Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nianze kwa kuunga mkono hoja ya Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Nchi za Afrika. Kwa kweli nafikiri hili Azimio limekuja kwa wakati wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kulileta Azimio hili ambalo ni muhimu sana, lakini pia naipongeza sana Kamati ya Viwanda na Biashara kwa kuchambua kwa undani sana Azimio hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ina historia ndefu. Nchi yetu imekuwa ni nchi ambayo iliongoza mapambano ya ukombozi wa Afrika wa kisiasa na nchi zetu zote zimepata sasa uhuru, lakini tunabaki nyuma katika kuongoza mapambano ya ukombozi wa kiuchumi, Sasa hili Azimio lengo ni kuleta ukombozi wa kiuchumi. Ndiyo maana lengo la Azimio hili ni kuchochea uchumi na biashara katika nchi za Afrika. Kwa hiyo, mimi nafikiri ni wazo ambalo ni zuri sana.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu tusibaki nyuma, kila wakati tunatakiwa tuwe mbele, kama tulivyoongoza mapambano ya kupata uhuru tuongoze na mapambano ya kuleta uhuru wa kiuchumi. Kwa hiyo, hili mimi nafikiri lazima tuwe mbele. Pili, nchi yetu imekaa kijiografia mahali pazuri (strategically located). Sasa lazima tutumie fursa hii ya nchi yetu kuwa strategically located ili tuweze kunufaika na biashara ya nchi hizi ambazo tumezisaidia sana katika kuleta ukombozi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukua hali ya biashara Bara la Afrika linatisha. Sisi tunafanya biashara katika nchi za Afrika kwa asilimia 17, nchi za Ulaya asilimia 69, nchi za Asia asilimia 60, Mabara mengine yote ni zaidi ya asilimia 60. Kwa hiyo, umefika wakati lazima tufanye biashara na sisi, tufufue tuweze kufanya vizuri. Na mimi ninaamini hili litatusaidia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninao mfano hai. Nimeona kwa mfano wananchi wa kule Songwe wanavyopata shida hasa inapokuja katika kufanya biashara na nchi za jirani. Tuko pale karibu tunapakana na Malawi na Zambia, tuko ni lango la SADC lakini tunapata shida kwa sababu ya kutokuwa na misingi na mambo mazuri ya kufanya biashara katika hizi nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano pale Tunduma unakuta kwamba wananchi wanaagiza mbolea Zambia, ina bei ya chini sana, iko bei ya chini kabisa, lakini ukichukua mbegu ziko bei ya chini sana na ziko mbegu nzuri kabisa zinazofaa kwenye kilimo. Wananchi wale wakienda kununua kule wanapoziingiza Tanzania wanavyofukuzwa, wanavyokamatwa utafikiri wamefanya uhaini. Kwa hiyo, hili suala mimi nafikiri kwamba tukianzisha haya maeneo yanatusaidia sana katika kuweza kutuachia biashara katika maeneo ya namna hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo ambayo lazima tuyazingatie na Mheshimiwa Waziri na Serikali lazima tufanye kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba tunahamasisha ili nchi yetu iweze kupata manufaa ya hili Azimio.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ni tija. Tija katika bidhaa zetu kwenye kilimo iko chini, kama wenzangu walivyosema. Tija kwenye bidhaa zetu iko chini, bidhaa zetu haziwezi kushindana na bidhaa kutoka maeneo mengine. Kwa hiyo ni wajibu wetu sisi kuhakikisha kwamba tunaongeza tija ili bei iwe nzuri ili zi-meet ubora unaotakiwa wa kuweza kushindana katika hii biashara. Mimi naamini hiyo itatusaidia sana tukiweza kuifanya hivyo. Wameweka mifano ya bidhaa za kilimo, wameweka bidhaa mbalimbali mimi sitaki kurudia, lakini nataka kusema kwamba hilo ni suala la msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, tunapoenda kufanya biashara swali ambalo ni lazima tujiulize ni biashara ya namna gani tunakwenda kufanya. Tunasema kama ni biashara ya kuuza malighafi hiyo ni biashara mbaya. Biashara inatakiwa ukauze bidhaa zilizoongezwa thamani, hiyo ndiyo biashara ambayo inatakiwa tuingine nayo katika Bara la Afrika. Hapa tusijipe moyo kwamba tunakwenda kuuza malighafi au tunakwenda kufanya nini, hiyo haitatusaidia kwa sababu tunayo matatizo ya msingi katika nchi hii ambayo ni kupunguza umaskini na kutengeneza ajira kwa watu wetu. Ili tuweze kufikia hayo yote lazima tujenge viwanda imara, tuongeze thamani ya bidhaa zetu, ndiyo tutaweza kutoa ajira na ndiyo tutaweza kupunguza umaskini wa watu wetu katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, mimi nafikiri mkazo lazima uwe katika kuongeza thamani ya mazao yetu, ndiyo tutaweza kushindana vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo eneo lingine katika nchi za Afrika ambalo lazima tubadilike kifikra. Tuanze kujenga uaminifu, Waafrika walio wengi si waaminifu. Katika biashara sasa hivi tunazoenda kushindana tunaenda kushindana na baadhi ya nchi wapo watu ambao si waaminifu. Kwa hiyo na sisi lazima tujitahadhari na watu wetu wawe waaminifu. Ujue kabisa kwamba ukikopa unatakiwa ulipe, ukifanya biashara, ukiingia mkataba u-deliver. Kama inatakiwa upeleke bidhaa ndani ya wiki moja upeleke ndani ya wiki moja. Tukiendelea na uswahili wetu ambao tumeuzoea huu mimi nadhani kwamba hatutaweza kufanikiwa na kuona manufaa mapana ya azimio hili ambalo nafikiri ni muhimu sana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nataka kusema kwamba hili Azimio limekuja kwa wakati muafaka tuliunge mkono, tushikamane na Serikali tuhakikishe kwamba kweli tunaenda kunufaika na Azimio hili na wananchi wetu waandaliwe vizuri, wapewe elimu ya kutosha ili waende sasa, twende tukafanye biashara katika hizi nchi za Afrika na sisi tufungue mipaka na masoko ya bidhaa zetu yapatikane.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)