Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Bahati Khamis Kombo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza, nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia kutupa uhai na uzima na tukaweza kufika hapa tukiwa katika hali ya salama na amani kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru tena wewe kwa kunipa nafasi hii ikiwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge letu hili Tukufu. Nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa kuwa ni Rais wetu na akiwa ni mwanamama. Niseme tu mwanamama huyu ni hodari mno na ni shujaa. Tunamuombea dua Mwenyezi Mungu amjalie azidi kuimarika zaidi. Mama yetu koleza majani ya chai na kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee moja kwa moja katika bajeti yetu. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wa Fedha kwa kutuletea bajeti hii ambayo imewagusa Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja katika upande wa TASAF, naipongeza Serikali yetu kwa kutenga tena bajeti ya kutuletea miradi hii ya TASAF. Kwa kweli miradi hii imesaidia sana kaya zetu maskini na tuna imani kwamba kwa bajeti hii itazidi kuimarika zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwa upande wa Zanzibar, ripoti imeonyesha kwamba Zanzibar imefanya vizuri. Naipongeza sana Serikali yangu ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kufanya vizuri katika kusimamia miradi hii ya TASAF, lakini pia pongezi zaidi ziende kwa wasimamizi wakuu walioweza kuisimamia TASAF Zanzibar na tukaweza kufikia lengo kuu lililokusudiwa na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja katika mchango wangu wangu wa pili kwa upande wa Jeshi letu la Polisi. Mheshimiwa Waziri hapa amegusia changamoto ya Jeshi la Polisi. Nimwambie tu Mheshimiwa Waziri waende wakaitatue changamoto hii kwani Jeshi letu la Polisi linafanya kazi nyingi usiku na mchana bila kujali mvua au jua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha akae makini anisikilize katika jambo hili moja ambalo naomba kulichangia. Jeshi letu la Polisi, kuna fedha ambazo wanazikosa, hawa wenzetu baadhi yao natoa mfano; mwanajeshi huyu anapokea shilingi 565,000 anatakiwa apewe asilimia 15 ya mshahara wake ikiwa ni posho la pango. La kusikitisha mwanajeshi huyu anatakiwa apewe shilingi 84,750, lakini posho anayopewa ni shilingi 40,545. Mheshimiwa Waziri aende akakae na Waziri mwenzake ili waweze kuitatua changamoto hii Jeshi letu liweze kufanya kazi likiwa na ufanisi mzuri na hii haki yao ya posho waweze kuipata kwa mujibu wa utaratibu uliopangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu sina la ziada ila nampongeza tena mama yetu Mama Samia, niwaambie Waheshimiwa Wabunge tunapompongeza mama tunamsahau baba, tumpongeze na baba yetu kwani yeye ndiye anayempa maliwazo mazuri na akaweza kutuongoza vizuri. Nakushukuru. (Makofi)