Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi kuchangia katika Wizara hii ambayo ni kichocheo kikubwa na muhimu sana cha maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaanza na wananchi wangu. Wilaya yangu ya Mkalama ina vijiji 70 na katika vijiji hivyo 20 bado havijapata umeme na katika vijiji hivi ambavyo havijapata umeme Mheshimiwa Waziri iko kata nzima ya Mwanga ambayo haijawahi kuona umeme kata hii. Mheshimiwa Waziri, tarehe 17 Aprili, 2020 ulikuja Mwanga na Serikali ikakosa pale kwamba kesho yake tu tarehe 18 nguzo za umeme zitamwagika kama maji pale, wananchi walishangilia sana. Lakini, mpaka leo Kata hii wananchi wa vijiji hivi vya Kata ya Mwanga ambavyo ni Msisai, Kidarafa, Mwanga, Kidigida, Msiu na Marera bado wanaota tu kwamba nguzo zitamwagika alisema Waziri. Nashukuru kwamba umeendelea kuwa Waziri katika Wizara hii na hivyo naamini sasa hutaiangusha kauli hii ya Serikali ambayo ilionesha kwamba nguzo zingemwagika kama mvua lakini mpaka leo kata hii haijapata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Wziri nikuombe katika Awamu hii ya REA III kata hii iwe kata ya kwanza kupata umeme katika vijiji hivi 20 vilivyobaki. Mbaya zaidi Mheshimiwa Waziri, katika wakandarasi uliowaagiza kwenye Mkoa wa Singida ulimuagiza Ms Central Electrical International Limited kwenda kufunga umeme Singida. Lakini tulipomfuata akasema hana scope ya Mkalama. Scope yake ni Ikungi na Singida Rural. Kwa hiyo, mpaka hivi ninavyoongea REA Awamu ya III sisi hatuna mkandarasi, tuna kiini macho. Labda ningeomba katika majibu utakayokuja nayo utuambie mkandarasi wetu nani ili tumfuate tuweze kuona umeme unapatikana Mkalama.

Mheshimiwa Spika, nimuombe Waziri kweli bei tumeshusha shilingi 27,000 kuingiza umeme na ametangaza leo hakuna kuuziwa nguzo lakini umeme unapofika huko vijijini wananchi wanakuwa wengi sna wanasubiri kuwekewa umeme. Waliolipia 27,000 na ambao hawajalipia 27,000. Hawa wanaoweka umeme wanasema sababu za vifaa vingine ambavyo vinasababisha uweze kuwekewa umeme. Nguzo zenyewe za LV kwa mfano kwenye Jimbo langu nguzo zinatakiwa 1400, hakuna. Kuna waya za ABC milimeta 50, kilometa 74 zinatakiwa, hakuna! Hiyo ni reference najua na majimbo mengine itakuwa hakuna. Suspension clamp karibu 990 hamna! Tension clamp 60 hamna, staycompletewith 140 hamna.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Waziri tunapopeleka tuwapelee na hivi vifaa ili ile foleni ya kuwekewa umeme sasa kwa 27,000 iweze kufanikiwa. Kwa sababu, tunasema 27,000 lakini wananchi wako wengi wameshafanya wiring wengine wanasubiri lakini ukiwagusa TANESCO hivi vifaa hawana na ukifuatilia kweli, hawana! Nakushukuru Mheshimiwa Waziri umekuwa mwepesi sana wa kuchukua hatua kw watendaji wazembe, hilo nikupongeze. Lakini nikuombe wapelekee na hivi vifaa ili unapowachukulia hatua wasiwe na sababu ya kulalamika hukuwapelekea vifaa halafu umewachukulia hatua kwamba ni wazembe ili hili zoezi la 27 na umeme kufika kule vijijini wananchi walipate kwa kuhakikisha basi vifaa hivi vinakwenda. (Makofi)

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa kuna taarifa endelea.

T A A R I F A

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe Taarifa mzungumzaji anayezungumza sasa kwamba wako baadhi ya watu wenye uwezo wao ambao kutokana sasa na vifaa vile kutokuwepo wanakuwa tayari kwa hiari yao kulipa nguzo pamoja na zile gharama kwa hiari yao. Kwa hiyo, wale watu walioko kule nao wanashindwa kufanya hivyo hata kama wangeweza kufanya hivyo kutokana na kwamba bei imewekwa elekezi 27,000 wale wenye uwezo walio wachache.

SPIKA: Mheshimiwa Mtinga unapokea Taarifa hiyo?

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, naipokea lakini sifurahishwi sana na hii. Wenye uwezo wanaweza wakasababisha TANESCO wakalalia huko kwenye uwezo na wananchi wetu wenye vipato vidogo ikashindikana. Kwa hivyo, ningeomba tu vifaa viende halafu wananchi wote wapate umeme kwa hiyo 27,000 ambayo Serikali yetu imeiweka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa niusemee na Mkoa wangu, Mheshimiwa Waziri wakati unafungua matumizi ya gesi majumbani kule Lindi ulisema kwenye hotuba yako kwamba mikoa itakayofuata baada ya Dar es Salaam ni Mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida uliitaja. Tulishangilia sana jambo hili kwamba sasa na sisi tutapata umeme wa gesi kupitia bomba ili kwenye nyumba zetu tuweze kusambaziwa gesi. Lakini katika hotuba yako nilikuwa nasikiliza kwa makini sana ili niweze kuona ule msukumo wa hotuba yako ukiendana na bajeti, sikulisikia hili.

Mheshimiwa Spika, nikuombe, jambo hili ni la muhimu sana, kupata gesi ya majumbani ambayo tumeweka bomba kwa gharama kubwa sana limefika Dar es Salaam na tunatumia kidogo mno kwa kiasi cha gesi inayofika pale.

Sasa huu mpango uliusema kwenye hotuba ambayo nilikuwa najua ni hotuba ya ukombozi hujalisema kwenye bajeti. Labda pengine utakapokuja kwenye kujumuisha useme huu mpango wa kutoa bomba lile la gesi kutoka Dar es Salaam kuja Morogoro kuja Dodoma na hatimaye kufika Singida kwenye mkoa wangu kama upo au au haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niwaombe tu Serikali hivi vitu vingine kama bajeti inakuwa ngumu na miradi hii ni mikubwa, tusisahau private sector. Najua shirika la TPDC limepewa mamlaka ya kisheria kama hodhi kufanya hili jambo peke yake. Mzigo huu unakuwa mzito, private sector ipo na watu wana fedha. Mimi ningeshauri Wizara muwe mnaangalia na vitu vingine kama hivi vizuri mnaruhusu private sector isaidie basi huduma hizi zinaweza kufika haraka sana katika nyumba zetu.

Mheshimiwa Spika, hii gesi itasaidia sana kulinda mazingira, ni faida mtambuka, kwanza maisha ya wananchi yatashuka kwa maana gharama zitashuka kwa sababu wataacha kununua mkaa kwa bei kubwa lakini vile vile mazingira ya nchi katika mikoa yetu hii yataboreka kwa sababu watumiaji wakubwa sana wa mkaa wako mjini. Sasa kama mabomba ya gesi yakifika ina maana soko la mkaa litakufa na mazingira yetu yatapona na fedha nyingi zinazokwenda Wizara ya Mazingira kwa ajili ya kuokoa miti zitakuwa zimepona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, huu ni mradi ambao utakuwa ni wa kimkakati kabisa. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri, jambo hili ulilisema wewe kama Serikali. Usiliweke kando. Ni jambo la muhimu sana, najua gesi ikifika Singida mwisho itakwenda mpaka Shinyanga na mwisho itamaliza nchi yetu yote. Mradi wa maji unatoka Ziwa Viktoria, upishane na gesi kwenda kule. Nchi yetu ni kubwa, ni soko tosha la miradi yetu ya kimkakati kwa hiyo tuitumie vizuri kwa kuhakikisha gesi hii inafika Singida kama ambavyo ulikuwa umesema kwenye hotuba yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sipendi sana kugongewa kelele. Naomba nishukuru na kuunga mkono hoja. Mheshimiwa Waziri uje na majibu kuhusu jambo hili la gesi. Ahsante sana na suala la umeme kule Mwanga na vijiji vilivyobaki. Ahsante sana. (Makofi)