Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa nafasi na mimi niungane na wenzangu kupongeza Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na vyombo vyake kwa ulinzi mzuri wa nchi yetu. Tunajua tunajivunia tunu za Taifa na mahsusi kwenye upande wa amani tunajua Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na vyombo vyake wanachangia sana katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo kuna mambo kadhaa ambayo yanahitaji kuboreshwa ndani ya Wizara yetu hiyo ili ustawi wa wananchi uweze kuwepo katika sehemu mbalimbali za nchi yetu. Najua ni bahati kwa nchi au mkoa kuwa na ujirani na nchi zingine. Kwa mfano, Mkoa wa Kagera tunapakana na nchi tano; Uganda, Rwanda, Burundi, DRC na Sudan Kusini. Hata hivyo, wananchi wa Mkoa wa Kagera wamekuwa ni wahanga na hasa katika kutambuliwa na kupewa Vitambulisho vyao vya Taifa ili waweze kupata huduma zingine ambazo wanastahili kupewa kwa mfano kusajili simu zao. Pia tumeona Wizara ya Kilimo imekuja na utaratibu wa kusajili wananchi kulipwa fedha zao kupitia simu zao, huduma hizo wamekuwa wakizikosa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia Wilaya ya Misenyi, Kyerwa, Karagwe, Ngara wote tumekuwa wahanga wa kukosa vitambulisho na wananchi wanaishi kwa tabu kama vile hawapo ndani ya nchi yao. Suala hili limesababisha Mkoa wa Kagera ukadorora katika maendeleo. Mtu hawezi kufanya kitu kizuri, hawezi kulima shamba zuri, hawezi kujenga nyumba nzuri kwa sababu kesho ataambiwa wewe siyo raia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nijikite sana kwenye Wilaya ya Misenyi ambapo ndiyo jimbo langu. Kuna familia baba ameambiwa siyo raia, mama ni raia, mtoto wa kwanza ni raia, wa pili siyo raia. Sasa mpaka tunaleta mtafaruku katika familia, watu wanaenda kutafuta hata vinasaba maana baba anamuuliza mama huyu sasa ambaye siyo raia ni wa nani?

Mheshimiwa Spika, kwa Wilaya yetu ya Misenyi ukitaka kumpima mwananchi kwa kuongea Kiswahili au kuimba Wimbo wa Taifa sisi wote siyo raia. Hii ni kwa sababu mimi naongea Kihaya, Mnyankole akiongea Kinyankole tunaelewana bila shida. Sasa unaponipima kwa kusema kwamba niongee Kiswahili au niimbe Wimbo wa Taifa, hatuwatendei haki. Sisi wote ni mashahidi tukipangana kwenye mstari kila mmoja umpime anaimba Wimbo wa Taifa mpaka mwisho kuna wengine watateleza katikati, sasa hicho ndiyo kipimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wote ni mashuhuda Wilaya ya Misenyi umekuwa ni uwanja wa vita ya Uganda na Tanzania. Sisi ndiyo tulikuwa wahanga, mwingiliano wa kabila mbalimbali kutoka Uganda umekuwepo na tukaishi kama jamii moja. Sasa leo kigezo cha Wizara cha kusema kwamba imba Wimbo wa Taifa, ongea Kiswahili, watu wanaongea Kinyankole, Kihaya, tunaongea Kiganda vizuri kabisa na wao wanaongea hivyo hivyo. Kwa kweli suala la vitambulisho katika Wilaya ya Misenyi kwa kweli limekuwa ni janga la kitaifa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba wameanza kujitahidi wanapata namba, hivi kinachoshindikana ku-print kale kakadi ni nini? Tumekuwa kwenye halmashauri kule tuna- print kadi za wazee za bima za afya kuna mashine Sh.25,000, una-print vile vitambulisho unampa mtu anaendelea na maisha yake. Ile namba ukishaingiza kwenye computer kule kwako unakotaka itasoma, lakini hata kitambulisho kile ambacho unaweza ku-print kwa Sh.200, kwenye Wizara yetu imeshindikana, shida ni nini?

Mheshimiwa Spika, wananchi wetu wamepata shida sana kuhusiana na jambo hili. Cha ajabu wakati wa uchanguzi wote ni raia lakini ikija kwenye kuwatambua kama Watanzania siyo raia. Mimi wamenituma, kupitia Kiti chako watuambie kama sisi siyo raia tupelekwe kwenye nchi ambayo tunastahili twende kuishi huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini Watanzania ndiyo wanatakiwa kufaidi maziwa na asali ndani ya nchi yetu. Sasa kumwambia Mtanzania halisi kwamba hajaongea Kiswahili, Kiganda, Kihaya hicho siyo kipimo. Waende waangalie maana zile kaya zipo. Ukienda kule kwetu Bukoba sisi tunapojenga boma ni kama uwanja wote huu wa ofizi za Bunge, ni mtu ana mji wake na migomba yake imemzunguka, ukivuka hapo unaenda mji mwingine tunahesabika kirahisi, mtu yupo tangia mwaka 1920 leo uamwambia siyo raia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi nzuri wanayofanya Wizara ya Mambo ya Ndani kwenye eneo hilo bado hawajafanya vizuri. Hii inasababisha wakati mwingine majeshi yao wanaitumia kama loophole kwamba nikuite raia au siyo raia, unasemaje? Kwa hiyo, niombe sana Wizara ya Mambo ya Ndani ilichukulie kwa uzito suala hili ili wananchi waweze kuwa na raha katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)