Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa hii nafasi niwe miongoni mwa watu ambao watachangia Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, kwanza anianze kwa kumpongeza Waziri kwa kazi nzuri yeye na Naibu wake, Katibu Mkuu kwa kweli wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wananchi wetu wanapata mwanga ingawa kuna changamoto. Lakini pia niwapongeze viongozi wa REA, DG wa REA naye anafanya kazi nzuri kuhakikisha anasambaza umeme na sisi tunajivunia kuwa na DG huyu kwa sababu umeme kweli umefika katika vijiji mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo bado tuna changamoto nilipochaguliwa na wananchi wa Jimbo la Igalula nilikuja hapa kujua hatma ya vijiji vyangu ambavyo bado havijafikiwa na nishati ya umeme na uzuri Mheshimiwa Waziri alinijibu Bungeni na bado tukafanya naye safari ya kwenda kwa wananchi wangu kuwaambia lini umeme utawafikia wananchi wangu. Hilo nilikushukuru sana Mheshimiwa Waziri, tulifika katika Kijiji cha Izumba, Kata ya Miyenze na ulikuta watu wengi, walikupokea kwa furaha kwa sababu walijua wewe ulikuja na umeme. Lakini matarajio yao hayakuwa kama tulivyokuwa tumetarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakumbuka na naomba nikunukuu na siku ile tulikuwa wote wewe Waziri na Naibu wako na Mkurugenzi wa REA naye alikuwepo na Bodi yako yote ya REA ilikuwepo. Uliwaambia wananchi ilikuwa tarehe 16 Machi ukawahakikishia kufikia mwisho wa mwezi wa nne umeme Izumba utakuwa umewaka na ukawahakikishia ukasema leo umekuja na wakandarasi utawaacha pale pale ili waanze kuwasambazia wananchi umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ni mwezi Juni tarehe 2, 2021; wananchi wa Izumba hawajaona nguzo, yule mkandarasi tulivyoondoka na yeye akaondoka, sasa hivi amebaki anakwenda anaondoka. Nikuombe Mheshimiwa Waziri tunamaliza Bunge tarehe 30 ya mwezi Juni, 2021 ninakwenda ziara kule sasa kama nikizomewa ujue umenisababishia wewe ule mzomeo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nikuombe Mheshimiwa Waziri kwa hizi siku chache naomba uniwashie umeme, nikiunganishi kati ya wananchi na Serikali, ninapokwenda kule tena kuwaambia nitaenda kuiambia Serikali wakati Serikali ndiyo niliipeleka kweli Mheshimiwa Waziri utanipa wakati mgumu mwisho wake na mimi nitakuwa upande wa Serikali nikabaki nashangaa kauli ya Serikali haijatimizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri, wananchi wa Kata za Miyenze, Tura, Miswaki na Lutende wote wanahitaji na wanamatumaini makubwa ya kupatiwa umeme, naomba uwasaidie kwa sababu ulitoa kauli hiyo kwa bashishi kubwa na wao wakakupigia makofi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada za Serikali kutupelekea umeme, mkandarasi amekwenda kwenye baadhi ya vijiji ameenda kuwashirikisha Waheshimiwa Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji wakisema jiandaeni umeme unakuja. Lakini mkandarasi anasema mimi nitaleta umeme, nitasambaza kilometa moja tu kwenye kijiji.

Mheshimiwa Spika, mimi niiombe Serikali pamoja na nia njema ya kupeleka umeme, msitupelekee mgogoro mwingine ambao utazalika ndani ya mgogoro mwingine kwa sababu unapopeleka kilometa moja na mkaweka idadi ya watu labda 20 wataunganishiwa wakati watu ambao wapo tayari kuunganishiwa umeme zaidi ya 20.

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kama yule mkandarasi mnampa mkataba wa kilometa moja muwe mna fedha za ziada anapomaliza kilometa moja TANESCO anaanza kazi ya kuunganishia wateja wengine ambao waliobaki. Leo unaponiambia mji kama wa Kata ya Tura unapeleka nyumba 20 nani umpelekee nani usimpelekee, Mji katika Kata ya Miyenze unapeleka nyumba 20 nani umpelekee na nani usimpelekee; wale wote ni wapiga kura. Niiombe Serikali itusaidie hii scope iongezwe kidogo kutoka kwenye kilometa moja basi angalau kwenye kijiji ifike hata kilometa tatu au nne itakuwa imetusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kuna changamoto moja ambayo Serikali maana kwamba Wizara na TANESCO wanacheza ngoma mbili tofauti. Leo Serikali inatuambia mwananchi akilipa shilingi 27,000 anaunganishiwa nishati ya umeme. Lakini ukienda kwenye uhalisia sivyo mwananchi analipa shilingi 27,000 unakuta nishati ya umeme iko zaidi ya kilometa moja huyo akilipa shilingi 27,000 kweli kiuhalisia atapata umeme?

Mheshimiwa Spika, ukienda TANESCO anakwambia sina bajeti, siwezi kupeleka umeme kwa sababu inahitaji nguzo zaidi ya kumi, sasa TANESCO hujampa fedha na amepokea fedha ya mteja, unapotoa kauli kama Waziri kusema shilingi 27,000 wananchi wanataka kweli kulipa shilingi 27,000 wapate umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali hebu kuweni na dawati maalum la kutoa elimu. Ile shilingi 27,000 ukomo wake uko wapi, je, kama kuna ziada muda gani wa kusubiri ili ninyi mjipange muweze kufanya hiyo kazi ya kumuunganishia umeme, kuliko sasa hivi imekuwa vurugu match. Leo hii Kata ya Goweko kuna umeme jazilizi ambao umepelekwa kule mradi ambao nilikuomba Mheshimiwa Waziri. Lakini wamepeleka kwa idadi ya nguzo 35 zimekamilika, lakini wananchi bado na wameshalipa shilingi 27,000 wanasema sasa sisi tunafanyaje, wameenda TANESCO wanaambiwa sisi hatuna bajeti. Nikuombe Goweko pale tuongezee nguzo zingine kwa sababu ulisema hii kauli na wenyewe wanaisimamia hata kama ipo nje ya ule mkataba mimi nikuombe sana nisaidie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nirudi sasa kwenye sekta ya mafuta; kwanza niipongeze Serikali kwa jitihada zake za kuchukua jukumu la kuweka vinasaba, niipongeze sana, mlipoipeleka TBS kule mmefanya uamuzi mzuri na sisi kama Wabunge tulitoa hilo kwa sababu kuiona kampuni inanufaika kushinda Serikali na ndiyo maana tukasema hivi vinasaba tuviweke wenyewe. Nikiri tu ni mdau mzuri wa mafuta katika sekta hii naomba nishauri jambo moja. EWURA wanafanyakazi nzuri sana, lakini wao nao wana changamoto, leo EWURA amekuwa akienda tu sehemu kama kuna makosa, haulizi hata kosa limetokana na nini yeye kazi yake ni kufungia tu kituo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa sijui ndiyo wamesoma professional ya kufunga tu, lakini wao hawajikagui kama wana upungufu, wenyewe wanaona wafanyabiashara ndiyo wana mapungufu. Mimi nitoe ushahidi kidogo juu ya EWURA wanavyofanya leo tunasema vinasaba viwekwe kwenye mafuta, lakini mafuta yaliyowekewa vinasaba na ambavyo havijawekewa vinasaba kwa mteja wa kawaida hajui kitu chochote, hata mwenyewe sijui mafuta yapi yamewekewa vinasaba na yapi hayajawekewa vinasaba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo akija yeye na machine yake ndiyo anaiamini kama Msahafu au Biblia akiweka pale ikikataa anasema hii ina vinasaba kidogo haijafikia kile kiwango. Sasa hicho kidogo nani aliweka? Na ikiwekwa inaoneshaje kama imewekwa kidogo? Nikuombe Mheshimiwa Waziri na hili naomba ulichukulie u-serious hawa jamaa wanasumbua sana wafanyabiashara yaani wamekuwa wao ndiyo miungu watu wakifika pale funga kiri hapa kuwa nimekuta kuna kosa na kama nataka nifanye biashara na kiri haraka haraka nikulipe faini yako tuachane kisalama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini unakuta muda fulani wameonea ukichukua yale yale mafuta ukaenda kupima machine nyingine inaleta kipimo tofauti ya kwao ya kwanza, wamepima na wamekufungia na wamekudhalilisha imesema inamakosa, umeenda kwingine ipo sawa ukirudi huku wanasema aisee kanuni ya fidia hamna wewe endelea kufanya biashara. Badilisheni hizi kanuni la sivyo wajiangalie na wao na siye tutakuja siku moja wakaja wakakutana na magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hapa watu wamesema vituo vya vijijini vipunguziwe masharti ni kweli, leo mnaruhusu watu kulala na petrol mnashindwa kumruhusu mtu haraka haraka aweke mafuta pale nje pump moja mnaweka mavibali mengi, yaani kibali kukamilisha kupata shell ya mafuta yaani uwe na siyo chini ya shilingi milioni 30. Sasa kwa mwananchi wa kijijini ukimwambia milioni 30 anaipata wapi? Kuna teknolojia zimekuja nyingi kuna kontena linatembea yaani ukiweka kontena…

SPIKA: Ahante sana.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, huku ndiyo kulikuwa panoge, nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)