Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika

Hon. Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye hoja hii muhimu ya kuridhia Azimio la Eneo Huru la Biashara Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nianze kwa kuunga mkono hoja, na kimsingi kama ambavyo wajumbe wengi wamesema labda na mimi niseme tu kidogo. Eneo Huru la Biashara Afrika ni utaratibu wa pamoja wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika unaolenga kuchochea uchumi na biashara miongoni mwa nchi wanachama.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kama walivyochangia wachangiaji wengi na kukubaliana na Azimio hili, lengo hasa litakuwa ni kufunguliana masoko ya biashara ya bidhaa na huduma, kuondeleana ushuru wa forodha, pamoja na kulegeza vikwazo na masharti mbalimbali ili kuhakikisha Afrika tunafanya biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji wengi wamekubaliana, lakini wametoa baadhi ya maoni kwa upande wa Serikali. Na mimi kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba maoni haya tunayachukua na moja ya mikakati ambayo tunaenda kuitekeleza ni kuhakikisha tunaendeleza kuimarisha mazingira bora au wezeshi ya kufanya biashara katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia katika hilo kweli kulikuwa kuna changamoto kidogo, kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge, na tuliona baadhi ya hata wafanyabiashara wakubwa wakiondoka, wakiondoa mitaji yao na kuwekeza katika nchi zingine, lakini sasa baada ya maboresho yanayoendelea hasa kupitia blue print kama mlivyosema Waheshimiwa Wabunge tunaona tayari wawekezaji wengi wanaanza kurudi kuwekeza hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, maana yake hili ni move nzuri ambayo na sisi tuitumie nafasi hii sasa kuvutia mitaji mingi kwa kuweka mazingira wezeshi ili tuanze kuzalisha nchini na kuuza katika eneo hili la biashara la Afrika kwa faida zaidi kulingana na utaratibu tunaoendana nao sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, wameongelea kuhusiana na kuhakikisha sekta binafsi inawezeshwa au inashirikishwa. Hili tunalichukua na kuhakikisha kweli sasa tunaenda ku-engage; na kama ulivyosema wengine tayari sekta binafsi imeshasema faida kubwa ambayo wataenda kuipata au manufaa makubwa ya Tanzania kuridhia mkataba huu wa eneo huru la biashara Afrika, kwamba wao wataenda kufaidika Zaidi, na ni wengi wamesema.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tutaendelea kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa ndani na hasa kwenye kukidhi viwango, kwa maana ya kuhakikisha unahamasisha uzalishaji wa tija kwenye bidhaa zetu lakini na mazao. Kama walivyosema wengine, kwamba angalau sasa bidhaa zetu na mazao yetu yawe shindani kulingana na soko la sasa, lakini hasa kwenye hili soko la Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, wameongelea kuhusiana na sekta ya biashara ndogo, kwamba lazima hawa nao pia tuendelee kuwawezesha. Ni kweli, tuhakikishe sasa sekta ndogo kwa maana wajasiliamali waweze kuzalisha kibiashara kwa kuhakikisha kwamba vifungashio vyao vinakuwa vya viwango, lakini pia hata ubora; na hii tunaenda kuhakikisha tunafanya hivyo kwa sababu sasa hivi tunaenda kuandaa sera ya ubora. Tuwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba tutaenda kutekeleza au tutaingia tukiwa na nguvu katika soko hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwa ujumla wake Waheshimiwa Wabunge wameongelea sana kuhusiana na umuhimu wa sisi kama Bara la Afrika kuanza sasa kuishi pamoja, kwa maana ya kufanya biashara pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli changamoto mojawapo kubwa sana katika kufanya biashara katika bara letu ni miundombinu. Kwa mfano; utakuta mtu anataka kwenda labda hata Kongo tu hapo, kama kwa njia ya ndege maana yake lazima uende Ethiopia au hata nchi za nje ili kesho yake ulale, uje Kongo, DRC. Sasa unakuta miundombinu hii ndiyo imekuwa na changamoto kubwa sana ya sisi kwenye kufanya biashara katika Bara la Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo moja wapo ya vitu ambavyo vitaenda kutupelekea kuhakikisha sasa tunaimarisha miundombinu yetu hii ni moja ya fursa ambayo naamini, kama alivyosema Mheshimiwa Mwijage na mwingine, kwamba sasa miundombinu hii itajengwa kwa sababu tunajua tunakwenda kufanya biashara kati ya nchi na nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili pia, naona kwa mfano; hata kwenye njia tu za barabara watu wanaouza mazao mbalimbali ikiwemo hata mbao kupeleka Kongo badala ya kukatisha hapa tunaenda mpaka Zambia halafu uanze kurudi hivi. Maana yake kwa miundombinu hii inapelekea bidhaa zetu kuwa uncompetitive, kwamba zitakuwa sasa haziwezi kushindana na bidhaa hata za kutoka ulaya kwa sababu ya miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niwaombe, kama ambavyo wote wamekubali, kwamba tuunge mkono Azimio hili kwa sababu lina manufaa mengi kwa nchi yetu, lakini pia kwa Bara zima la Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)