Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa nafasi na mimi niungane na wachangiaji waliotangulia kuipongeza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kazi nzuri wanayoifanya ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwamba Jeshi la Ulinzi limekuwa likifanya kazi kubwa na hasa katika Wilaya na Majimbo ambayo yapo mipakani mwa Nchi yetu kama Mheshimiwa Waziri alivyosema katika hotuba yake na Wilaya ya Misenyi ni mojawapo ya sehemu ambayo Wizara ya Ulinzi imefanya kazi kubwa kuhakikisha amani na usalama ndani ya Wilaya yetu ya Misenyi inakuwepo na hasa katika eneo la kudhibiti wahamiaji ambao walikuwa wanatoka nchi za jirani kuja kufanya machungo ya mifugo yao ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri hiyo katika eneo hilo, tunaomba maboresho kidogo katika Jeshi letu la Ulinzi. Ukiangalia katika eneo ambalo lipo mpakani kabisa eneo la Kata ya Kakunyu, vijiji vya Kakunyu, Bugango na Bugwenkoma; mpaka wa Jeshi letu upo karibu kilometa 20 kutoka mpakani, maana yake unaacha vile vijiji nyuma na nchi ya Uganda halafu wenyewe mpaka upo mbele ya vijiji. Kwa kweli pamoja na kazi nzuri ya Jeshi letu wananchi wamekuwa wakipata taabu sana kwasababu kweli lazima Jeshi letu lijiridhishe unapokuwa unatoka eneo hilo kuja Makao Makuu ya Wilaya, kwa hiyo katika msafara huo unakuta na baadhi ya wananchi wanapata kero ndogo ndogo ambazo zinaweza kudhibitiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe sana, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri unajua kabisa Wilaya ya Misenyi ilitenga maeneo mazuri kule kwenye mpaka kabisa zipo heka za kutosha. Mimi ningeshauri Wizara yako ione sasa ule mpaka ambao upo katikati baada ya vijiji uweze kuhamia katikati ya nchi ya Uganda na Tanzania ili wananchi wetu sasa vijiji hivyo nilivyotaja wawe huru kuendelea na shughuli zao na pale wanapokuwa wanakwenda Wilayani basi wasipate bughudha nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma Randama ya Wizara ya Ulinzi, tunaona kazi nzuri wanayoifanya na hasa katika eneo la ushirikiano na mamlaka za kiraia. Kuna kazi nzuri zimefanyika, lakini katika eneo hilo, kuna suala lingine ambalo ningeweza kushauri Wizara iboreshe. Ni mahusiano au utatuzi wa migogoro kati ya jeshi letu ulinzi na wananchi. Wilaya ya Misenyi wote tunajua kwamba ulikuwa ni uwanja wa vita vya Kagera ambavyo vilihitimishwa mwezi Juni, 1979. Kwa hiyo, umeacha maafa mengi sana katika eneo hilo na wananchi wanapokuwa wanaendelea mambo hayo kuyaona wanahisi bado tupo ndani ya vita.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1978 Jeshi letu lilikuja na wananchi walikuwa tayari kujitoa kwa ajili ya kutoa rasilimali kuwezesha jeshi letu ili kupigana vile vita ambavyo kimsingi sisi wananchi tulikuwa na maslahi nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Kyaka, Kijiji cha Kurifani, Kitongoji cha Biawamara wananchi walitoa maeneo yao kwa ajili ya kuhakikisha jeshi letu linakaa salama, linaweka nyenzo zake, zinapigana vita vizuri. Na wananchi walitoa eneo ambalo lenyewe lilikuwa liko wazi na wao wakabaki na mashamba yao na miji yao maisha yakaendelea. Jeshi likatulia pale likafanya kazi nzuri iliyotukuka na tukafanikiwa kumkimbiza Nduli Iddi Amini nje ya mipaka ya Tanzania, lakini pia na kuwakomboa Waganda. Baada ya miaka baadaye sasa Jeshi limebadilika likawa mwenyeji wale wanachi wamekuwa wahamiaji. Maana yake sasa hivi wananchi ndio wanavamia eneo la jeshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha kidogo, katika eneo hilo eneo ni kubwa mno na eneo ni pori kubwa mno, wananchi wana mashamba yao na miji yao, lakini hata hiyo miji hawaruhusiwi kuendeleza, huruhusiwi kulima, huruhusiwi kufanya chochote, kwamba ni eneo la jeshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nikuombe kupitia kiti chako, Serikali ya Wilaya imeandika sana kupeleka suala hili Wizara ya Ulinzi kwa Katibu Mkuu, lakini kitu chochote ambacho kimefanyika mpaka leo. Mimi mwenyewe nimekuja hapa Bungeni nimemuandikia Mheshimiwa Waziri ki-note kwamba kule Misenyi, Kyaka, Kyawamara kuna matatizo haya nafikiri kwa sababu ya majukumu yako naomba ulifanyie kazi na nikuombe Mheshimiwa Waziri twende kule ukaone hali mwenyewe kwa sababu hii ni hali ambao inatatulika ukienda mwenyewe pamoja na wasaidizi wako tuweze kuwaokoa wananchi, kutowagombanisha na jeshi letu ambalo linafanya kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Katika suala lingine Wilaya ya Misenyi, kuna eneo ambalo tulikuwa wahanga ambapo mabomu ya Iddi Amini kweli yalikuwa pale na yakabomoa eneo la kanisa, kwa sasa hivi yaliyobaki ni magofu. Tunaishukuru Serikali tukufu ambayo imeweza kujenga Kanisa na wananchi waliendelea na ibada zao katika eneo lingine. Eneo hilo liko kati kati ya Kata ya Kyaka ambayo ni mjini kabisa ambapo sasa kwa sababu lipo katika eneo la mwinuko inaonekana katika kata nzima ambayo ni mjini pale. Sasa mahema hayo yamebakizwa ni magofu ambayo ni vipande vya kuta vya hilo kanisa ambalo lilikuwepo enzi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wakiangalia yale mabaki wanahisi kama vita vinarudi au hatuna mahusiano mazuri na nchi ya Uganda au kuna nini ambacho Serikali isingeweza kutengeneza eneo hilo likawa ni zuri, likawa la kivutio la kumbukumbu nzuri badala yake limekuwa ni magugu yamejaa pale na mwananchi akikosea kidogo akapita katika eneo hilo, hivyo viboko atakavyoambulia siyo vya nchi hii.

Kwa hiyo, mimi niombe sana na niishauri Serikali eneo hilo linaweza kufanyiwa matumizi mawili either Jeshi likawekeza sehemu nzuri ya kuweza watu kupumzika pale. Ni view nzuri ya Mto Kagera ambayo kila mmoja anauona Mto Kagera kwa kona zake na Daraja la Mto Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama Jeshi haliwezi, linaweza likatoa eneo hilo kwa Serikali ya Wilaya kwa Halmashauri ikawekeza kitu kizuri na wananchi au ikawa ni eneo la open space wananchi wakawa wanapumzika pale. (Makofi)

Kwa hiyo niombe sana jeshi letu liweze kuangalia masuala haya kwa mapana na hiyo ni sambamba na uwanja wa mashujaa ambao Mwalimu Nyerere alipokea wanajeshi wetu kutoka Uganda baada ya vita. Na eneo hili lipo kati kati ya nji, ni pori, ni nyasi ndefu na hivyo unakuta inaleta taswira mbaya pale maana yake inaonekana ni eneo la jeshi lisilofanyiwa usafi, ni eneo la jeshi lisiloendelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niomb jeshi letu pamoja na kuwa na haki yakutunza maeneo yake ya kumbukumbu na kihistoria kwa sababu mahali pale sio sehemu ya vifaa vya kijeshi, kwa mfano; uwanja huo wa mashujaa umeshazungukwa na Halmashauri, umezungukwa na wananchi, unawezekana ukawekezwa katika taswira nzuri, ukaendelea kumilikiwa na jeshi, lakini ukatumia kwa shughuli za Kiserikali kama ambavyo wanatumika. Ni eneo ambalo viongozi wetu wa Kitaifa wakija pale tunafanyia mikutano. Tukiwa na makongamo tunafanyia mikutano pale, lakini kwa kweli ukiuona uwanja huo ni uwanja ambao haupo nadhifu na kwa kweli ukisema kwamba majeshi yetu yalikuja yakapokelewa na Mheshimiwa Amiri Jeshi Mkuu wakati huo inakuwa haileti tija nzuri kwa taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe sana, mheshimiwa Waziri pamoja na Wasaidizi wake baada ya kipindi hiki cha Bajeti twende Wilaya ya Misenyi wakakague sehemu ya Byawamara, maeneo ambayo yanaleta changamoto kwa wananchi, wakaangalie lile eneo la kanisa ambalo limebaki kama kumbukumbu, wakaangalie uwanja wa mashujaa ndani ya Wilaya ya Misenyi, uweze kuwekewa mkakati madhubuti viboreshwe na viweze kuwa ni kumbukumbu njema kwa ajili ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuwashukuru Jeshi wanaendelea kufanya kazi, sisi ambao tupo mipakani tunaona mchango mkubwa wanaoufanya na niendelee kumshukuru pia na Mkuu wetu wa Wilaya lakini kimsingi ni tunda la Jeshi ambaye ni Kanali Dennis Mwila ambaye amekuwa ni nguzo kubwa katika eneo letu kuhakikisha ulinzi wa Wilaya ya Misenyi unakuwepo. (Makofi)

Kwa hiyo, nipende pia kusema kwamba baadhi ya maeneo kama wachangiaji wengine walivyosema tunahitaji kuwa viongozi ambao wamepitia katika vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanaweza kulindwa vizuri na amani wananchi hao inaendelea kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nikushukuru kwa nafasi naunga mkono hoja. Niombe basi Mheshimiwa Waziri baada ya majukumu hayo akaitembelee Wilaya ya Misenyi tuweze kutatua hizo changamoto za wananchi. Nakushukuru. (Makofi)