Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii ya kuchangia Mpango huu. Nianze kwanza kuipongeza Serikali yetu chini ya Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya kutuletea Mpango huu mzuri. Naipongeza pia Wizara kwa kazi nzuri ambayo wamefanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja nilikuwa nasoma journal moja ambayo imeandikwa na Royal Irish Academy ikizungumzia juu ya vyama vikongwe kubakia madarakani. Walifanya uchambuzi mzuri sana, walipofika kwenye CCM wakaeleza kwamba CCM ipo madarakani na ina uwezo wa kuendelea kuwa madarakani kwa sababu baada ya uchaguzi huwa wana-stick kwenye kutekeleza Ilani, hawafanyi manipulations na kufanya mambo mengine mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa nasoma Mpango huu, kikubwa nilichokuwa najaribu kukitazama ni hicho kwamba umeendana vipi na ilani yetu? Mimi nimeridhika kabisa kwamba Mpango ulioletwa uko sambamba na Ilani na kwa hiyo, kama ilivyo kawaida kwamba kwenye Mfumo wa Vyama Vingi, chama kinachoshinda kwenye uchaguzi Ilani yake inageuka kuwa sera, basi tuungane kwa pamoja tutekeleze Mpango huu, tuutungie sheria, bajeti ikija tupitishe mafungu tukatekeleze kwa pamoja na kwa umoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri tu mambo machache. Suala la kwanza ni elimu. Endapo kweli tutataka kama ambavyo tunataka kwamba vijana wetu washiriki katika uchumi wa viwanda na waweze kufaidi matunda ya nchi kufikia katika uchumi wa kati, basi suala la VETA ni lazima tulitilie mkazo sana kama ambavyo imezungumzwa kwenye Mpango. Vipo Vyuo vya VETA ambavyo vilianzishwa na wananchi kwa kushirikiana na marafiki na wafadhili mbalimbali; kwenye Jimbo langu viko viwili; kuna kimoja kiko Tarafa ya Usangi na kingine kiko Tarafa ya Ugweno, ni muhimu hivi vikafufuliwa viweze kufanya kazi kwa sababu huduma yake bado inahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunahitaji Vyuo vya VETA katika kila wilaya ambavyo vitaendena na uchumi wa eneo husika. Kwa mfano, Kanda ya Kaskazini tuko kwenye utalii na madini; basi Vyuo vyetu vya VETA viendane na kutengeneza vijana watakaoshiriki kwenye uchumi huo. Halikadhalika, Kanda ya Ziwa kama kuna uvuvi na madini, basi twende hivyo hivyo ili tuhakikishe kweli vyuo vyetu vinawafaidisha vijana wa maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunahitaji kuendelea kutilia mkazo elimu ya juu. Dhana kwamba kwa sasa hivi elimu ya juu imeanza kuwa irrelevant, hiyo mimi sikubaliani nayo kabisa, kwa sababu mbili. Kwanza, huwezi kupigana vita ukawa na Askari wa chini peke yao bila Majenerali. Halikadhalika, liko suala kwamba dunia imekuwa kijiji, tunahitaji ku-export hata grains. Kama tunavyopeleka wachezaji akina Mbwana Samatta wakacheze nje huko, pia tunahitaji wasomi wetu waende wakafanye kazi za kibingwa huko nje. Wako wengi mpaka sasa hivi ambao wanafanya kazi hiyo, hata waliotoka kwenye Jimbo langu, lakini tunahitaji succession plan kwamba hawa wanapostaafu, wapatikane wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, kwa hiyo, tutilie mkazo pia elimu ya juu, kwenye Jimbo langu tuna ardhi kubwa sana, kwa hiyo, ninaalika kabisa Serikali ije kuwekeza hata kwenye vyuo vikuu. Tuna ardhi ya kutosha, tufanye kazi hiyo, pamoja na Vyuo vya VETA lakini pia tuendelee kutengeneza akili kubwa kwa ajili ya kuingia kwenye Soko la Dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotakiwa ni kwamba wataalam wetu wa elimu watutengenezee mitaala ambayo itawafanya wahitimu wasiabudu vyeti. Kuna nchi jirani tu hapa, kuna kijana ame-graduate International Relations and Diplomacy lakini akaenda kuanzisha car wash. Sasa yeye kwa sababu amefikia level hiyo, anaenda kwa Mabalozi na Mashirika ya Kimataifa, anasaini mikataba ya kuwaoshea magari, analipwa dola. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kijana mwingine atakuja akuambie naomba mtaji wa kuanzisha car wash shilingi milioni tano, sijui nitanunua hoover na hiki na hiki; akishaanzisha car wash anakaa hapo anasubiri wateja wamfuate, yeye anaongea habari ya Arsenal na nini akisubiri wateja waje, badala ya kwenda kuwagongea mlango. Bora hata angezungumza Simba na Yanga maana ni za kwetu. Kwa upande wa elimu napenda nisema hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kilimo, naungana na wote ambao wamesema kabisa kwamba kilimo ni moja ya vitu ambavyo vitatutoa kiuchumi, lakini lazima twende kwenye kilimo cha umwagiliaji. Nchi yetu ina vyanzo vingi sana vya umwagiliaji kiasi ambacho hata suala la greenhouse linaweza likaja kama second option.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa sababu kengele imelia, ipo miradi kwa mfano kwenye Jimbo langu, naishukuru Serikali kwamba…

(Hapa kengele ya pili ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)