Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami nichukue nafasi hii kuchangia katika maeneo kama matatu hivi. Kwanza kabisa, nitachangia kuhusu upandikizaji wa watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwanamke au familia kukosa mtoto linaumiza sana. Mwanamke asipokuwa na mtoto anaumwa mno, na ni ugonjwa. Kisaikolojia na hata maisha kwa ujumla kwake hayana amani. Sasa kuna huu upandikizaji wa watoto nje ya nchi. Mtu hana mtoto, anajaribu kwa madaktari hapa, wanasema wewe lazima ukafanyiwe upandikizaji. Sasa hii ya upandikizaji inachukua fedha nyingi mno. Wanawake hawawezi kwenda China wala South Africa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya, hebu tuwasaidie wanawake kama tunavyosaidia magonjwa ya moyo na figo, watu wanasaidiwa, wanakwenda nje. Basi hata kama ni shilingi milioni 20, Serikali ichangie angalau nusu na yule mtu aambiwe na wewe saidia ongeza kiasi. Kwa kufanya hivyo, tutasaidia wanawake wengi sana. Pia Serikali ianze kujipanga. Tutakwenda kutafuta watoto huko nje mpaka lini? Ndiyo maana kunatokea maneno kwamba unajuaje kama zile mbegu ni za mume wako? Kwa sababu unaenda kupandikizwa kule nje, labda watachukua mbegu nyingine, wataweka ili mradi mtu arudi na mtoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali ianze kujipanga katika utaalam huo, tuwe na maabara hapa Tanzania, nasi tuanze test tube babies, tuianze wenyewe hapa Tanzania. Haya mambo ya kwenda nje yatatuletea matatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, naipongeza sana Serikali, ilipofanya zoezi la tohara hasa kwa watani zangu kule Tabora, Mwanza, nasikia hata huko Sumbawanga, hili jambo lilikuwa ni zuri kwa manufaa ya afya na hasa katika kupungiza maambukizi ya Ukimwi. Sasa wamefanya hiyo kazi ya tohara ya wanaume vizuri sana, naomba sana Serikali ijipange kumaliza kabisa tatizo la ukeketaji wa wanawake katika mikoa ambayo bado ukeketaji unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepata ushahidi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, anasema licha ya juhudi zile zote; seminars na workshops bado watoto wanakeketwa. Sasa Mheshimiwa Ummy alifanya, alijitahidi sana, mimi leo nawaomba na wanaume mtusaidie kupiga kampeni kwamba msichana au mwanamke aliyekeketwa hataolewa. Mkianza ninyi, itasaidia kwa sababu asili ya mwanamke kukeketwa ilitokana na wanaume kutaka kuwagandamiza wanawake wasipate hisia katika tendo la ndoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kidogo nieleze, tunaliona hili jambo ni rahisi sana au la kawaida. Nimefanya utafiti, hawa wanawake waliokeketwa ukiongea nao inasikitisha. Kwanza wana madhara yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanamke aliyekeketwa anapewa ulemavu makusudi. Unamkata mtu kidole hiki cha mwisho makusudi tu, hawezi kufa lakini hawezi kushika ugali vizuri. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sina nia ya kuwachekesha lakini nasema ukweli kisayansi. Imagine mtu akikukata ulimi hapa mbele, hutakufa lakini huwezi kuonja. Kwa hiyo, wanawake hao kwanza wanapata ulemavu, kwa sababu wanaondolewa kiungo ambacho akipaswi kuondolewa. Yaani ile ni kama kufyeka; na sehemu nyingine wanafyeka mpaka zile labia minora sasa hilo ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maumivu makali, ulemavu, halafu wanawake hao wakiingia katika kuolewa, wanabakwa kwa sababu hawasikii kabisa, nisemeje kwa Kiswahili? Hawasikii hisia na hawafikii orgasm. Sasa huyo mwanamke anaishi maisha yote. Mmoja aliniambia, nimezaa watoto watano mwanangu, sijui mnachosema eti kuna raha na furaha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni shida sana. Wengi hupata ulemavu, maumivu makali wakati wa kujifungua, wakati mwingine lile kovu sasa linaweza likachanika. Hawa wanaweza kupata Ukimwi, kwa sababu vile visu siyo kwamba wanabadilisha. Sijui wanatumia visu au mapanga, mimi sijui. (Kicheko/Makofi)

MBUNGE FULANI: Eeh! (Kicheko)

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, wengine wanapata Ukimwi, tetanus na magonjwa mengine. Halafu waki-bleed sana lazima watakuwa anemic. Kwa hiyo, hayo ni madhara. Naiomba sana Serikali sasa hivi itoe tamko, Wizara ya Afya pamoja na Katiba na Sheria, mtoe tamko la kutokomeza kabisa kama tulivyoweza kutokomeza wale waliokuwa wanawachinja albino. Wale wanaowaita mangariba, bado wapo na huo ukeketaji umehama kwenye ile mikoa huko mpaka Dar es salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu wengi mnajua kuna kundi lile ambalo linatoka Mara, liko Ukonga na Segerea. Kuna watoto kule walitoroka; nina uhakika na nina Ushahidi kwamba watoto wawili walitoroka kukimbia kukeketwa. Kwa hiyo, naliomba sasa ulibebe Waziri wa Afya tufanye kampeni, tuandike andiko zuri kutumia hata celebrity wetu, hilo litapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, Kituo cha Afya, Mkwawa University kinahudumia watu zaidi ya 50,000. Namwomba sasa Waziri, ikiwezekana tuongozane akaangalie pale. Kinatakiwa kipandishwe sasa kiwe Hospitali kwa sababu kinahudumia watu wengi. Hiyo itasaidia sana kupunguza msongamano kwenye ile hospitali ya mkoa pamoja na Hospitali ya Rufaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho tiba asili zinatusaidia, tiba mbadala zinatusaidia, lakini sasa hivi hizo dawa ni ghali mno. Mtu akishindwa kupata dawa hospitali, akaenda kule anaambiwa shilingi 50,000, au shilingi 100,000. Kwa hiyo, naomba Wizara hapo ikae vizuri na hao watu wa tiba asili hizi ambazo mmezitambua, bei zao zishuke. Maana yake mtu anakubali kwenda kule ili aishi. Sasa bei yao ni kubwa sana kuliko hata bei ya dawa za hospitali ya kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)