Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Muharami Shabani Mkenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. MUHARAMY S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwako kwa kupata nafasi hii. Napenda pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema hadi kufikia siku ya leo. Napenda pia niwashukuru wananchi wenzangu wa Jimbo la Bagamoyo kwa kunipa heshima kubwa ya kuwa hapa leo. Pia napenda niishukuru familia yangu, ndugu zangu na jamaa zangu kwa kuni-support hadi nimefikia hatua hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja katika Mpango. Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango amewasilisha Mpango wake; kwa kweli kabisa ni mpango mmoja ambao ni mzuri sana, kama jina lake lilivyo Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niguse katika suala zima la kilimo. Katika mpango nataka nijikite zaidi katika kilimo cha umwagiliaji. Serikali katika hotuba yake ya Mpango imezungumza kwamba hekta za umwagiliaji ziko 461,378 na ina mpango wa kuongeza hekta hizo hadi kufikia 694,715.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze; pale kwetu Bagamoyo tuna kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Mto Ruvu. Kilimo hiki kinawasaidia watu wengi sana. Si Mto Ruvu pekee, tuna Mto Wami ambao una nafasi kubwa sana katika kuisaidia nchi katika kilimo hiki cha umwagiliaji, kwa sababu mwaka 1966 mwezi Oktoba kulifanyika study na kampuni moja ya watu wa Sweden ambayo ilikuwa inafanya kazi ya kufanya utafiti wa mradi wa umeme pamoja na bwawa kubwa sana la umwagiliaji katika Mto Wami ambalo lilitakiwa liwe pale Mandera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali, bwawa hili likitumika katika kilimo cha umwagiliaji maeneo mengi sana ya Bagamoyo pamoja na Mkoa wa Pwani, Kibaha, yanaweza yakapata maji mengi sana kupitia mradi huu kwa sababu ni bwawa ambalo limefanyiwa study na makaratasi yake yapo, nafikiri hata Wizara inalitambua hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nirudi katika suala la wavuvi. Bagamoyo kwetu sisi tunashughulika na uvuvi na kwa bahati nzuri Serikali mwaka huu kupitia jemedari wake, Rais Dkt. John Pombe Magufuli, wameamua kununua meli nane za uvuvi. Nina imani katika meli hizo Bagamoyo inaweza ikapatiwa meli moja; sina shaka na hilo kwa sababu Chuo cha Uvuvi Mbegani ambacho kina wataalam wengi sana wanaojua masuala ya uvuvi tuko nacho pale. Niwashauri ndugu zangu, suala hili la uvuvi tukilishikilia linaweza likatuingizia pesa nyingi sana katika nchi yetu. Kwa sababu mwaka 2015/2016 mauzo yalikuwa dola bilioni 379, mwaka 2019/2020, mauzo yanaonesha yalikuwa dola bilioni 506,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri; pale Bagamoyo pana mradi mmoja wa kufuga jongoo bahari. Hawa jongoo bahari bei yake ni kubwa sana duniani. Hata Waheshimiwa Wabunge mki-google katika hizo tablets zenu sea cucumber, world price market ni shilingi ngapi, mtaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Mheshimiwa Naibu Waziri alitembelea pale tulikwenda sehemu ambako wanafugia yale madude. Kilo moja ya jongoo bahari ni Sh.65,000. Sasa tukielekeza katika miradi kama hii Serikali inaweza ikatupatia pesa nyingi sana na kuhakikisha mipango yetu ya maendeleo itakuwa sawa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana, muda umekwisha Mheshimiwa.

MHE. MUHARAMY S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mengi, lakini naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)