Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Afya. Kwanza nianze kwa kuwapongeza Wizara hasa Waziri na Naibu kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee hospitali yangu ya Mkoa wa Morogoro ambayo nilishaiongelea hapa ndani. Kwanza napongeza kwa upanuzi ambao wanaufanya kwenye hospitali hii ila ni upanuzi wa kwenda juu. Kwa hiyo sehemu ya hospitali ile kama wanavyojua Hospitali ya Mkoa wa Morogoro inapokea wagonjwa wengi hapo na majeruhi wengi sana, kwa hiyo sehemu hiyo haitoshi. Hapa nilishaomba kuwa kijengwe kituo au hospitali kubwa ya kisasa ya Morogoro ambayo inaweza ikapokea wagonjwa wengi na majeruhi wengi ambao huwa wanapokelewa hapo kutoka kwenye mikoa mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hospitali hii ni kubwa lakini haina CT-SCAN. Kutokana na matatizo yaliyo hapo nilishaongea na Mheshimiwa Naibu Waziri na Waziri wakaniambia kuwa CT-SCAN ipo kwenye meli inakuja, sasa je, imefikia wapi na itafika lini hapa hospitalini Morogoro au itakaa bandarini mpaka lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo kwenye Hospitali yetu ya Morogoro tunaloomba kutokana na umuhimu wa hospitali hii ni mtambo wa oxygen ambao nilishaongea na wenyewe, nikaambiwa kuwa nitaambatana na Naibu Waziri aende kunionesha mahali pa kujenga hicho kituo cha mtambo wa oxygen. Mheshimiwa Waziri akija kuhitimisha hapa aniambie kwamba ni lini tutaambatana na Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri kwenda kuona hicho kituo cha oxygen kitakapojengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naomba kuliongelea kwenye Hospitali hii ya Morogoro ni wataalam Mabingwa, nalo naomba liweze kuangaliwa kwenye Hospitali yetu hii ya Morogoro ambayo inatibu wagonjwa wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nimekumbana nalo, naomba nisisitize sana kuhusu upungufu wa dawa kwenye hospitali zetu na upungufu wa dawa kwenye vituo vyetu vya afya. Upungufu wa dawa kila mahali ni tatizo. Hata hivyo, nashukuru Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake amesema viwanda vinajengwa vya kutengeneza dawa, basi naomba viangaliwe ili basi tatizo hili liweze kupungua kwa sababu limekuwa kubwa sana kwenye nchi yetu na kila mmoja anazungumzia upungufu wa madawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye taarifa ya Serikali wanasema dawa zipo, lakini namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Doroth naye tuliongea mara nyingi kuhusu upungufu wa dawa, naye akakiri kweli kuwa atafuatilia upungufu wa dawa na wale wote wanaoiba dawa atawafuatilia. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba aliangalie hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo kwa uharaka naomba kulizungumzia ni Bima ya Afya. Unakuta mtu amelazwa ICU anaandikiwa dawa ya kutibiwa wakati yeye amelazwa, yaani anaumwa sana kwa sababu kupelekwa ICU ni kuwa unaumwa sana, lakini unaandikiwa dawa ambazo hazipatikani, inabidi eti uende kununua, inawezekana hiyo? Kwa hiyo naomba hiyo Bima ya Afya nayo iangaliwe, iendane na madawa yanayotolewa pia na Bima ya Afya kwa wote ijulikane ni lini itaweza kutolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee utafiti, uangaliwe...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagogwa Mheshimiwa.

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana lakini utafiti ufanyike kwa magonjwa ambayo…

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

NAIBU SPIKA: Kwa magonjwa ambayo…

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa magonjwa ambayo hayaambukizi yakiwepo kisukari, kansa, pressure, ugonjwa wa Ini na figo naomba utafiti ufanyike sio kutuambia kuwa hayatibiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)