Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana wewe mwenyewe binafsi kwanza asubuhi ya leo kwa kunipa nafasi ya kwanza kabisa kuchangia majadiliano haya kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara, lakini pia nikupongeze kwa kurudi tena hapo mezani na kutuongozea Bunge letu. Pongezi hizi nizipeleke pia kwa Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, watendaji wote na watumishi wa Wizara ya Viwanda na Biashara kwanza kabisa kwa hotuba nzuri kabisa, fupi, inayoeleweka, yenye malengo makubwa ya kimkakati, lakini kwa namna ilivyooanisha kati ya Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano wa Maendeleo na ule wa Mwaka Mmoja amechanganya pia humo ndani na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa maana ya kutaka kuwatekelezea watu na ndio maana tulisema Ilani hii ni bora ukilinganisha na ilani nyingi zilizoko Barani Afrika kwa sababu ina malengo makuu na yanayotekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie hasa kwenye maeneo matano. Eneo la kwanza kabisa ni utaratibu huu unaotumika sasa na Serikali kwa ajili ya kufanya kuhesabu mali zinazozalishwa kwenye viwanda vya vinywaji, almaarufu kama ETS, ufinyu wa bajeti ya Wizara hii, lakini pia pamoja na masuala ya economic drivers ili tuweze kuisaidia Wizara tuweze pia kuisaidia na nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mkakati ambao nchi yetu imejiwekea tunaweza tukaita ni Wizara mama, na mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara tunafahamu mengi na huwa tunayajadili kule ndani, lakini mwishoni lazima tuyalete hapa ili tuweze kuishauri zaidi Serikali na yaingie kwenye taratibu zetu za Kibunge kwa maana ya Hansard ili kuweza kulisaidia Taifa letu. Malengo ya kuanzisha viwanda ni mazuri sana, lakini namna ya kufikia utekelezaji wa mambo haya ndio sehemu ambayo kidogo inaleta kutokufanya vizuri kwenye mambo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nchi yetu imekubali na imechagua viwanda kuwa kama ni sehemu ya economic drivers. Ni kati ya vile vitu vikubwa ambavyo tunategemea nchi yetu ikasimame ili kupandisha zaidi uchumi wetu, lakini pia kuwasaidia wananchi. Tunafahamu kuna mikakati mikubwa ya Serikali kwenye masuala ua Liganga na Mchuchuma, lakini haya ndio mambo yatakayokwenda kupandisha uchumi wa Kusini, matumizi mazuri ya Bandari ya Mtwara pamoja na kubana matumizi kwenye National Reserve kwa maana ya pesa tutakayotumia nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tulipoanza kutekeleza mradi wa Standard Gauge Railway kutoka Dar es Salaam kwenda mpaka Kigoma na Tabora mwanzoni kabisa tungefikiria tofauti kwa kuanza kuchimba kile chuma kilichopo Liganga na Mchuchuma ili chuma kile kiweze kutumika kutengeneza reli yetu na kiasi cha pesa kinachobakia kiweze kutumika kufanya mambo mengine kama economic driver, lakini kuchagua ni kuanza. Sasa na sisi tulichagua kuanza kutengeneza SGR, sasa hebu tuone kwa sababu pia kuna mkakati wa kutengeneza reli ya Kusini itakayoanzia Mbamba Bay, itapita Songea, itapita Masasi, itapita maeneo ya Ndanda kuelekea Bandari ya Mtwara ili kuweza kukuza uchumi wa watu wa Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi tuone namna sasa ya kuanza kutekeleza mradi huu wa Liganga na Mchuchuma ambao umeanza kutajwa siku nyingi sisi tukiwa wadogo kabisa huko na huu ni uchumi mkubwa kabisa utakaoweza kuendeleza zaidi maeneo ya Kusini ambayo kwa namna fulani yalikuwa yanaonekana kama yametolewa kwenye mkakati wa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado hapo hapo kwenye suala la economic drivers. Ukiangalia kwenye sekta zinazokua vizuri kuna sekta ya ujenzi inakua kwa asilimia 14 na wote tunakubaliana. Kwa mfano tunapokuwa na barabara bora kwa vyovyote vile tutakuwa na biashara nzuri, tutakuwa na barabara nzuri pia zinazoweza kusafirisha mazao kutoka eneo moja kwenda eneo lingine ikasaidia pia kuwakuza wakulima wetu. Suala la umeme pia limekua kwa asilimia nane, lakini pia kuna suala la usafirishaji na lenyewe karibu asilimia 11.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukienda kwenye mchango kwenye GDP kilimo kinachangia almost asilimia 36 kwenye GDP. Viwanda vinachangia asilimia 24 kwenye GDP, lakini ukija kuangalia kwa ujumla bajeti ya kilimo pamoja na bajeti ya kiwanda ni ndogo sana. Mfano kama ambao nilisema pale toka mwanzo kwamba Mchuchuma na Liganga awamu iliyopita kwa maana ya bajeti iliyopita wamepelekewa shilingi milioni 120 tu halafu leo tunasema tunataka tuone Mchuchuma na Liganga vinakwenda kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya majadiliano yanayofanywa na Serikali na hivi vitu vimetajwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, hebu basi fanyeni hima muone namna sasa ya kukuza uchumi wetu kama ambavyo iko China kwa ajili ya viwanda vya chuma, kwa ajili ya kuboresha ile Bandari ya Mtwara ambako uwekezaji mkubwa kabisa pale umefanyika, lakini hatuoni sasa tija ya kutumia ile bandari kwa sababu kimsingi hatuna mizigo mikubwa ya kuweza kupeleka pale. Tunategemea uzalishaji, mzigo pekee mkubwa unaopelekwa Bandari ya Mtwara ni korosho peke yake, kwa nini sasa tusione na kile chuma tunatakiwa tukilete bandarini kwa ajili ya kukisafirisha kwenda nje, lakini pia tutengeneze na viwanda kwenye maeneo hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo pia Wizara ya Viwanda na Biashara wanatakiwa walione, kubadilisha sheria kidogo hasa zaidi kwenye matumizi ya mazao ya shambani na kila mara nimekuwa najaribu kuwaeleza kwenye hili jambo tufungamanishe Wizara ya Viwanda, Wizara ya Biashara pamoja na TIC au Wizara ya Uwekezaji. Hivi ni karibu sawa vitu vinavyoingiliana, vitu vinavyofanya kazi kwa kushabihiana, wawe na mahusiano mazuri ili tuweze kupata definition ya kila kimoja. Tujue majukumu halisi ya Wizara ya Viwanda na Biashara, wafungamanishe na majukumu halisi ya Wizara ya hawa TIC, lakini pia tuangalie kwenye Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nitoe mfano hapa na kila mara nimekuwa nasema hapa ndani ya Bunge kuhusiana na mazao yanayobakia shambani hasa zaidi baada ya mavuno ya korosho. Huwa wanatupa kitu fulani kinaitwa kochoko, wenzetu wa Scotland mwaka jana wametengeneza ile pombe yao inaitwa Scotish Whisky wameingiza almost 4.5 billion Euro kwa ajili ya kutengeneza hii pombe. Na sisi tunavyo vifaa vya kutengenezea hivi kwa mfano kochoko. Nia sasa wakulima wale wanunue yale mabibo yanayobakia waweze ku-extract tuweze kupata pesa za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilisema nitaliongelea hap ani suala la ETS. Hakuna mgogoro kwamba baada ya Serikali kuamua kutumia mfumo huu wa ETS (Electonic Tax Stamps) kwa ajili ya kuhesabu bidhaa kwenye viwanda ni kweli imeongeza mapato na imepunguza kabisa wizi. Sasa suala lililopo ni kwamba, wafanyabiashara wanalalamikia kwamba, kazi ya ETS ni kuhesabu tu, hii Kampuni ya SIPA, inahesabu chupa moja moja wanaweka pale label na kwenda kuiambia Serikali kwamba kiwanda kwa mfano cha Cocacola kimezalisha chupa 500 tunaomba mkazitoze kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa utakuta kwa mfano juice ya mls 200 kodi inayoipata Serikali ni shilingi 1.08, lakini juice hiyo hiyo ya mls 200 fedha anayoipata SIPA kwa kuhesabu kile kichupa kimoja ni shilingi 23. Sasa mtaona hizi gharama zinakwenda kumuongezea mlaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba sana na Katibu Mkuu wa Wizara Mheshimiwa Dotto James ndio alikuwa ni mmoja wa waasisi wa huu utaratibu na yupo huko kwenu, hebu muangalie kwa nini tusitafute kampuni nyingine itakayoweka hizo stamps, itakayokuwa inahesabu kwa gharama nafuu zaidi ili mapato yake nayo yalingane. Haileti tija akilini kuona eti Serikali inapata shilingi 1.08 alafu yule aliyefanya kazi ya kuhesabu chupa na kuitaarifu Serikali kwamba nimehesabu hizi chupa inapata shilingi 25 katika juice ya mls 200 sawa sawa na ilivyo kwenye soda, kwenye Cocacola au na Pepsi au na nyingine gharama ni kubwa sana ya kuhesabu kuliko ushuru unaokusanywa na Serikali kwa hili nalo tukaliangalie vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya maendeleo mwaka jana imepata asilimia 23 tu Wizara hii ni kubwa, lakini sio sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuone pia kuhusu masuala ya viwanda vilivyobinafsishwa Mheshimiwa Waziri umeyataja hapa, ninafikiri umekwenda kuyafanyia kazi tuone kiwanda cha Buko cha Korosho pale Masasi kila siku tukiwauliza mnasema kwamba kuna kesi inayoendelea mahakamani, lakini kuna jambo kubwa ambalo tunakwenda sasa hivi kukutana nalo, kuna biashara za korosho zitaanza hivi karibuni na msimu wa korosho unakenda kufunguliwa na suala kubwa sana Waziri la unyaufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakapokuwa unamaliza kutoa hotuba yako na hili utueleze tunaomba sasa kufahamu kinagaubaga na Serikali iseme kwa neno moja je, kuna unyaufu ama la kwenye zao la korosho ili sasa wale wanaokuja kufanya biashara ya korosho, wanaokuja kuhudumia maghala waweze kujua wazi toka wanaanza hii biashara kama ni kweli kuna unyaufu au hakuna kwa sababu imekuwa ikileta mkanganyika mkubwa sana.

Mheshimiwa Waziri niombe pia kukukumbusha suala la blueprint. Imetengenezwa blueprint na Serikali hii na kila siku tunasema kwamba tunaweza tukatumia blueprint ili kuondoa vikwazo vinavyowakuta wafanya biashara kwa hilo nalo ukalifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi uliyonipatia ahsante kwa muda wako. (Makofi)