Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Abdallah Jafari Chaurembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia katika bajeti ya Wizara hii ya Nishati na Madini.

Kwanza kabisa niipongeze sana Serikali yetu hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri wanazoendelea kuzifanya katika miradi mikubwa, miradi ya kitaifa, ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wameizungumza. Kwa kweli na mimi niendelee kuuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali yetu.

Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake na viongozi wote wa wizara kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya katika kuhakikisha suala hili la Nishati na Madini linakwenda vizuri katika Nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, tarehe 25 Februari, 2018 Serikali yetu ilitujengea sub-station kubwa pale Mbagala ambayo imekuwa na uwezo wa kuzalisha Megawatts 42 za umeme ambazo zimekwenda sana kunufaisha katika Jimbo la Mbagala. Katika kipindi hiki ambacho tumeanza kutumia sub-station hiyo kwa kweli wananchi wa Jimbo langu la Mbagala walikuwa hawana tatizo lolote la umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini baada ya kufika mwaka 2020 mahitaji ya Jimbo letu la Mbagala ni Megawatts 32; 2020 ilipofika kwa kuwa Ndugu zetu wa Mkuranga Mkoani Pwani wao hawana sub-station ya umeme, umeme ule ambao unatoka kwenye sub-station ya Mbagala umepelekwa Mkuranga pamoja Lindi. Kitu kilichosababisha Jimbo la Mbagala libaki na Megawatts 8 tu, kitu ambacho kimesababisha sasa tatizo kubwa la umeme katika Jimbo la Mbagala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kinachofanyika hivi sasa tumekuwa tukipewa umeme kutoka Ilala, Kinyerezi na umeme mwingine ukitoka pale Kurasini. Kwa kuwa umeme huu umekuwa ukitoka sehemu tofauti tofauti; umekuwa na shida kubwa sana ya ukatikaji wa mara kwa mara. Kwa wastani siku moja nilimuonesha Naibu Waziri, kwa siku umeme umekatika zaidi ya mara 45. Sasa tunajiuliza sisi wananchi wa Mbagala tuna tatizo gani? Kama sub-station Serikali yetu imetujengea yenye uwezo wa kuzalisha megawatts 42 uwezo wetu wa kutumia ni Megawatts 32; kwa nini umeme ambao unatokana na sub-station ya Mbagala unapelekwa Mkuranga? Huku ukituacha watu Mbagala tukiwa na masikitiko na malalamiko makubwa ya ukatikaji wa umeme mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliuliza swali la msingi hapa katika Bunge lako hili Tukufu, Mheshimiwa Waziri alinijibu kwamba sub-station ile inakwenda kufungwa transformer ya MVA 50; lakini nimepitia bajeti ya wizara sijaona mahali ambapo imetengwa fedha kwa ajili ya mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe Jimbo la Mbagala ndio jimbo lenye watu wengi katika Nchi hii, na ndio jimbo lilitoa kura nyingi kwa Chama Cha Mapinduzi, sasa niwaombe sana, niwaombe sana, tafuteni utaratibu mwingine wa kuwapa umeme watu wa Mkuranga. Watu wa Jimbo la Mbagala tuendelee kunufaika na sub-station ambayo imejengwa katika Jimbo letu la Mbagala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni mzalendo wa Nchi kwa ujumla, naamini kwamba Mkuranga nao wanahitaji sana suala zima la umeme. Hebu tuangalie namna ya kujenga sub-station Mkuranga ili waweze kujitegemea na sisi Mbagala tuendelee ku-enjoy na matunda ya sub-station ile ambayo imejengwa Mbagala.

Mheshimiwa Spika, wateja wa umeme walioko katika Jimbo la Mbagala ni wateja 75,563. Naamini idadi hii ni kubwa kulinganisha na mikoa mingine ya ki-Tanesco katika Nchi yetu. Idadi ya maunganisho mapya kwa mwezi tuna wastani wa maunganisho 400 kwa kila mwezi. Sasa sielewi kwa nini Tanesco na wizara hii tunashindwa kufanya Mbagala ikawa mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa Mbagala kuwa mkoa, tunakwenda kuondokana na matatizo mengi ukiangalia mita, nguzo na vifaa vingine lazima twende tukapate main store ambayo iko mkoani. Na kulingana na ukubwa wa Mbagala na maunganisho haya mapya ya kila mwezi yanapelekea kunakuwa na ucheleweshaji mkubwa wa kupata huduma hiyo. Wakati nauliza swali Mheshimiwa Waziri alinijibu tuandike maombi; sidhani kama ipo haja ya kuandika maombi. Ninyi wenyewe Tanesco mnaona, ninyi wenyewe wizara mnaona umuhimu wa eneo, hebu niwaombe sana muangalie Wilaya hii ya Mbagala iweze kupata hadhi ya kuwa mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ipo miradi mbalimbali inaendelea katika jimbo langu la Mbagala. Upo ule mradi wa Malela kule Tuangoma, Yamoto Band kule Mbande, Machimbo pale Azam, Mponda, Yatima n.k. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miradi hii imekuwa na changamoto kubwa baadhi ya maeneo zinaletwa nguzo kulingana na idadi ya mradi lakini ukifika pale baadhi ya wananchi kwa kutaka umeme walikuwa wameshajiungia umeme kwa kulipa TANESCO na wakaletewa nguzo. Zile nguzo zinazobaki kwenye mradi zinarudi kwanini zirudi wakati bado upo uhitaji wa umeme katika maeneo yale? Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri kama wananchi wamejitahidi kuvuta umeme na mradi umekuja katika eneo lile; basi nguzo zinazobaki ziendelee kufanya extension katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Nimekuwa nikipata changamoto sana katika maeneo ya Kata ya Chamazi, Charambe, Mianzini, Kirungule, Kiburugwa, Mbagala, Mbagala Kuu, Tuangoma, Kijichi, pamoja na kata ya Kibondemaji. Niwaombe sana wizara, niwaombe sana, nguzo zile zinazobaki ziendelee kuhudumia maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini lipo tatizo la zile zilizokuwa mita za zamani, wananchi wetu wengi wa Mbagala mnafaham vipato vyao ni vya chini, wengine wameuza majumba yao Kariakoo wamekuja kuhamia Mbagala, nyumba walioyoikuta wameikuta ina mita ya zamani ina deni mpaka milioni 8; leo hii unamtaka mwananchi akinunua umeme wa shilingi 1,000 akatwe nusu ya fedha ile illipe deni la nyuma. Kwa kweli tutakuwa hatuwatendei haki wakazi wetu wa Mbagala. Niiombe sana wizara, iangalie namna bora ya kuweza kumaliza haya madeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie, Mbagala bado wanakaa watu wa vipato vya chini Mheshimiwa Waziri; hebu tuangalie namna ambayo watu wa Mbagala si kupata huduma ya umeme wa REA bali wafanye maunganisho kama wanavyounganishwa katika watu wanaopata huduma ya REA. Kwa sababu miundombinu ipo, isipokuwa uwezo wao ni mdogo wa kulipia. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, nafahamu sana utendaji wako wa kazi na kwa sababu lengo letu ni kuongeza mapato katika Shirika letu hili la Umeme la TANESCO basi tutoe namna wananchi wale wanapoweza kuunganishwa umeme kwa kutumia gharama za REA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Nikushukuru sana na niunge mkono hoja. (Makofi)