Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana na mimi tena kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Lakini wakati naanza kuchangia, nikumbushe kidogo historia yangu labda na historia ya Wilaya yetu ya Masasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafanya hivyo kwa sababu, tuna tatizo kidogo kwa hiyo, nataka niishauri Serikali, niipongeze kwa kazi nzuri walizozifanya. Lakini pia sasa, tukubaliane kimsingi tunakwenda kufanya nini, ili kuhakikisha Wilaya ya Masasi inapata umeme wa uhakika na vijiji vyake vyote pamoja na Majimbo yote na hasa zaidi Mkoa wa Mtwara wote kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utakumbuka Bunge lililopita, nikiwa natokea huko huko Wilaya ya Masasi na ninapoitaja Wilaya ya Masasi Waheshimiwa Wabunge naomba mkumbuke kwamba, ni kati ya wilaya kongwe sana zilizoko nchini Tanzania ilianzishwa kati ya mwaka 1920 na mwaka 1928. Na Wabunge wengi wamepita pale mbalimbali ndiko alikotokea hata Mheshimiwa Rais wa nchi hii wa Awamu zilizopita, Mheshimiwa Rais Mkapa na mimi nilikuwa kwa mara ya kwanza Mbunge nikitokea kwenye Chama cha upinzani, lakini wananchi wa Masasi walinichagua wa Wilaya ya Masasi na Jimbo la Ndanda hasa ambalo lilikuwa jipya kabisa ili niweze kuwawakilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini wao walitambua kabisa kwamba, wamenichagua ili nishirikiane nao kuja kuisemea Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ndani ya Bunge lako Tukufu na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi toka wakati huo na kipindi chote, inatambua kwamba na imeahidi kila kijiji kitapata umeme na kila sehemu kwenye zile huduma kubwa za kijamii kama kanisa, misikiti na maeneo mengine yatapata umeme. Sasa, wakati naingia kuliwakilisha Jimbo la Ndanda mwaka 2015 tulikuwa na vijiji 42 ambavyo havina umeme kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mpaka sasa hivi Wizara hii imefanya kazi nzuri na vijiji vilivyobakia bila kuwa na umeme ni 19 tu. Lakini kwa ahadi hapa ya Mheshimiwa Waziri anatuambia kwa sababu, mambo hayo yapo ndani ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kazi hiyo itakwenda kufanyika ndani ya muda mfupi ujao. Lakini, nataka niwakumbushe na kuwapongeza sana Wizara kwa kazi yao, nipongeze pia uongozi wa Wilaya ya Masasi kwa maana ya Management nzima ya TANESCO Wilaya ya Masasi kwa kazi nzuri wanayoifanya, Mkoa Eng. Fadhili pamoja na Kanda Mzee wetu pale Mzee Makota kwa kazi nzuri sana wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze pia TANESCO kwamba, tulikuwa tunatamani sana sisi tuliotokea Wilaya ya Masasi kwa sababu miradi ya REA kipindi kilichopita, ilikuwa imekwama sana kutokana na aina ya mkandarasi ambaye walimleta wakati huo. Tumepata mkandarasi bora kabisa ninaamini katika wakandarasi wengi walioko pale ambaye ni Namis Cooperate, amefanya kazi nzuri sana ya umeme vijijini kwenye maeneo mengi na ninaamini sasa amekuja kuwa suluhu ya tatizo la umeme, kwenye Wilaya yetu ya Masasi na Mkoa wa Mtwara, Majimbo ya Ndanda, Masasi pamoja na Lulindi na ninaamini kazi hii ataifanya kwa uhakika mkubwa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikutana na Waziri siku chache na nikamuambia mapendekezo yangu, kuna Kata mbili ambazo hazina umeme kabisa, Kata ya Msikisi na vijiji vyake vyote, vijiji vya Namalembo, Liwale pamoja na Msikisi yenyewe. Kata ya Mpanyani na vijiji vyake vyote, ikiwemo Namalembo, Mpanyani, Muungano pamoja na vijiji vingine vilivyobakia havina umeme kabisa. Kwa hiyo, ninaomba kabisa mkandarasi huyu atakapokuwa anakwenda kufanya shughuli yake ya umeme kule, ambaye tunaambiwa sasa hivi yuko site. Kabla hawajaenda eneo lingine lolote kwenda kufanya kazi ya umeme, waanzie na maeneo haya kwa sababu, watu hawa hawana umeme kabisa bora hata Kata zingine na vijiji vingine wanao umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna tatizo kubwa la usambazaji kwa maana ya kwamba, miradi iliyokuwa imekwenda kwenye maeneo hayo ikianzia maeneo ya Nanganga, maeneo ya Mumbulu ukija maeneo ya Mkwera, ukienda maeneo ya Ndanda Kijiji cha Ndolo, ukienda maeneo ya Mwena Kijiji cha Ndunda, ukija Chikundi Kijiji cha Mkalapa, lakini pamoja na maeneo ya kanisani, ukija Chigugu maeneo ya Mbemba pamoja na Mbaju umeme haujajitosheleza. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri huduma ile ya ujazilizi sasa wakati TANESCO wanafanya shughuli zao zingine na umeme unasambazwa kule basi wahakikishe kwa namna ya pekee wanakwenda kufanya ujazilizi kwenye maeneo haya, ili wananchi wa Kata hizi wote kwa pamoja wapate umeme sawa sawa, kwa mujibu wa Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi kwa sababu, ndio iliyosimama na ndiyo inayotekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina mashaka kidogo na namna ambavyo Wizara hii imejipanga kuhusu kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati na hapa nataka niongelee suala la gesi. Mpaka sasa hivi gesi iliyoko Mtwara inatumika kwa wastani wa asilimia 10 tu. Lakini nataka niwakumbushe Wizara kwamba, Serikali ilikopa fedha nyingi sana kuona lile bomba linatolewa kutokea Mtwara na linapelekwa Dar es Salaam kwa ajili ya matumizi hii ni kwa ajili ya kukuza uchumi wa Mtwara na watu wake.

Mheshimiwa Spika, lakini mkumbuke pia kwamba, sehemu kubwa ya uchumi sisi tunategemea kwenye gesi kwa sasa, tunaomba sasa basi miradi hii itekelezwe mapema sana. Kwa sababu, sehemu pekee iliyobakia tunafanya tu kazi za korosho, ndio maana inapofika wakati wa korosho maana wote tunalazimika kusema kwa sababu, ni sehemu ambayo tunategemea kupata fedha kidogo. Lakini miradi ya gesi ikianza hata uzalishaji wa korosho nao utaongezeka na sisi tutakuwa tuna amani kwa sababu, na bandari yetu ya Mtwara pamoja na Mtwara Corridor kwa ujumla, kwa maana ya hii Southern Reli pamoja na bandari ya Mtwara, ambayo Serikali imeweka fedha nyingi na yenyewe itaweza kufanya kazi zake vizuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimuombe kabisa Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-windup, atueleze mkakati madhubuti wa kurudi tena kwenye matumizi ya gesi kujenga kile kiwanda kwa ajili ya kuchenjua hii gesi asilia maeneo ya Lindi, kwa maana ya mradi wa NLG na matumizi makubwa ya gesi. Kwa sababu, inashangaza kuona wilaya kama wenzetu Wilaya ya Madaba, ambako anatokea rafiki yangu hapa, Mheshimiwa Muhagama kwamba ni wilaya iliyoanzia mwaka 2015, unailinganisha na Wilaya ya Masasi yenye miaka zaidi ya 50, kwa sababu imeanza miaka 28 kabla ya uhuru wa nchi yetu kwamba, Madaba wao wamejitosheleza kwa umeme na vijiji vyake vyote vimepata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sisi bado tunaongelea umeme uliobora kwa maana ya kutokukatika katika lakini pia, umeme unaotosha kwenye vijiji vyote. Sasa mtutendee haki wilaya hii ni ya siku nyingi na kama vigezo vya mgawanyo wa mikoa, ilikuwa ni kutokana na umri wa wilaya, Wilaya yetu ya Masasi ingekuwa imeshakuwa mkoa siku nyingi kabisa kabla hata ya wilaya nyingi za Tanzania hii hazijazaliwa. Hata mikoa mingine imeikuta Wilaya ya Masasi ikiendelea ku-exist. Kwa hiyo, niombe sana kazi hii muifanye kwa uhakika kwa sababu, sisi tunatoka kwenye wilaya kongwe kabisa, lakini miundombinu yetu sio mizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nashauri Serikali kwamba, iangalie uwezekano wa kuwa na line maalum kabisa inayokwenda Masasi kwa sababu, itapita Ndanda kutokana na ukuaji wa eneo hili kwasababu, sasa hivi ni kama business hub. Ni Mji mkubwa kibiashara unaotegemewa sana na Mkoa wa Mtwara, ukiacha Mkoa wa Mtwara wenyewe mjini kwa sababu, sehemu kubwa ya uchumi wao walikuwa wanategemea uchumi wa gesi. Lakini Wilaya ya Masasi sehemu kubwa ya uchumi wao sasa hivi ni masuala ya mazao ya korosho.

Mheshimiwa Spika, lakini pale ndipo kuliko na junction ya barabara inayokwenda Songea, inayokwenda Nachingwea, inayokwenda Newala na inayorudi Mtwara Mjini. Kwa hiyo, ni eneo kubwa la kibiashara lakini uchumi wake unazorota kutokana na matatizo ya kukatikakatika umeme mara kwa mara. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri hakikisha sasa ile line ambayo iko kilometa 120 kutokea Masasi kwenda Mahumbika, mnatupa line pekee ambayo haitakuwa interrupted hapa njiani. Itoke Mahumbika moja kwa moja iende Masasi moja kwa moja kiasi kwamba, likitokea tatizo lolote la umeme njiani ni rahisi kuirekebisha na bajeti yake nadhani imeletwa kwenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wataalam wa pale wanatuambia, nilikuwa naongea na Engineer Fadhili hapa karibuni kwamba, mkiamua kutumia nguzo za cement itatumika kama bilioni 10, lakini mkiamua kutumia nguzo za miti ni kama bilioni 6 ambayo sio njia ya kudumu sana. sasa hicho ndio kiasi pekee tunachokiomba, hatutamani miradi mikubwa kama ile iliyofanyika kule Namtumbo hapo karibuni. Kama miradi iliyofanyika Madaba, kama ambavyo walisema pale mwanzoni, tunataka mradi ambao utatuhakikishia umeme wa uhakika Masasi ili tuweze kupata umeme ambao utakuwa haukatikikatiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaposema Masasi ni Wilaya yenye Majimbo matatu matatizo yetu sisi yanafanana, tunatambua hapa Mheshimiwa Waziri Mheshimiwa Geofrey kila mara huwa mnakutana. Kwa hiyo, ona namna na wewe ya kumshauri Waziri mnakuwa wote kwenye cabinet tuweze kupata Masasi umeme wa uhakika. Tuweze kupata Lulindi umeme wa uhakika, tuweze kupata Ndanda umeme wa uhakika kwa sababu Mji huu unakua na ili wawekezaji waweze kuja eneo letu, ni pamoja na kupata uhakika wa umeme pamoja na miundombinu mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo niendelee kumkumbusha Waziri kwamba, ili kufanikisha vizuri kwenye hii Mtwara Corridor na matumizi ya bandari ya Mtwara basi ihakikishe sasa miradi ile ya gesi inafufuliwa. Kulikuwa kuna ahadi ya Serikali kutengeneza kituo cha uzalishaji wa umeme wa gesi Mtwara, nakumbuka ilikuwa kama KVA 380 hivi au kitu kama hicho, lakini hatuoni chochote kinachoendelea. Sasa ni muda mrefu na tuone kwamba, tutumie advantage iliyopo sasa kufufua miradi yetu ya gesi kwa sababu, si vizuri sana kusema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kutokana na mgogoro ulioko Mozambique bado watu wanatamani kuwekeza Tanzania kwa sababu, ya amani iliyopo, mazingira yetu ni rafiki kabisa kwenye masuala ya uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa nikuombe, kama ambavyo nimesisitiza toka mwanzo mkandarasi ameshafika Masasi ambaye ni Kampuni nzuri sana ya Namis Cooperate, akaanze kazi kwenye Jimbo la Ndanda, kwenye Kata ya Msikisi na Kata ya Mpanyali tu. Akimaliza hapo huko kulikobakia kwingine sisi wenyewe tutakaa tutaongea na kujua nini tunataka tukifanye, lakini naomba kazi hiyo ikafanyike hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nisisitize tu kuhusu usambazaji umeme vijijini, kwenye vijiji nilivyovitaja kwasababu, maeneo haya yanapitiwa na umeme mkubwa unaokwenda Masasi.

Mheshimiwa Spika, nishukuru sana kwa nafasi hii na ninaunga mkono hoja kwa asilimia 100. Naomba haya niliyoshauri Serikali basi ikayafanyie kazi kwa mujibu wa Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi. Ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)