Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Ardhi. Naomba nianze kumpongeza Waziri wa Ardhi pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya; na Wizara hii kwa kweli wamejitahidi kuituliza kwa kiasi fulani.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri wanayoifanya Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, kuna changamoto mbalimbali ambayo sitaacha kuendelea kuwaambia ili waweze kuendelea kutatua na kuhakikisha kwamba wanazidi kung’aa. Kwanza kabisa urasimishaji wa makazi. Suala la urasimishaji wa makazi ni changamoto. Mmekuja na mpango wa kuwapa makampuni ili waweze kufanya urasimishaji wa makazi, lakini makampuni haya hayana uwezo, kwa sababu hawana wataalam mahususi wa kuhakikisha kwamba wanapima ardhi kwa manufaa ya wananchi. Wamekuwa kama ni matapeli fulani hivi ambao kule kijijini kwanza hawaeleweki, wakienda wanajifichaficha, hawana ushirikiano na viongozi vya wa vijiji, kata na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima, Wizara nzima wakaangalia eneo hili la urasimishaji wa makazi ikiwezekana waangalie yale makampuni ambayo hayana uwezo, lakini pia waongezee Halmashauri ili iweze kushirikiana kuhakikisha kwamba wananchi wanapimiwa ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la wawekezaji kutumia mashamba makubwa kukopa fedha katika Taifa letu na hatimaye kuingia mtini watakapokuwa wamepata hizo fedha. Hili ni suala la kuangalia kwa makini kwa sababu wawekezaji wanakuja wakisema tunawekeza, lakini mwisho wa siku wanakopa fedha kwenye benki zetu na kwenye taasisi zetu za fedha na baadaye wanatoweka na fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe mfano mmoja. Kuna shamba moja kwenye Jimbo langu la Arumeru Magharibi Lucy Estate. Mwekezaji huyu alikopa fedha kutoka Benki ya Standard Chartered na baadaye wakakopa NSSF kiasi cha shilingi zaidi ya bilioni tisa, wametoweka, hakuna uwekezaji wala chochote. Wakati huo huo, baada ya kuona Standard Chartered inataka kuuza hilo shamba na NSSF waliamua kuweka objection mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaona kwamba tunapata hasara kwa sababu ya mali yetu. Shamba ni letu, fedha tumewakopesha, kwa nini tunawaachia hiyo loophole kiasi hicho? Naishauri Serikali kwamba ni vizuri kama mwekezaji anakuja; tuseme umekuja unataka kuwekeza Tanzania kuhusu masuala ya ardhi, basi uwe na asilimia 50 na unachotaka kuwekeza, ndiyo uweze kukopa kwenye Benki zetu na taasisi. Vinginevyo tutaendelea kupoteza ardhi na mwisho wa siku wananchi hawatakuwa na faida na Serikali yetu haitakuwa na faida yoyote. kwa hiyo, naomba Waziri atakapokuja atuambie hili eneo la wawekezaji kutumia loophole hiyo, hatusemi wawekezaji ni watu wabaya, ni wazuri lakini sheria zetu tutaliangalia vipi ili ziwe na manufaa?

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni mashambapori. Kwa mfano, shamba hilo la Lucy sasa ni zaidi ya miaka kama 15, liko, ni shamba zuri, lina rutuba Arusha, hakuna elimu; shamba la Gomba Estate liko pale, ni shamba zuri halilimwi, lakini nazungumzia kilimo. Nitazungumziaje kilimo kama tunaweza kuacha maeneo mazuri kama hayo bila kutumia kwa manufaa ya wananchi wetu ili kuongeza ajira, kukuza uchumi wa nchi yetu? Tunasema kilimo, tunatunza ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri pia maeneo haya ayaangalie kwa sababu inaumiza sana, wananchi hawana ardhi, lakini ardhi inalala miaka 15, 20, 30 hailimwi na ni ardhi ambayo inalimika vizuri, inaingia kila aina ya mazao, inasikitisha na inakera.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shamba la Aga Khan ambapo walisema wanajenga Chuo Kikuu tangu mwaka 2006. Wameng’oa kahawa na hilo shamba lilikuwa linaajiri zaidi ya watu 1,500 mpaka 2,000; wameng’oa kahawa, wamefanya nini, wamesema wanajenga Chuo Kikuu tangu 2006, hawajajenga Chuo Kikuu mpaka leo. Je si ukiukwaji wa Sheria za Ardhi Na. 5 na Na. 4 za Ardhi na sheria nyingine za umiliki? Ni kwa nini Mheshimiwa Waziri sehemu hii usiiangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili shamba wananchi wanalilalamikia ni zaidi ya ekari 4,000 kasoro limekaa; kwa sababu gani? Ni eneo ambalo linaingia aina ya mazao yote, ilikuwa inalimwa maharage, ilikuwa inalimwa ngano na mazao mengine mengi; maua na kadhalika. Wananchi walikuwa wanapata ajira; na Serikali sasa hivi haipati kodi kutokana na mazao ambayo yangelimwa pale hakuna. Tumeacha, tumenyamaza: Je, Aga Khan tunawaogopa, siamini kama Mheshimiwa Waziri Lukuvi anaweza kuwaogopa Aga Khan, kwa sababu hakuna mtu aliyeko juu ya sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wote tuko chini ya sheria, kwa hiyo, naomba eneo hili liangaliwe hasa katika shamba la Aga Khan. Naomba Mheshimiwa Waziri atembelee hilo eneo akague shamba lote aone. Asione tu kwamba sisi tunaongea kwa sababu labda tuna chuki, hapana. Tunataka kueleza namna na azima ya wananchi ambao tunataka Taifa letu liende.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shamba la Gomba Estate pia tumewapa JKT sawa, lakini je, wananchi ambao wako maeneo hayo, wao wanapata nini? Hili nalo tuliangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende eneo lingine la Mabaraza ya Ardhi. Mabaraza ya Ardhi inaanzia kwenye ngazi ya vijiji kwa maana ya Kushauri Kata na baadaye Wilaya. Mabaraza haya hasa katika ngazi ya wilaya kuna changamoto kubwa ya ucheleweshaji wa kesi. Kesi inaweza ikakaa mwaka mzima, miaka miwili, miaka mitatu mpaka minne. Hii siyo sawa, ni kuwakosesha wananchi haki. Hili nalo liangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa Mabaraza haya wanatakiwa waangalie namna ya kutoa circular kuwapa posho hasa watu wa kwenye ngazi ya Kata, wanateseka. Tunaepukaje rushwa? Tunasema tunaondoa rushwa kwenye mfumo wa Mahakama, kama watu hao hatujawawekea mfumo mzuri, kwa mfano ufunguzi wa kesi kwenye Baraza la Kata, hayo makatarasi wale watu wanapata wapi kama hakuna chochote ambacho wanapewa kwa ajili ya kuweza kufanya hivyo kazi na kuwaangalia pia namna ya kuwapa posho?

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la migogoro ya ardhi hasa baina ya wananchi na taasisi zetu za Umma imekidhiri. Kwa mfano, kuna mgogoro wa Kata ya Oldonyosambu, wananchi wale waliondolewa kutoka Oldonyosambu Jeshi letu likachukuwa eneo hilo. Ni vizuri sana kwa sababu ni kwa manufaa ya Taifa letu, lakini sheria inasema, mtu unapotaka kuchukuwa ardhi , mmiliki lazima apewe fidia. Tunaomba Serikali ihakikishe kwamba inapotaka kuchukuwa eneo, iwape wananchi fidia na wale wananchi wale wananchi wa Odonyosambu wakumbukwe k wa sababu hii ni haki yao ya msingi. Kuwaondoa bila kuwapa haki yao, siyo sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wananchi na Nengun’g Kata ya Musa walishinda kesi Mahakama Kuu toka mwaka 2016, lakini taasisi yetu ya TMA imeng’ang’ania. Ni kwa nini tusiheshimu sheria? Naomba hii migogoro itatuliwe kwa sababu wananchi wanajiona hawana haki na wakati naamini kwamba chini ya Chama cha Mapinduzi, chama chetu, kimetengeneza ilani ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata haki zao kikamilifu. Kwa hiyo, naamini hili litatendewa haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shamba lingine la Mlangalini Kiserya ,nao halikadhalika ni hivyo hivyo. Wananchi wamenyang’anywa kupitia Jeshi lakini bado hawapati haki zao, kutoka kule Kiserya Kata ya Mlangalini. Nayasema haya ili Mheshimiwa Waziri aweze kuona kwamba kuna haja ya kuangalia hayo maeneo kwa kushirikiana na Wizara nyingine kutatua hii migogoro, maana haileti picha nzuri kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni suala la mabenki kukataa kutoa mikopo kwa kutumia hati miliki ya kimila. Benki nyingi zinakataa hiyo hati kwa sababu wanasema haina value. Sasa ni vizuri Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla tuangalie hati hii, tusije tukawa tunasema tuweke tu hati ya kimila lakini wananchi hawanufaiki. Mtu kuwa na hati ni kwa ajili ya kumsaidia kupata mikopo na mambo mengine mengi. Kwa hiyo, kama haina value, basi Serikali iseme wazi kwamba hii hati haina value. Kwa hiyo, wananchi wasihangaike kuiweka, lakini naamini kwa sababu Serikali ilikuwa na nia njema, hati hiyo lazima ina value.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba baadaye pia Mheshimiwa Waziri atakapokuwa ana-wind-up, atueleze hiyo hati ni kwa nini mabenki hayapokei na kuna benki nyingine zinasema labda tunaweza tukawapa shilingi milioni tatu tu, mwisho wa hiyo hati. Sababu hakuna. Kwa hiyo, bado kuna changamoto katika hiyo hati.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)