Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kusimama tena ndani ya Bunge hili Tukufu kutoa mchango wangu ndani kwa Taifa langu. Naomba tu niishukuru sana familia yangu, wapiga kura wangu kwa kazi kubwa waliyoifanya kunileta hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa matumaini. Najua nasikilizwa hap ana watu hapa ndani, lakini najua nasikilizwa na Watanzania sehemu mbalimbali ya nchi yetu. Naomba tu niseme hivi, nina matumaini makubwa kwa nchi yangu leo kuliko ilivyokuwa jana. My hope for this country is greater today than it was yesterday. Nataka niwaambie Watanzania wanaonisikiliza kwamba tunakokwenda ni kuzuri sana.

Sasa nina bahati ya kuwa hapa ndani leo, tangu nimeingia nasikiliza watu wanaongea, nasikiliza napata muda wa kujifunza. Namshukuru Mungu niko hapa ndani nashiriki, zamani nilikuwa nawaangalia mnaongea nikiwa nje. Najifunza kitu kimoja kikubwa sana. Ukiwa hapa ndani kuna wakati uweke fence kwenye akili yako, ujiwekee fence, useme hiki hakiwezi kuingia kwenye kichwa changu, hiki kinaweza kikaingia maana kuna mtu anaongea kitu halafu najiuliza hivi huyu hajui yanayoendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii inakua, tena inakua kwa kasi! Nani hajui tulipotoka? Nani hajui?

T A A R I F A

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe Taarifa Mheshimiwa Mbunge Eric Shigongo anayeongea kwamba katika Bunge hili sisi tuko kwa niaba ya wananchi tunatoa mawazo yetu na ya wananchi, kwa hiyo pana uhuru wa mawazo yote tunayoongea ni sahihi mahali hapa. Mwisho wa siku tunakuja na kitu kimoja. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shigongo hajamtaja mtu, endelea tu.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa hiyo sijaipokea kwa sababu sijamtaja mtu yeyote. Nataka niwaeleze Watanzania na niwaeleze watu wote walioko hapa ndani kwamba mnapoamua kujenga uchumi kuna transition period. Kuna kipindi cha mpito lazima mpite. Hata ukisoma historia ya China wakati wa Mao Tse Tung kulikuwa na kipindi kigumu sana walikipitia wale watu hatimae wakafika walipo leo. Yawezekana tunapita lakini tumeshaanza kupita kwenye transition hivi sasa mambo yanaenda kuwa safi. Nataka kuwaambia Watanzania wanaonisikiliza kwamba ya kwamba wawe na matumaini, wawe na imani na kiongozi wetu mkuu, wawe na Imani na Bunge hili ya kwamba tunakokwenda ni kuzuri na kazi inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nichangie Mpango wa Mwaka mmoja na wa Miaka Mitano. Nasema hivi; nitachangia eneo la digital economy, uchumi wa kidijitali. Eneo la viwanda na nikipata nafasi nitachangia eneo la mitaala yetu ya elimu kwa ajili ya watoto wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia nizungumze mambo matatu tu ya muhimu kwamba we are a blessed country. Tanzania kama Tanzania ni nchi iliyobarikiwa sana. Kuna mtu alisema kwamba Mungu wakati anaumba dunia inawezekana siku ya saba alikuwa yuko Tanzania, maliasili zote aliziacha hapa wakati anakung’uta kung’uta mavazi yake ili arejee alikung’uta kila kitu akaacha hapa. Kaacha gesi, makaa ya mawe, almasi, dhahabu na kadhalika. Wakati anaondoka wanasema akadondosha handkerchief yake pale Arusha kadondosha Tanzanite pale haipo sehemu nyingine duniani. This is a blessed country, tukusanyikeni hapa tuzungumze namna ya kutumia utajiri wetu kupeleka Taifa letu mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka kulizungumzia ni uchumi wa kati. Hatujafika kwenye uchumi wa kati accidentally, hatujafika kwa bahati mbaya. Kuna mambo tuliyafanya yametufikisha hapo. Mambo hayo tuliyoyafanya tunayajua, basi tukayafanye mara mbili zaidi tulivyokuwa tukifanya zamani. Tutapanda kutoka uchumi wa kati wa chini kwenda uchumi wa kati wa juu, hili linawezekana. Hilo ni jambo la pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu linahusu kufanya kazi kwa juhudi kubwa. Haukuwepo Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza hapa nikawakumbusha Wabunge juu ya checklist manifesto, kuandaa mpango kama huu uliokuja halafu mnakuwa mna-tick kimoja kimoja mnachokifanya baadaye kwenye siku ya pili au mwaka wa pili mnahama na yale ambayo hamkuyatimiza huko nyuma. Lazima tuwe na checklist manifesto ya namna ya kutekeleza mambo yote tunayoyapanga kwenye mpango huu na tuanze moja baada ya lingine na tupange vipaumbele vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Afrika huwa inateseka na tatizo kubwa sana la kupanga priorities. Sisi tukatae, sisi tuwe watu tunapanga priorities zetu sawasawa, tunaanzia hapa kwa sababu ni muhimu, tunakuja hapa, tunakwenda hapa, tunakwenda pale. Watu tufanye kazi, Rais wetu anafanya kazi sana. Tuna Rais mchapa kazi, Rais visionary, lazima tumuunge mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais huyu hana maneno mengi na hazungumzi sana. Mfano, juzi alikuwa Mwanza akasema huko Dar-Es-Salaam nikija nikute shule imejengwa; imejengwa haijajengwa?

WABUNGE FULANI: Imejengwa.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo ndiye Rais tuliye naye tufananye nae Watanzania wote tufanye kazi kwa nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napenda kusoma vitabu. Kaka yangu Waziri wa Sheria aliwahi kuniambia msemo mmoja niurudie hapa, akasema ili ufanikiwe lazima uwe na kitu kinaitwa Bibliophilia, yaani usome sana vitabu. Sijasoma sana lakini napenda kusoma sana vitabu. Nimesoma kitabu cha Jack Welch, Jack Welch is a number one general manager in the history of the world. Huyu ndio aliyeitoa General Electric kwenye kufilisika mpaka kuwa number one company in America.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jack Welch alisema ili uongoze watu lazima ufanye mambo mawili. La kwanza uwaongoze kwa compassion, kwa kuwasukuma au uwaongoze kwa persuasion, kwa kuwasihi na kuwabembeleza wafanye kazi. Hapa Tanzania na Afrika Jack Walsh angekuja kufanya kazi hapa angefilisika. Kwa sababu hapa Tanzania ukitaka kuwapeleka watu kwa kuwabembeleza kazi haziendi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina kampuni binafsi; nilijaribu persuasion ikanishinda nikaamua kutumia compassion kwamba anayetaka kusukumwa anasukumwa anafanya kazi anayetaka kubembelezwa anabembelezwa anafanya kazi. Hapa Afrika mambo yote mawili yafanye kazi. Rais wetu anataka kazi. Ukipewa jukumu lifanye kwa nguvu zote ndiyo tunaweza kutoka hapa tulipo kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye digital economy. China wamegundua kwamba, manufacturing imeanza ku-decline, imeanza kushuka, ndiyo maana wakaamua sasa tuwekeze kwenye digital economy, uchumi wa kidigitali, ndio maana wanakimbia kwenye mambo ya 5G tunayaona. Sasa hivi duniani hapa China inaongoza katika mambo ya digital, kwa nini alifanya hivyo? Wanataka ku-cover lile gap ambalo litatokea manufacturing itakapo- fail.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hakuna ubaya kwa sisi kujikita kwenye kutengeneza viwanda, ni sawa kabisa, lakini hebu tuelekezeni na akili yetu upande wa pili kwenye digital economy. Kwa nini tunaacha nchi jirani hapa zinajivuna kama zenyewe ndiyo Silicon Valley ya East Africa? Tuna vijana wana akili hapa Tanzania sijawahi kuona. Wanagundua vitu vingi, lakini hawana mtaji hawa watoto, wanatoka UDOM hapo; wamejifunza mambo makubwa kabisa ya kuleta solution kwa changamoto tulizonazo lakini hawana capital na hawawezi wakaenda benki leo na idea akapewa mkopo, haiwezekani, benki zetu sio rafiki wa masikini. Sasa kama tunaweza kukopesha fedha kwa kijiji milioni 50, kama tunaweza kupeleka pesa kwenye halmashauri kuna shida gani hawa vijana wetu wakapewa guarantee ndogo tu kwa benki kwamba, you have the best idea, sisi tutaku-sponsor wewe utengeneze application yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ni-declare interest, mimi nina run media company. Pale kwetu tuna online radio, tulihangaika sana tulipopata kazi ya kuweka redio kwenye mabasi ya mwendokasi pale Dar-Es-Salaam, tulikosa technology. Tukapata South African partner halafu akajitoa, tukabaki tumekwama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini huwezi ukaamini waliotupa solution hiyo ni vijana wamemaliza UDOM hapa? Vijana wale wametengeneza king’amuzi cha kwao ambacho kinanasa matangazo kutoka ofisini kwetu mpaka kwenye mabasi yote ya mwendokasi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Watanzania let us trust our children, tuwaamini na tuwawezeshe watoto wetu.

MWENYEKITI: Ahsante sana ni kengele ya pili.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekit, ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)