Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa namna ya pekee kwa kunipa nafasi ya kuchangia asubuhi hii kwenye Wizara ya Maji kama ambavyo hoja iko mezani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri. Naamini imetokea hii kwa sababu ya umahiri wa wasaidizi wake akiwemo Naibu Katibu Mkuu, mama yetu tulimwona hapa mchana na kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwenye utendaji wao wa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na nichukue pia nafasi hii kumpongeza Meneja wa MANAWASA Masasi, Ndugu David pamoja na Meneja wa Wilaya wa RUWASA Masasi Eng. Juma kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa sababu ni wasaidizi wake na tunapokuwa na shida wakati fulani tunakwenda kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niyaseme machache kwa maana sasa ya kutaka kuboresha kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri. Nimesikia hapa unatajwa mradi wa maji wa Ruvuma. Sina uhakika sana kama Mheshimiwa Waziri wewe mwenyewe umefika pale, lakini mradi huu ni ukombozi mkubwa sana hasa zaidi kwa sisi wakazi wa Mtwara kwa maana ya Mkoa, Wilaya ya Masasi na hasa Jimbo la Ndanda, kwa sababu utaenda kuangazia kwenye Kata za Usikisi na Matutwe, Mpanyani pamoja na Majani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokiomba kikubwa kwa Mheshimiwa Waziri, mradi huu utekelezaji wake basi uwe wa haraka kwa sababu shida ya maji anaifahamu na ukiangalia katika statistics katika mikoa karibu yote ya Tanzania, Mkoa wa Mtwara ndiyo uko chini kabisa kwenye upatikanaji wa miradi ya maji. Naye ni shahidi, amekuja kule mara nyingi, tumefanya kikao pamoja naye kama Wabunge wote wa Mtwara kwa ushirikiano wetu ili kuweza kusisitiza kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee kabisa, naomba pia ukamilishwaji wa miradi inayoendelea kwa sababu nayo isije ikawa chechefu. Kuna mradi wa Liloya, Chikukwe utakaohudumia vijiji 26. Mpaka sasa uko pale kwenye asilimia 75 au 80. Tunaomba Mheshimiwa Waziri utakaposimama basi utueleze ukamilishaji wake utakuwa lini kwa sababu unasaidia eneo kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua nafasi hii pia kushauri kwamba pafanyike maboresho makubwa kwenye mradi wa maji wa Ndanda kwa sababu eneo hilo limekuwa linakua kila siku na linaongezeka. Wananchi wale wanahitaji maji ya kutosha. Kwa hiyo, tuhakikishe na mradi ule nao unaboreshwa na kukamilika kwa kushirikiana na engineer wetu wa RUWASA wa Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina jambo moja ambalo pia napenda nimshauri Mheshimiwa Waziri kwa ruhusa yako. Tunajua kwamba kuna mtandao wa umeme wa Taifa ambao unaitwa National Grid, lakini sidhani kama Wizara imeshawahi kufikiria kwamba tunahitaji kuwa na mtandao wa maji na wenyewe wa Kitaifa. Kwa sababu tuna Ziwa Tanganyika Tutakapoamua kulitumia Ziwa Tanganyika, Mto Rufiji, Mto Ruvuma, Lake Nyasa pamoja na Lake Victoria tunaweza tukaapata mtandao mzuri sana wa maji wa Kitaifa badala ya hali iliyoko sasa tunahangaika na small water ports ili iweze kusaidia wananchi katika eneo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naeleza hapo mwanzoni kwamba Jimbo la Ndanda limegawanyika katika mazingira mawili; upande huu wa Mashariki tatizo la maji siyo kubwa sana kama ambavyo iko upande wa Magharibi. Bahati nzuri pamoja na kwamba nimepata nafasi ya kuchangia, tumekuwa tunakaa na Waziri kila mara kujaribu kushauriana namna ya kusaidia zile Kata nilizozitaja. Nami namwomba kabisa Waziri kwa makini kabisa ahakikishe miradi hii inatekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua kuna ahadi ya visima, kusuluhisha hili jambo kwa muda mfupi, tumepata visima kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, lakini sasa tunataka tupate maji ya uhakika. Ndiyo maana unapokuja mradi wa Mto Ruvuma tunaufurahia sana kwa sababu tunaamini utakuwa ni suluhisho la kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa kuna tatizo. Sasa hivi tunapata misaada kutoka kwa wafadhili mbalimbali kwa ajili ya visima na wakati mwingine kupata hata network ya usambazaji wa mabomba katika maeneo fulani. Nilikuwa hapa na marafiki zangu, mliwaona asubuhi ambao ni watu wa Relief Partners International kutoka Texas, Marekani na shirika lao lingine la Thirst No More. Kumekuwa na malalamiko kidogo kwamba mara nyingi wanapoleta vifaa Tanzania kwa ajili ya kuja kusaidia watu wenye haja ya maji, vinapofika kwenye maeneo kwa ajili ya kutaka kuvi-clear wanakuwa wanatozwa kodi kubwa sana kana kwamba wao wanakuja pia kufanya biashara wakati purely wanavileta kwa ajili ya msaada kutoka kwenye michango ya wafadhili kule kwao. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri hebu angalia namba ya kurekebisha hizi tozo. Badala ya kuwatoza gharama kubwa sana, pesa hiyo ingeweza kuleta hata visima vingi kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naweza kutoa tu mfano eneo la Ndanda kama ambavyo nimesema toka mwanzo. Tumefanikiwa kupata visima vitatu kwa wafadhili hawa japokuwa wameahidi kupata vingi zaidi. Ila wanavyojaribu ku-import vitu hapa kwa ajili ya kusaidia; walileta rig hapa, wamelipa kodi karibu dola 60,000. Wanaleta vifaa kwa maana ya pumps, wanasema ukinunua pump tatu Nairobi, gharama ile ni sawa sawa na kununua pump moja Tanzania. Kwa hiyo, gharama zetu sisi ni kubwa zaidi kuliko ambavyo inafanyika Nairobi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wao mara nyingi wanapenda kwenda kununua Nairobi, halafu waje kutumia Tanzania kwa sababu ya ku-save, lakini bado wanapofika border kuna utaratibu unafanyika wa kujaribu kuthaminisha kwamba kwenye SH kodi fulani ambayo inatumika Tanzania pump hii thamani yake ni shilingi 700,000/=. Kwa hiyo, kodi yake itakuwa hivi. Ila kimsingi, wao hawajanunulia Tanzania, wanaingiza kutoka nchi ya jirani kwa maana ya Nairobi (tutolee mfano) lakini bado wanatakiwa walipe kodi kana kwamba wamenunua Tanzania. Kwa hiyo, kodi zinakuwa juu, wanashindwa kutimiza malengo yao na wale wanapata pesa kutoka kwa wafadhili lakini gharama za miradi zinakuwa kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, jambo lingine kama alivyosema Mheshimiwa Eng. Ezra Chiwelesa katika suala la viunganishi, katika miradi hii ya maji ukiiangalia, sehemu kubwa ambayo inachukua gharama kubwa sana ni kwenye masuala ya viunganishi pamoja na masuala ya mabomba.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna miradi mingi katika maeneo mbalimbali na nita-cite tena mfano wa Ndanda. Tuna mradi kwenye Kata Nanganga kwa maana ya Kijiji cha Mumburu na maeneo ya Mkwera. Kwa bahati mbaya sana mmeamua ku-centralize suala la manunuzi ambalo linafanywa na watu waliopo Mtwara Mjini ambao hawafahamu kabisa mazingira yaliyopo pale Ndanda, kiasi kwamba tunahamasisha wananchi wachimbe mitaro kwa ajili ya kulaza mabomba lakini mpaka mwishoni, mitaro ile inakuja kufukiwa na maji ya mvua kwa sababu mvua zinaendelea kunyesha maeneo haya na ukiuliza kwa nini? Wanasema mtu wa manunuzi kwa sababu anakaa mbali na eneo hili na anasimamia miradi mingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri ahakikishe Masasi tunapata mtu wa manunuzi ili kuweza ku-fast-track hii miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi wetu mwingine wa Chiwata. Kwa sababu Chiwata ni Kata ambayo iko nje kidogo pembezoni ya Jimbo la Ndanda, imejitenga na iko juu kabisa ya mlima. Tuna mradi pale wa thamani karibu shilingi milioni 400 utaanza kutekelezwa karibuni, lakini bado tunakaribia kwenda kumaliza mwaka, tumebakiza takribani mwezi mmoja na siku chache hizi zilizobakia, pesa hiyo haijaenda na mradi huo haujaanza kutekelezwa. Tunapata wasiwasi kwamba zitabakia siku chache zaidi halafu mtakuja kutuambia kifungu kile kimefungwa, tusubiri sasa mwaka wa fedha ujao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kama kuna taratibu za manunuzi zinachelewa zipelekwe hapo mapema, hizo pesa zitoke wananchi wale waweze kupata maji kwa sababu wamekuwa wanasubiri kwa muda mrefu na eneo hili limekuwa na kiu kwa muda mrefu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, nampongeza Mheshimiwa Waziri kama nilivyosema mwanzoni na sina mengi ya kusema katika Wizara yake kwa sababu tumekuwa tunawasiliana kila mara. Napongeza pia utendaji wa kazi wa watu wake akiwemo Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu kwa namna wanavyotupa ushirikiano; Engineer wetu wa RUWASA wa Wilaya pamoja na Engineer wa MUNAWASA wa kule Masasi kwa ushirikiano wao. Tumekuwa tunawafanyia vikao vya mara kwa mara pamoja na Madiwani kuhakikisha tunapata suluhisho la kudumu la maji yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na ninaamini kaka yangu na ndugu yangu hapa Mheshimiwa Aweso atakapokuja kujumuisha, atatueleza mikakati yake mahususi kabisa kwa ajili ya Mkoa wa Mtwara, kwa ajili ya Wilaya ya Masasi, kwa ajili ya Jimbo la Ndanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)