Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kidogo katika Wizara hii muhimu katika ustawi wa Taifa letu. Awali kabisa kwanza ningependa kutoa pongezi kwa Wilaya ya Kigamboni kwa shughuli waliyoifanya ya kuweza kumbaini mwizi wa mafuta kwa kweli nilipoisikiliza ile clip nilijisia vibaya sana nikaona kwamba kumbe wafanyabiashara wetu wanahujumiwa kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Sara Msafiri Pamoja na uongozi wake wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na kwa miaka hii miwili niseme kwamba bado wamechelewa wanatakiwa wajidhatiti kuhakikisha maeneo yale ya Kigamboni yanakuwa salama kwa ajili ya kuhakikisha mafuta hayaibiwi tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ningependa kuipongeza Wizara hii kwa sababu Waziri wa Wizara hii na viongozi wake wamekuwa ni watu wanaotusikiliza vyema na pia wamekuwa wakitoa ushirikiano kwetu mkubwa tunapokuwa na changamoto katika maeneo yetu tunawashukuru sana viongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitapenda kujielekeza moja kwa moja kwenye changamoto za wananchi bajeti kweli ni nzuri inatia matumaini lakini kama ilivyo ada hatuwezi tukaacha kuongelea changamoto za wananchi wetu ambazo wanakuwa wanatupasia ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto ambazo tunakabiliana nazo ni Pamoja na usambazaji wa umeme ambao unaenda kwa kulega lega na tunapokuwa taunafuatilia tunaambiwa kwamba bajeti inayotoka katika Wizara kwenda katika maeneo yetu kwa ajili ya usambazaji wa umeme inakuwa ni ndogo sana kiasi kwamba mwisho wa siku mameneja wetu katika mikoa na wilaya zetu wanapata changamoto ya kuonekana kama hawafanyikazi kumbe bajeti wanayopewa kwa ajili ya kuhakikisha umeme unawafikia wananchi inakuwa ni ndogo.

Mheshimiwa Spika, nilitamani kuiomba Wizara itengeneze mkakati mzuri ambao utahakikisha umeme unasambazwa kwa ukubwa kwa maana ya kwamba wanapokuwa wanaweka bajeti ndogo ile tija ya usambazaji wa umeme inakuwa haionekaniki na wananchi watakuwa wanaendelea kuona kwamba watu wa TANESCO ni watu wanaokula rushwa sana kitu ambacho wakati mwingine unakuta hata wale mameneja hizo rushwa hawali ila tu ni mazingira ya usambazaji umeme yanakuwa yako duni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nilipenda kuongelea suala la umeme wa REA kwa maeneo ya mjini. Siyo miji yote kwamba ina mitaa katika miji mingine mfano mimi kwangu kule Tunduma tuna maeneo mengine ambayo ni vijiji ndani ya mji mfano Chiwezi, Mpande ni maeneo ambayo kwa kweli ni magumu kwa usambazaji wa bajeti hii inayopelekwa kuweza kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano nikitolea eneo la Chiwezi bajeti tu ya kupeleka umeme kule ili iweze kufika ni takriban bilioni mbili wakati huo huo meneja wetu wa wilaya anapewa bajeti ya milioni 260. Kwa hiyo, unakuta mazingira kama hayo maeneo kama ya Chiwezi yanaweza yakawa hayapati umeme kwa wakati na mwisho wa siku nilitamani sana kuiomba Wizara ichukue hii kama special mission ya kuweza kuhakikisha maeneo haya yanapata umeme kwa bajeti ambayo ni nje ya ile wanayokuwa wametoa kwenye wilaya.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kumekuwepo na changamoto ya umeme kukosa nguvu na kitendo cha umeme kukosa nguvu mara nyingi huwa kinatokea pale ambapo transformer inakuwa imezidiwa uwezo wa kufanyakazi na tukiangalia transformer nyingi zinazokuwa zimewekwa vijijini yaani ni zile zenye uwezo mdogo unakuta ndani ya muda mfupi zile transformer zinakuwa zinazidiwa kiasi kwamba umeme unakuwa hauna nguvu. Nilitamani sasa kama Wizara waje na mpango mbadala badala ya kupeleka hizo transformer zenye uwezo mdogo maeneo yote wajaribu maeneo mengine kwa assessment zao wapeleke zile transformer ambazo zitakuwa ni kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umeme unapokuwa unakosa nguvu ina maana kwamba kazi nyingi zinashindwa kufanyika vizuri na hata kama watu wamejiajiri kupitia umeme unakuta wanashindwa kufanya kazi zao ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ningependa kuongelea suala la bei za umeme tunapoongelea Wizara hii ya Nishati kwenye kipengele cha umeme hii ndiyo sehemu watanzania wengi wanaweza kujiajiri. Kaatika kujiajiri huku gharama za umeme zinapokuwa ziko juu ina maana uendeshaji wa hizo projects zao unakuwa uko juu na ndiyo tunarudi palepale kwamba ushindani wa soko wazalishaji wa bidhaa watashindwa kuendana na gharama za soko kwa maana ya kwamba ushindani utakuwa ni mkubwa Zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najaribu ku-imagine mfano watu maeneo kama ya institution kama shule, labda hospitali, hoteli hawa watu wanapata wakati mgumu wa ku-run haya maeneo kulingana na kwamba gharama zinakuwa zinapanda na kile kipengele cha kusema sijui kuna tariff one, tariff two kwa matumizi ambayo ni ya kawaida tulitamani Wizara iweze kuliangazia na kuliondoa kwa sababu haiwezekaniki mtu anayetumia umeme eti kisa anatumia umeme mwingi ndiyo apewe gharama kubwa wakati yule anayetumia umeme kidogo anapewa gharama kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika principle ya soko maeneo yote anayetumia kikubwa ndiye anayeongezewa. Kwa hiyo, nilitamani Wizara katika hili waweze kujitafakari na kuangalia namna gani wanatusaidia watanzania tuwe wateja wao wazuri ili tuweze kufanya mambo ambayo yataleta maendeleo kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kupitia hotuba ya Waziri nimefurahi sana kuona mradi wa kusafirisha umeme kutoka Iringa, Mbeya, Tunduma hadi Sumbawanga kwangu nimeona ni faraja kwa sababu hali ya umeme kwenye eneo letu la Mkoa wa Songwe limekuwa ni jambo ambalo wananchi wanalalamika sana. Umeme haupo, umeme unakatika katika mara kwa mara na inapofika Jumamosi wananchi wameshajiandaa…

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge na hasa kuna wengine wananigeuzia na viti kabisa nitafikia mahali nitaanza kutaja makundi ya wazozaji humu ndani itakuwa ni aibu maana yake nawaona nina kioo hapa ambacho kinanionyesha na kutaka kuangalia.

Sasa nikikutaja ni aibu kwa wapiga kura wako lakini pia kanuni hairuhusu kugeuza kiti ukampa mgongo Spika. Kwa hiyo, angalieni huku huku tumuangalie anayechangia. Mheshimiwa Neema Mwandabila endelea. (Makofi)

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante nadhani utanilindia muda wangu huo mchache.

Mheshimiwa Spika, nimefarijika kuona huu mradi wa usafirishaji wa umeme unaotoka Iringa kuelekea Sumbawanga ambapo kwa upande wa Tunduma kutakuwa na kituo cha kupozea umeme. Kwangu naiona faraja kwa sababu wananchi ni kitu wanachokisubiria kwa hamu umeme umekuwa ni wa shida sana, na kumekuwa na changamoto ya umeme kukatika kila inapofika Jumamosi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama umeme utakuwa unapozewa Tunduma naamini kabisa zile changamoto zingine zinazokuwa zinatokea zinapelekea umeme kukatika katika zitaweza kupungua, na gharama ya mradi huu ni trilioni 1.4 na nikiangalia kuanzia pesa iliyotengwa hii bilioni moja kwa namna fulani inatupunguza matumaini kwamba utaenda kwa kasi hii japo naamini kabisa Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hii Pamoja na Katibu Mkuu wako vizuri kuweza kutusaidia, kwa hiyo, nilitamani bajeti iwe angalau inasoma vizuri ili kuweza kututia matumaini kwamba mradi huu utaenda kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sitajitendea haki kama nitashindwa kuongelea suala la joto ardhi sisi kwetu kule Songwe tumebahatika kuwa na eneo ambalo linakiashiria cha joto ardhi eneo la Nanyala Mbozi. Mheshimiwa Waziri aliweza kutembelea eneo lile akaangalia lakini kwenye hii hotuba sijaona akizungumza neno katika eneo hili nilitamani kwa niaba ya wananchi wa Songwe tungependa kusikia kwamba baada ya yeye kutembea pale amekuja na mkakati gani wa kutusaidia kama wana Songwe ile fursa ya kuweza kupata umeme iweze kuwa revealed kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia sisi Songwe pia tuna utajiri wa makaa ya mawe sijaona katika hotuba wakiongelea kitu hiki hata kidogo na tunajua makaa ya mawe ni nishati sasa nashindwa kuelewa kwamba haya makaa ya mawe yanachukuliwa kwa namna gani. Kwa hiyo nilitamani kuona kwamba Wizara kama Wizara imejipangaje kutumia haya makaa ya mawe yaliyopo kwetu kule Ileje katika namna ambayo itakuwa na tija katika uzalishaji wa umeme na nishati zingine.

SPIKA: Ahsante Neema Gerald Mwandabila.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante niseme tu naunga mkono hoja na niwatakie viongozi utekelezaji mwema. (Makofi)