ya walimwengu yamebadilika kama vile usafiri wa anga ulivyobadilika baada ya matukio ya Osama Bin Laden, usafiri wa anga umebadilika kabisa na UVIKO-19 maisha yetu ndani ya ulimwengu huu tuliokuwa nao hayawezi kurudi kama yalivyokuwa mwanzo. Athari zake zimekuwa kubwa ulimwengu mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sayansi inatuambia kwamba UVIKO-19 ni janga ambalo ni la kibaguzi, linaathiri rika tofauti, linaathiri watu wenye maradhi sugu tofauti, linaathiri maskini tofauti. Kwa hiyo lazima janga hili na utaratibu wetu wote huu tuliokuwa nao tuuangalie kwa utofauti wake ambao unaathiri sehemu mbalimbali. Kwa mantiki hiyo basi, tiba ya janga la UVIKO-19 ambayo ndiyo maudhui yetu yote haya ya hizi fedha tulizopewa, lazima ziangaliwe kwa maeneo ambayo limetuathiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu kwa ujumla maneno yote yanayozungumzwa; mpango wetu na mipango yetu yote imepangwa na imelenga kutatua mambo makuu matatu. Mambo hayo makuu matatu ambayo Mwasisi wetu wa Tanzania hii amepambana nayo na sisi tunaendelea kupambana nayo; mambo makuu matatu ni yapi? Adui ujinga, adui maradhi na adui umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu ukiutazama umelenga kutatua na umepambana na maadui wawili tu; adui ujinga na adui maradhi. Ukiangalia kipaumbele katika afya, kuna intervention kubwa sana kwenye afya. Ukiangalia kwenye afya kuna intervention kubwa, lakini umaskini haujaguswa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umaskini kwa Tanzania ni nini? Umaskini ni kilimo. Mheshimiwa Nape amezungumza vizuri katika hilo, lakini ningependa tu kugusia kilimo katika maeneo gani. Wajumbe wengi hapa wamezungumzia kilimo katika sehemu moja, lakini kilimo ukikiangalia na athari zake ni sehemu kuu tatu. Kilimo awali, sehemu ya kwanza ya kilimo ni mbolea, mbegu bora, maji ya kumwagilia na kupanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu kuu ya kilimo ya pili ni, Waingereza wanasema post-harvest losses, athari inayotokea baada ya kupata mazao yao. Asilimia 40 ya hasara yetu katika kilimo inapatikana baada ya kupata mazao na sehemu kuu ya tatu ni masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili tuweze kuhimili hili janga la umaskini, ili tupambane na adui maskini kwa kupitia njia ya kilimo tuna mambo ya msingi matatu ya kufanya. Na hayo lazima Serikali kupitia mpango huu iwekeze katika hayo makuu matatu ili kupata tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka iliyopita kabla ya mapinduzi yaliyotokea ya kisera, nitayasema Zimbabwe, hakuna nchi ulimwenguni ambayo ilikuwa inafanya vizuri katika sekta ya kilimo kama Zimbabwe. Nasema ulimwenguni, kwa nini? Zimbabwe ndiyo nchi pekee ambayo haikuweka ruzuku katika sekta ya kilimo. Kilimo chao kilikuwa kinakwenda kibiashara, mazao yakawa rahisi, faida ikawa kubwa. Nini wamekifanya Zimbabwe ambacho sisi tunaweza kuiga tukafika huko walikofika wao? Hilo ndilo jambo la kwanza la kutazama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa walilolifanya Zimbabwe, unajua Nchi yetu ya Tanzania kwanza imejipanga vizuri zaidi kushinda Zimbabwe, kwa sababu kuna maeneo ambayo yako juu kama Nyanda za Juu Kusini, halafu kuna mabonde yanatiririka mpaka kwenye bahari na mito mingi inakwenda mpaka kwenye bahari. Jambo kuu ambalo Zimbabwe waliweza kufanya ni kuweka mabwawa. Kwa hiyo, focus iwe kuweka mabwawa ili tuweze kuwa na maji ya kufanya irrigation. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kisayansi imethibitishwa na hiyo ndiyo njia rahisi zaidi kuathiri sekta ya kilimo; mabwawa. Zimbabwe watu waliobahatika kufika Zimbabwe, utabiri wa hali ya hewa kila siku asubuhi na jioni mtaambiwa leo kutakuwa kuna mvua, lakini bwawa hili liko asilimia 50 limejaa, bwawa lile asilimia 75 limejaa, bwawa lile kule asilimia 100. Ilikuwa sehemu ya msingi kabisa katika uhai wa Nchi ya Zimbabwe. Sisi pia tujikite kwenye mabwawa zaidi kushinda visima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, post-harvest losses, tatizo lake nini? Ni maghala. Tuweke maghala, tuweke cold storage. Kwa sababu haya yatafanya mambo mawili makuu; kwanza tutaokoa yale mazao ambayo tumeshayavuna, lakini pili, maghala ndiyo center ya mauzo, ita-solve tatizo la tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwenye maghala kutakuwa kuna wataalam wa vipimo, wanasema bwana mpunga wetu huu ni wa grade hii, unawekwa kwenye mtandao ili mnunuzi asipate taabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, hakuna tatizo la soko, tatizo la soko halipo, kila kitu kinahitajika. Tatizo lililopo ni ufikishaji sokoni. Teknolojia tunayo ambayo inaweza kuondoa hilo tatizo kabisa. Teknolojia ipo, tunaweza kulipa kimtandao; teknolojia ipo ambayo tunaweza kununua na ku-grade kila kitu kimtandao. Sasa tuta-solve mambo makuu mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda kuishauri Wizara ya Fedha kutazama upya, kama wengi walivyosema, suala la kilimo, lakini maeneo makuu ambayo tunapenda yaangaliwe na yatiliwe mkazo mkubwa kabisa ni mabwawa ya maji ndani ya nchi yetu, ghala na cold storage investment ndani ya nchi yetu na mtandao wa kuwezesha sisi kuuza na kuhakikisha watu wote na sekta hii inaboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nashukuru sana. (Makofi)