Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kimsingi mimi nianze kwa kuunga hoja mkono. Naunga mkono hoja ili nisije nikasahau huko mbeleni. Nianze mchango wangu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania sasa tunapaswa kubadilika. Tuanze sisi viongozi na Watanzania wote kwa ujumla, tunabadilikaje? Ninavyozungumzia kubadilika namaanisha kwamba tunapaswa kufikiri kimkakati, yaani kila mmoja wetu afikiri kimkakati. Kufikiri kimkakati kutatusaidia kwa sababu kwanza tunakaribisha ushindani na kwenye ushindani maana yake anayeweza kuwa na uwezo katika kushinda atashinda tu, na sisi kwa bahati mbaya sasa, kwasababu hii ni fursa kwetu inaweza ikawa bahati mbaya kwetu sisi tukawa walaji na si wauzaji. Sasa lazima tufikiri kimkakati wote kwa pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Uwekezaji pamoja na Wizara yetu ya Mambo ya Nje. Nianze na Wizara ya Mambo ya Nje. Tuna Balozi mbalimbali kwenye nchi mbalimbali hapa Afrika, Balozi zetu sasa nazo zifikiri kimkakati. Tunao Mabalozi, lakini pia tuna maafisa ambao wapo Ubalozini. Je? tunaowapeleka kule; nimuombe pia Waziri wa Mambo ya Nje, tutazame wale maafisa wetu waliopo huko nje wapo kimkakati? Au tunawapeleka tu kwa sababu waende kutoa huduma kwenye balozi hizo. Nadhani nao tungepaswa kuwapeleka watu ambao wanakwenda kuwa Mabalozi na maafisa ambao wapo kimkakati. Lakini pia na Balozi zetu pia zitumike kimkakati ili kuboresha biashara huko nje ya nchi ambako Balozi zetu zipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende eneo lingine. Nimezungumzia Wizara ya Viwanda na Biashara. Wizara ya Viwanda na Biashara sasa tubadilike na sisi tuwe walezi wa wafanyabiashara wa ndani ya nchi yetu. Kwa mfano; tunaona mtu kama Bakhresa, Azam ukienda takriban nchi zote za SADC anafanya biashara huko, tunaona mfano mzuri. Vilevile tunaona benki ya CRDB leo wapo Burundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu hawa wanapaswa kulelewa, na wakilelewa hawa wachache wengine watavutiwa na wakivutiwa wengine maana yake pia itaongeza wigo mpana kwa wale wawekezaji nje ya nchi hizi ndani ya Bara letu la Afrika. Kwa hiyo Wizara ya Viwanda na Biashara sasa mnaweza kuwa walezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri ni wenzetu China. Kampuni zote za ujenzi zinazokuja kujenga hapa Tanzania kutoka China zinakuwa funded na nchi zao, na China. Zenyewe zinapambana kutafuta tender zikipata tender zinakwenda kwao wanapewa fedha kwa ajili ya kuendelea na miradi ya ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na sisi yamkini tukashindwa kuwapa fedha hawa wafanyabiashara ndani ya nchi yetu, lakini tuwa-guarantee tu, tunaweza kuwapa dhamana tu, kwamba Serikali ikawa dhamana ya Watanzania wanaokwenda kufanya biashara ndani ya Bara letu la Afrika. Hii itasaidia kwenda kwenye ushindani ambao na sisi utatupa manufaa makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo lingine nizungumzie suala zima la taasisi za kifedha. Ukiitazama Kenya wana benki kadhaa hapa nchini ikiwemo KCB. Tujiulize Tanzania tuna benki gani kule Kenya? Sasa haya ni maswali ambayo kimsingi yanapaswa kutufikirisha ili na sisi tujipange kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia haitoshi, eneo lingine ni kuhusu suala zima la Sera na Sheria zetu, je, sera zetu na sheria zipo katika mtazamo ambao unaweza kutusaidia kama nchi kunufaika na mkataba huu?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo haya ni mambo ambayo nadhani kimsingi tunakwenda kwenye ushindani ambao kimsingi lazima tujiandae. Kwa mfano; tunaweza kuanza na jambo la tunatazama tu kwenye comparative advantage. Kwamba sisi kama Watanzania ni eneo gani tumekuwa mabingwa kwenye uzalishaji na tukatumia eneo hilo kutusaidia ku-compete na wenzetu, mathalani kwenye mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, imezungumzwa hapa, na leo tumepata changamoto hapa, ni jambo ambalo wengine watatushangaa. Tukiwa tunajadili kununua mahindi leo hii, yaani dunia inatushangaa, dunia ingetutazama sisi tukiwa tunajadili kuuza unga, kwamba tayari tumeshafanya processing na si mahindi. Sasa tukiona tunafikiri kujadili mahindi tutoke kujadili mahindi tujadili bidhaa ambayo inakwenda kuuzwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, huko Kenya tunakopeleka mahindi tunapata hasara kubwa sisi, hilo lazima mjue. Tunapata hasara kubwa kwa sababu unauza mahindi, kuna pumba na yana vitu vingi ambavyo tunavipeleka Kenya. Kwa hiyo tusiendelee kuuza raw materials tupeleke bidhaa ambazo tayari zimeandaliwa nchini. Na hili haliwezi kufanywa na Serikali, Serikali ibaki kuwa regulator na sekta binafsi sasa iende kwenye ku-capture production. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninayasema haya lengo langu likiwa ni kuona kwamba kama nchi tunakwenda kunufaika na mkataba huu wa eneo huru la biashara ndani ya Bara letu la Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika haya narudia kusema kwamba inawezekana, inawezekana tukifikiri kimkakati, na kufikiri kimkakati kutatuwezesha sisi kwenda kuwa washindani kwenye eneo huru la biashara ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)