Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshmiwa Spika, naomba kuwasilisha maelezo yangu kwa maandishi na naomba yawekwe kwenye Hansard. Naomba mchango wa jana ubadilishe na huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 9 Machi, 1967 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alichapisha falsafa ya elimu ya kujenga nchi ya kijamaa. Falsafa hii ni elimu ya kujitegemea ambayo ilitaka kuleta mapinduzi ya elimu katika nchi yetu. Mwalimu Nyerere alisema shabaha ya elimu ni kutafsiri maarifa na busara kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kinachofuata na kuwaandaa vijana kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi. Falsafa hii ilijenga kutatua changamoto za kutoa elimu yenye ubora tofauti kwa watu tofauti kulingana na kipato chao. Falsafa ya elimu ya kujitegemea ililenga kuondoa ugandamizwaji na wenye nguvu dhidi ya wanyonge na matajiri dhidi ya maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka karibu hamsini sasa tujiulize mfumo wetu wa elimu unatoa maarifa muafaka kwa vijana wetu? Mfumo wetu wa elimu unaondoa matabaka katika nchi yetu? Ni dhahiri kwamba hivi sasa tuna elimu kwa ajili ya watu maskini na elimu kwa ajili ya watu wenye uwezo. Tuna elimu kwa ajili ya sisi viongozi na walimu kwa ajili ya wapiga kura.
Mfumo wetu wa elimu unajenga matabaka ya walionacho na wasionacho na kutokana na hali hiyo Serikali sasa inaanza hata kutaka kudhibiti bei za shule binafsi ili wenye uwezo wasipandishiwe bei zikawa kubwa zaidi hasa baada ya Serikali mpya kubana mianya ya kupata mapato yasiyo halali kuwezesha kulipa ada kubwa. Kazi ya Serikali kimsingi ni kusaidia wanyonge wanaosoma kwenye mashule yenye hali mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike wakati sasa tujiulize maswali magumu kuhusu elimu. Tujiulize changamoto za elimu ya Tanzania nini? Ni suala la bajeti ndogo? Ni suala la ubora wa elimu? Kama ni kuhusu bajeti ni kwa nini uwekezaji mkubwa uliofanywa kwa miaka kumi ya Serikali ya Awamu ya Nne ambapo zaidi ya shilingi trilioni mbili zimewekwa kwenye elimu na haujaboresha elimu yetu? Kama ni kuhusu ubora ni kwa nini tumeshindwa kulitatua na kila siku tunarudia na kurudia na kurudia? Ni nini nyufa katika mfumo wetu wa elimu wa sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti ni dhahiri tumekuwa tukitoa majawabu yale yale kwa tatizo la ubora wa elimu tukitegemea matokeo tofauti. Tumekuwa tukilalamika kuhusu bajeti, bajeti iliwahi kufika 20% ya bajeti mwaka 2008 lakini hakuna kilichobadilika. Tumekuwa tukilalamika kuhusu ughali wa elimu na tukapanua udahili kwa kiwango kikubwa lakini bado shida za elimu zipo pale pale. Hata sasa tumetangaza elimu ya msingi bila malipo na tunatuma fedha yote kwenye mashule (capitation grants), udahili umeongezeka kwenye baadhi ya maeneo mpaka 140%. Lakini elimu bado haitengemai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana niliuliza rafiki zangu kwenye mtandao wa facebook kuhusu mambo gani wanayotaka kufanywa ili kuboresha elimu nchini kwetu. Nimeambatanisha maoni yao na kuwasilisha kwako ili yaingie kwenye Hansards za Bunge. Maoni ni mengi yanashabihiana na hali halisi ya elimu yetu. Kila Mtanzania analalamika na kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetunga sera mpya ya elimu inayounganisha elimu ya sasa ya msingi na sekondari na kuitwa elimu msingi. Tumeweka miaka kumi ya watoto kusoma elimu msingi. Muono wa sera ni kana kwamba changamoto zetu ni miaka ambayo watoto wanakaa shule. Mwandishi mmoja kuhusu elimu kaandika kitabu cha Rebirth of Education: Schooling isn‟t learning. Mwandishi huyu anaitwa Lant Pritchett. Naomba watu wote wanaopenda elimu nchini na wanotaka kuleta mapinduzi kwenye elimu wasome kitabu hiki. Kimsingi Pritchett anasema kukaa darasani sio kupata elimu, kwenye nchi nyingi zinazoendelea ikiwemo Tanzania tumewekeza kwenye kufikia malengo ya idadi ya watoto wanaoandikishwa badala ya kuwekeza kwenye kutoa maarifa kwa watoto. Ndiyo maana hapa nchini kwetu takribani vijana 60% wanaofanya mtihani wa kidato cha nne hufeli kwa kupata sifuri na kwenye baadhi ya mikoa kama Kigoma 86% hupata sifuri na daraja la nne. Watoto wanakwenda shuleni lakini hawajifunzi, hawapati elimu. Sera ya elimu lazima itoe fursa ya kuzalisha watoto wanaopata elimu na sio kukaa darasani tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa karibuni kabisa unaonyesha ni 40% pekee ya watoto wa darasa la nne wanaoweza kufanya hesabu hii, sita gawanya kwa tatu (6/3) au kuzidisha saba mara nane. Matokeo ya miaka na miaka ya uwezo yanaonyesha hali hiyo pia. Kwa mfano karibu 50% ya watoto wanaomaliza darasa la saba hawawezi kufanya mahesabu au kusoma hadithi ya darasa la tatu. Kwa nini watoto wetu hawajifunzi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, visababishi vya hali hii ni vingi sana, lakini kikubwa kuliko vyote ni mwalimu. Matatizo kuhusu mwalimu Tanzania ni lundo lakini tunaweza kuongelea mawili kwa leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa walimu katika miaka ya karibuni nchi yetu imepiga hatua katika kusomesha na kusambaza walimu. Lakini walimu wengi waliopo mashuleni hawafundishi. Utafiti wa karibuni kabisa unaonyesha kuwa ukifanya ziara ya kushtukiza mashuleni ni 47% ya walimu waliopo shuleni ndiyo waliopo darasani kufundisha vipindi walivyopangiwa.
Aidha, walimu wanafunzi nusu tu ya muda wanaopaswa kufundisha. Matokeo yake ni kwamba asilimia 50 ya muda wa watoto shuleni unapotea bila kusoma. Kiuchumi maana yake ni kwamba tunapoteza asilimia 50 ya uwekezaji katika elimu ukizingatia kwamba pesa nyingi katika elimu zinaenda katika mishahara ya walimu. Utafiti ambao umetolewa leo uitwao Tanzania Service Delivery Indicators unathibitisha kuwa 49% tu ya walimu wanaingia darasani na kufundisha zaidi ya nusu hawapo shuleni kabisa au hawafundishi. Utafiti huu umehoji walimu 3,692 na wanafunzi 4,041 na umefanywa na REPOA na Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii inasababishwa kwa kiasi kikubwa na motisha na usimamizi hafifu kwa walimu. Hivyo ni muhimu kufanya bidii kama nchi kutoa motisha kwa walimu lakini ni muhimu pia walimu wasimamiwe na wapewe mafunzo kazini ya mara kwa mara. Kwa sasa ni asilimia tano tu walimu wanakuambia wamewahi kuhudhuria mafunzo yoyote kazini katika miaka mitano iliyopita. Ndiyo maana tumekuwa tukidai kwa miaka mingi sana chombo cha kitaaluma cha walimu (Teachers‟ professional board) lakini Serikali imegoma kunyang‟anywa udhibiti wa walimu. Tuwekeze kwa mwalimu kama ninavyoshauri hapa chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya juu hapo ni balaa kabisa, ubora wa vyuo vikuu umeanza kutia shaka. Katika utafiti wa juzi juzi wa Times Higher Education hakuna chuo hata kimoja cha Tanzania kilichopo katika orodha ya vyuo bora 30 Afrika. Tupo nyuma ya Makerere na Nairobi ambavyo tulikuwa tunavizidi, hatufanyi uwekezaji katika tafiti. Nchi ilishaamua kuwekeza asilimia moja ya Pato la Taifa katika utafiti lakini hadi sasa Serikali imetoa 0.001%. Vitabu vya bajeti vinaonyesha kuwa bajeti kubwa ya elimu inakwenda elimu ya juu lakini kwenye mikopo. Uwekezaji kwenye utafiti haufanyiki na tutaathirika sana kama Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini falsafa ya Rais Magufuli katika elimu? Rais anasema Tanzania ya Magufuli ni Tanzania ya viwanda, viwanda kwenye nchi ya wajinga? Nani anafanya kazi kwenye viwanda hivyo? Nani atasimamia mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii na hata ya kisiasa yatakayoletwa na uchumi wa viwanda? Tunaposema tunataka nchi ya uchumi wa kati tunajua mahitaji ya elimu ya uchumi wa kati? Tunaelekeza rasilimali fedha katika kujenga rasilimali watu itakayoendesha uchumi wa viwanda? Tunaposema uchumi wa viwanda tunawasemea watoto wetu hatujisemei sisi, tunasemea kizazi kijacho. Tunakiandaa kwa Tanzania hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mahusiana chanya kati ya elimu na ukuaji wa uchumi, vilevile kuna mahusiano chanya katikati ya ubora wa rasilimali watu (elimu na afya) na ukuaji wa uchumi. Tafiti zinaonyesha kuwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zinaweza kwenda kwa kasi kiuchumi iwapo zitawekeza kwenye elimu na afya. Robo ya kasi ya ukuaji uchumi inaweza kuchangiwa ubora wa rasilimali watu pekee.
Hivyo tunapotaka kujenga uchumi wa viwanda na ili uchumi huo uwe na maana ni lazima kuwekeza vya kutosha kwenye elimu. Hata hivyo, ni lazima tuwekeze tukiwa na ushahidi wa kisanyansi kuhusu nyufa za elimu ya Tanzania (evidence based policy interventions).
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ndogo ya elimu ya ufundi peke yake inahitaji Watanzania wenye ujuzi wa juu milioni tatu ifikapo mwaka 2025. Pia Tanzania inahitaji watu wenye ujuzi wa ufundi (kutoka VETA na Technical Schools) wapato milioni saba ifikapo mwaka 2025.
Ni muhimu sana kufungua macho na kufanya maamuzi mahususi kuhusu elimu. Tunahitaji uwekezaji wa angalau 20% ya bajeti yetu kwenda kwenye elimu kwa miaka kumi ijayo ili kuweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye elimu. Hata hivyo, kipimo cha msingi cha mafanikio katika mfumo wa elimu ni kama watoto wanaotoka kwenye mfumo huo wa elimu wana maarifa, ujuzi na uwezo wa ulimwengu watakaoukabili. Hatuwezi kupata mafanikio haya bila kufumua mfumo wetu wa elimu, kupanua demokrasia ya utoaji elimu na kuhakikisha walimu wanapata motisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya motisha tunayoweza kuwapa walimu ni kuwalipa vizuri, kuwasimamia vizuri na kuwapa mitihani maalum kila wakati ili kuwapandisha madaraja.
Napendekeza salary scale ya walimu iwe sawa na angalau nusu ya salary scale ya Wabunge na viwango vya mishahara kati ya walimu wanaofundisha ngazi yoyote ile iwe sawa kulingana na usawa wa elimu, muda kazini na juhudi (performance based remunerations). Najua haya yaweza kuonekana magumu lakini naamini maneno aliyoyasema mwanaharakati wa elimu nchini Rakesh Rajani aliyepata kusema more of the same won‟t cut I anymore. Kama elimu ndio silaha kubwa ya kuleta maendeleo, ni lazima tufanye tofauti ili kuboresha elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kamati ya Bunge ya Huduma Maendeleo ya Jamii kwamba Taifa liunde Tume ya Wataalam ili kuweza kutafuta nyufa za elimu yetu na kutoa mapendekezo yanayotokana ushahidi wa kisayansi. Tuunde Tume ya Elimu sasa ili tuweze kuwa na muda wa kutosha wa kutatua changamoto za elimu nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika pendekezo la kuanzisha vyuo vya ufundi kila mkoa natoa maombi maalum kwa mkoa wa Kigoma kuanzisha Taasisi ya Teknolojia ya Ujiji (Ujiji Institute of Technology – UIT). Mji wa Ujiji ni moja ya miji mikongwe nchini ambayo inasinyaa kama sio kufa. Uanzishaji wa chuo utakaoweza kudahili angalau wanafunzi 5,000 itakuwa ni chachu kubwa ya maendeleo mji huu na Tanzania kwa ujumla. Taasisi ya Teknolojia ya Ujiji itaweza kusaidia sana kuziba mianya ya wataalam wa katika kwenye sekta ya usafirishaji (logistics) kwa kuzingatia kuwa Kigoma ni lango la Magharibi la Taifa letu. Napendekeza kuwa Serikali ilitazame kwa kina ombi hili ili kuweza kuongeza wataalam wa kati katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapendekeza pia Serikali itazame upya suala la sera ya vitabu ili kuhakikisha kuwa uwekezaji katika uchapishaji unaongezeka nchini. Nadhani ni wajibu wa Serikali kuhakikisha ubora wa vitabu badala ya yenyewe kuhangaika na kuandika na kuchapisha vitabu. Sera ya vitabu inazalisha ajira kwenye nchi na inawezesha Watanzania kutafuta fursa kwenye maeneo hayo pia. Wachapishaji wa ndani wanashindwa kukua kwa sababu Serikali imewabana. Serikali haipaswi kubana, inapaswa kuchochea ukuaji wa sekta ya uchapishaji.
Vilevile napendekeza sana tuwekeze kwenye maktaba za kijamii kwenye kata zetu na miji yetu. Maktaba hizi ziwe na vitabu na tuhamasishe watu wenye vitabu kutoa vitabu kwa maktaba hizi. Tujenge Taifa la wasomaji kwa kuhamasisha usomaji kuanzisha ngazi za chini kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasisitiza kuwa mapendekezo ya Kamati ya Bunge kuhusu namna ya kutoa mikopo na kuikusanya yachukuliwe kwa uzito unaostahili. Mikopo isiwe sehemu ya bajeti ya Wizara badala yake Bodi ipewe fedha moja kwa moja kutoka hazina (direct transfer) na mfumo wa malipo udhibitiwe. Ni lazima tufanye tafiti kuhakikisha kuwa ifikie wakati Bodi ya Mikopo iweze kujiendesha yenyewe kutokana na fedha zinazorejeshwa. Mfumo wa kutumia credit reference bureau na vitambulisho vya Taifa na hata mobile technology kuhakikisha mikopo inarejeshwa ni mfumo ambao utakuwa na mafanikio makubwa sana. Serikali ifanyie kazi pendekezo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasisitiza pia kuwa pendekezo la Kamati kuanzisha President Magufuli Scholarship Award lianze mara moja. Tuchukue watoto waliofanya vizuri angalau 50 kila mwaka na kuwasambaza kwenye vyuo vikuu vikubwa duniani. Ndani ya miaka kumi tutakuwa tumetengeneza mamia ya Watanzania wenye uwezo mkubwa kwenye nyanja zote nchini. Rais atakuwa ameacha jambo kubwa na la kukumbukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.