Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kupata dakika tano za kuchangia Mpango wetu wa Maendeleo Awamu ya Tatu. Ukiusoma ule mpango na hotuba ya Mheshimiwa Waziri utaona wazi kwamba umejikita katika shabaha nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza unasema, kuhakikisha kuwa uchumi wetu unakua kati ya asilimia 6 na asilimia 8. Pili, kuhakikisha kuwa mapato ya Halmashauri zetu yanatoka asilimia 15 mpaka 16.8 ya pato la Taifa. Tatu, ni kulinda mfumuko wa bei (inflation) tubaki katika single digit ya asilimia 3 mpaka asilimia 5. Nne, kuendelea ku-maintain hifadhi ya fedha za kigeni walau kwa miezi minne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Kilombero kazi yangu kubwa ni kuwakilisha mawazo na maoni yao kuhusu Mpango huu. Mathalani, ili kufikia shabaha hii ambayo imeandikwa hapa na Mheshimiwa Waziri katika Mpango wetu wa Halmashauri kujitegemea kwa hadi asilimia 16.8, kama walivyosema Wabunge wenzangu wengine waliotangulia, ni wazi kwamba tukijikita katika kilimo tunaweza kufanikisha jambo hili. Kwa mfano kwenye zao la miwa ya sukari, Mheshimiwa Rais alishaelekeza kwamba nchi yetu ijitegemee kwa sukari na wakulima wetu wamewekeza katika zao hili. Hata hivyo, taarifa za Wizara katika Mpango zinasema tunatupa miwa tani milioni moja kwa mwaka. Uwekezaji wa miwa peke yake katika Jimbo la Kilombero utakuza mapato ya Halmashauri kwa two percent na hapo tayari tutakuwa tumefikia shabaha ya pili ya Mpango wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni miradi mkakati katika Mpango wetu wa Maendeleo. Mathalani, Serikali imesema itaendelea kuwezesha miradi mkakati ili kuziwezesha tena Halmashauri. Jimbo langu la Kilombera na wananchi wetu, tayari wana andiko kuhusu soko na namna gani soko na stendi zitakavyokuza mapato ya Halmashauri kufikia shabaha ya Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nne ni kilimo kwa maana ya mpunga. Amezungumza mchangiaji wa kwanza, Mheshimiwa Prof. Muhongo hapa kwamba tuwekeza katika kilimo ili tuweze kuendelea. Amesema pia watu duniani ni karibu bilioni saba na nusu ya watu duniani wanatumia mpunga. Jimbo la Kilombero linazalisha mpunga kwa zaidi ya asilimia 70. Katika Mpango huu endapo tutawekeza katika kilimo cha mpunga kwa kiwango kubwa, tunaweza kufikia shabaha ya Mpango huu ambao ni kukuza mapato ya Halmashauri kutoka asilimia 15 mpaka asilimia 16.8. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengine ni mambo ya miundombinu. Mheshimiwa Waziri kama ulivyozungumza, mara kadhaa tumesema katika kilimo ambacho tunataka kukikuza ili tuweze kufikia maendeleo ya ukuaji wa uchumi kwa asilimia 6 -8 lazima tuwe na miundombinu ya kutosha ya kusafirisha mazao ya wananchi na wakulima wetu vijijini. Ndiyo maana mara nyingi tukisimama hapa tunazungumzia habari ya barabara ambazo zimekuwa historia kwa muda mrefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri tukajikita pia katika kuboresha miundombinu yetu. Mathalani katika Jimbo la Kilombero, tuna barabara hii tunaizungumzia mara zote ya Ifakara – Kidatu ambayo itaunganisha Wilaya za Ulanga, Malinyi, Mlimba, Kilombero, Mikumi na Mkoa wa Morogoro. Hatimaye itawawezesha wakulima wetu kuuza bidhaa zao vizuri na kuchangia katika pato letu la Taifa na kuchangia katika Mpango wetu wa maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni fursa mbalimbali ambazo zinatokea katika kilimo kwa kuwakumbuka wananchi hawa. Matahlani, alizungumza mama yangu mmoja Mbunge wa Morogoro hapa kwamba zamani kulikuwa na huduma za matrekta katika vijiji vyetu. Katika Mpango huu wa Maendeleo ambao tumesema asilimia karibu 80 ya wananchi ni wakulima, endapo tutarejesha matrekta katika vijiji vyetu tunaweza kufikia malengo yetu na hasa kwa Mkoa wa Morogoro ambao mimi ni Mbunge katika moja ya majimbo yake na umechaguliwa kuwa ghala la taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, endapo mpango wa maendeleo utakumbuka hii mikoa ambayo ni ghala la taifa, automatically tutakuza kilimo na tutapata maendeleo ya haraka na kufikia shabaha ya Mpango ya uchumi kukua kwa asilimia 6 mpaka 8, mapato ya Halmashauri kutoka asilimia 15 mpaka 16.8 kwa pato la Taifa, tutalinda mfumuko wa bei na tunaweza kuuza mazao yetu nje kupata fedha za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nawasilisha na naunga mkono hoja. (Makofi)