Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja kwenye matendo haya ya ukatili wanayofanyiwa Watanzania wenzetu. Kwa kweli inasikitisha sana ukiona Watanzania wenzetu na hasa akinamama na Watoto; katika takwimu ambayo Waziri ameisoma kwamba katika matukio 134,310 takribani matukio 106,196 wamefanyiwa akinamama na watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, sio hayo tu matukio, kuna matukio mengine yanafanyika huko wala hayarekodiwi popote, lakini jamii hii inaendelea kuteseka, inaendelea kuathirika kisaikolojia, wengine wanapoteza Maisha, wengine wanabaki na ulemavu wa maisha moja kwa moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepita juzi huku Babati na maeneo mengine kuna kesi ambayo mpaka akinamama wa UWT wameishikia kidedea. Kwa mfano jana kulikuwa na kesi pale Babati ya mtoto katika familia mama ana watoto wake na mtoto wa ndugu yakem lakini imepotea shilingi 1,500 alichokifanya ni kuchukua shilingi 200 kuiweka kwenye jiko la mkaa ilivyokuwa nyekundu amemwekea yule mtoto mkononi yule anayetaka kumwadhibu, mkono umeungua, kesi ile imepelekwa polisi, bahati nzuri tumechangia kuwasafirisha wale. Matukio kama haya ni mengi, lakini kinachofanyika, kesi kama hizi ambazo tayari zina ushahidi baadaye watakubaliana zitakwenda kwa wazee, zitaongelewa zitakwisha, pamoja na kesi za ubakaji na mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ku-create awareness, watu ambao wanaweza kuisemea wakahamasisha jamii sasa kutokomeza kabisa ni hawa Maafisa Ustawi wa Jamii ambapo sasa wapo wachache. Wilayani utamkuta Afisa Maendeleo ya Jamii au Afisa Ustawi yupo mmoja, kesi hizi ni nyingi, anashindwa kufuatilia, jamii inashindwa kuona wajibu wake. Naomba sasa Wizara hii kwa sababu kitengo hiki kipo kwao waongeze ajira ya Maafisa Ustawi wa Jamii, wafuatilie ili kwa pamoja tuweze kutokomeza matendo haya ya ukatili wanayofanyiwa Watanzania wenzetu pamoja na kuwasaidia vifaa vya usafiri na mengineyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachangia tena kwenye matibabu ambayo yanatolewa nchini kwetu. Kwanza ninaipongeza sana Wizara na Serikali yangu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba kuna matibabu ya dialysis yalikuwa hayatolewa ndani ya nchi yetu, alikuwa mwathirika au mgonjwa anayetakiwa kutibiwa lazima asafirishwe kwenda nje. Kwa hiyo utaona kwamba ni familia zenye uwezo ndizo zilikuwa zinaweza kumsafirisha mgonjwa wake kwenda kutibiwa nje. Naishukuru Serikali kwamba sasa huduma hii inatolewa nchini, lakini ni katika maeneo machache, ni hospitali kubwa, kwa mfano matibabu haya yanatolewa Benjamin Mkapa, KCMC, Bugando na Muhimbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, matibabu hayo yanatolewa, mtu akishakuwa anatibiwa anatakiwa kwenda angalau mara mbili, tatu kwa wiki, kwa hiyo kinachofanyika familia yenye mgonjwa kama huyo kama anatibiwa katika Hospitali ya Benjamini Mkapa inabidi wahamie Dodoma wapate pa kuishi, lazima mwanafamilia mmoja akae na mgonjwa na kwa hiyo inaathiri familia nzima kiuchumi na kila kitu na isitoshe matibabu haya ni ghali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara sasa ni kwa nini sasa matibabu haya yasitolewe katika Hospitali zote za Mkoa ili kuwarahisishia Watanzania angalau wapate matibabu haya karibu na mikoani na Hospitali hizi za Kanda. Vile vile waangalie gharama hizi zipunguzwe. Najua kuna changamoto kubwa sana za wataalam wanaoweza kutoa matibabu haya. Namwomba Waziri husika wa Wizara hii awapeleke mafunzo Madaktari pamoja na wataalam ili tuwe na wataalam wengi wa kutosha na matibabu haya yaweze kupatikana angalau katika Hospitali za Mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine la mwisho, naomba nichangie kuhusu bima ya Afya, watu wengi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele imeshagongwa Mheshimiwa.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)