Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia fursa ya kuanzisha mjadala huu. Nianze kwa kushukuru Wizara kwa kufanya kazi nzuri. Vilevile nimshukuru Rais na timu ya Serikali kwa mipango mizuri waliyotuletea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mpango wa Mwaka Mmoja ni sehemu ya Mpango wa Miaka Mitano. Kwa upande wangu niseme kwamba naunga mkono, miradi yote itatekelezwa na hasa ya Jimbo la Musoma Vijijini, ikiwemo na barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyosema na tunavyopaswa kufanya ni kutoa mapendekezo. Kwa hiyo, nianze kwa kusema hivi; kwenye mambo ya uchumi na maendeleo, ukitaka kupunguza umaskini popote duniani, ni lazima uchumi ukue siyo chini ya asilimia 8. Ndiyo maana Ilani yetu ya CCM wale waandishi walikuwa ni wataalam wazuri, tumecheza na asilimia 6 mpaka 7 kwa muda, tumekwenda mbele, lakini wataalam wanasema usiwe chini ya asilimia 8. Ukitaka kwenda kama China ilivyofanya toka miaka ya themanini mpaka leo hii, ni lazima uchumi wako ukue kwa zaidi ya asilimia 10 na siyo chini ya miaka kumi, ishirini, ndiyo unaweza kuwa nchi yenye kipato kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mchango wangu mimi ni namna gani sisi Tanzania tutafanya tuendelee kuwa nchi ya kipato cha kati. Waheshimiwa Wabunge, kipato cha kati kuna madaraja mule; kuna lower middle income, ndimo sisi tumo. Daraja hili maana yake unakuwa na pato ambalo ni kati ya dola 1,026 mpaka dola 4,035. Ndiyo maana Mpango wa Pili ulikuwa unasema Tanzania twende kwenye GDP per capita ya Dola 3,000, tulitegemea hivyo kama miaka ya nyuma huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi tumeingia tukiwa na Dola 1,122 na sasa hivi tuko watu milioni 60. Tukifika mwaka 2025 tutakuwa watu takriban milioni 70. Sasa tuchukue kwamba pato letu kwa mmoja mmoja, GDP per capita iwe ni Dola 1,200. Maana yake tatizo la kubaki kwenye 1,100, uchumi ukitetereka kidogo tu, unaanguka chini, unarudi kuwa kwenye nchi ya kipato cha chini. Ndiyo tatizo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi Waheshimiwa Wabunge, tunapaswa kuishauri Serikali tuzidi kwenda mbele. Kwa hiyo, tukiwa na pato la 1,200 kwa watu milioni 70, tunapaswa kuwa na GDP ya Dola za Kimarekani bilioni 68, sasa hivi tuko 50. Tukisema tunasogea kidogo ili tubaki pale katikati, twende kwenye GDP per capita ya 1,500, ukizidisha kwa 70 tunapaswa Serikali yetu na sisi wote tuwe na GDP ambayo iko kwenye Dola za Marekani bilioni 105. Angalia hiyo safari, kutoka GDP ya Dola bilioni 50 kwenda 84, kwenda 104, siyo kazi nyepesi, lakini tunaweza kwenda huko. Kwa hiyo, mapendekezo yangu ni tuone tufanyaje ili tuwe na uchumi unaokua kwa zaidi ya 8%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine cha kuweka maanani ni kwamba daima; na nashukuru ripoti imeweka maanani kwamba sisi ni sehemu ya hii dunia na kwamba tutauza bidhaa zetu kwenye Soko la Dunia. Hiyo ni muhimu sana. Kwenye mambo kama haya ni lazima ujilinganishe na mwenzako. Nami nimechukua nchi mbili tu za kujilinganisha nazo. Nimechukua ya kwanza Kenya ambao ni jirani zetu. Wenyewe GDP per capita yao sasa hivi ni Dola 2,075. Kwa hiyo hata wao wakiyumba hawawezi kushuka mpaka Dola 1,025. Mwaka 2025 GDP ya Kenya itakuwa Dola 2,593. Lazima tushindane nao, wao wamefanyaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine niliouchukua ni Seychelles. Nimechukua Seychelles kwa sababu wanaojua historia ya nchi yetu miaka ya 1980, bila Serikali yetu au wanajeshi wetu kwenda Seychelles, hali ilikuwa mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, GDP ya Seychelles, kwa kifupi, ndiyo ya kwanza kwa Bara zima la Afrika, lakini tuliwasaidia, tuliwapigania, wametuzidi. GDP per capita yao sasa hivi ni Dola 12,233. Mwaka 2025 GDP per capita yao itakuwa Dola 18,812. Ni kwamba Seychelles itakuwa ni nchi tajiri, itakuwa kwenye higher income. Higher income ni lazima uvuke GDP per capita iende zaidi ya Dola 18,000.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Profesa Muhogo, wale hatuwawezi kwa sababu population yao hata 300,000 hawafiki.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, GDP per capita ni suala la hesabu. Ni kama machungwa, ni hesabu, ni ratio. Ni Gross National Income divided by the population. Kwa hiyo, lazima ulinganishe tu. Hiyo ni hesabu, ni ratio. Ratio ni ratio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hivi, tutafikaje huko na tutabakije huko? Pendekezo langu la kwanza, kama mpango unavyosema, uzito wote tuweke kwenye kilimo. Kwa sababu, kwanza tuna tatizo la ajira, ambalo tutalijibu kupitia kwenye kilimo. Pili, tunahitaji malighafi kwa viwanda vya ndani na vya nje, tutapata kwenye kilimo. Sasa hapo kwenye kilimo tunaendaje? Cha kwanza kabisa, nilimsikia Mheshimiwa Naibu Waziri, alijibu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge na Serikali, mahali pa kuanzia pa kwanza ni suala la mbegu. Hili suala la mbegu ni suala ambalo duniani sasa hivi biashara yake ni bilioni 45 dunia nzima. India inajitahidi katika hizo bilioni 45 inachukua mbili. Kwa hiyo, sisi mahitaji ya mbegu lazima tuyatatue na tutayatatua kwa kuzalisha mbegu zetu na tutayatatua kwa kuwekeza kwenye utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka mingi, walioko kwenye sayansi na mambo ya uchumi ya dunia, tumeona uhusiano mzuri uliopo kati ya ukuaji wa uchumi na utafiti unaofanyika ndani ya nchi hiyo. Haiwezekani, haijawahi kutokea, labda iwe kwa miujiza na miujiza huwa ipo kwamba wewe huwekezi kwenye utafiti, ukaja kuitawala hii dunia, haiwezekani! China na Marekani wanapambana kwa ajili ya utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo, hilo ndiyo pendekezo langu la kwanza kwa upande wa kilimo.

(Hapa kengele ya kwanza ililia)

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Bado nadhani.

MBUNGE FULANI: Bado sana, endelea. MWENYEKITI: Bado dakika tano za mwisho. MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Ooh!
Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha hizo, nimechukua mazao ambayo lazima tuwekeze sana, kwa sababu yanaliwa sana duniani. Tunaweza tukalima kila kitu, lakini tulime mchele ambao zaidi ya asilimia 50 ya watu wote duniani ambao sasa hivi tupo bilioni 7.8 wanatumia mchele kama chakula kikuu (staple food). Cha pili ni ngano, nayo ni zaidi ya asilimia 50; cha tatu ni mahindi. Mahindi ni chakula na kwenye viwanda. Cha nne, nimechagua muhogo kwa sababu una matumizi zaidi ya 100 na unatumika sana viwandani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa pendekezo langu kwa sekta ya kilimo, tuzalishe mazao ambayo wananchi wengi duniani wanayatumia ambayo ni mchele, ngano, mahindi na mihogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha kilimo, kwa ajili ya muda, ninachopendekeza ni nishati. Naenda kwenye fedha nyingi, siyo ndogo ndogo. Nishati ni lazima tuzalishe umeme kutoka vyanzo vingi. Vyanzo vyetu sasa hivi ni maji na makaa ya mawe. Tumejenga transmission lines za 400KV za kupitisha umeme kwenda Kenya mpaka Ethiopia, kwenda Zambia mpaka soko la SADC huko. Zile lines zinaweza kupitisha Megawati 2,000 kwa mpigo, kwenda au kurudi. Kwa hiyo, eneo lingine ambalo litatupatia fedha nyingi…

(Hapa Mhe. Hussein M. Bashe alikatiza katikati ya Mwenyekiti na mchangiaji kinyume na Kanuni za Bunge)

SPIKA: Mheshimiwa Bashe, rudi ulikotoka, umemkatiza Profesa. Endelea Profesa.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, umeme huu tuutoe kwenye maji, tuutoe kwenye gesi na kwenye makaa ya mawe (coal), halafu na renewable (solar, wind, geothermal na kadhalika).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye coal hatuna hata megawatt moja. tulianza mjadala, tukaiambia dunia kwamba sisi hatujachafua mazingira kwa sababu siyo tu per capita, pollution yetu kwa kila mtu ni 0.22 tones per person per annum, huwezi kulinganisha na China na Marekani ambayo ina zaidi ya tani 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, eneo la pili la kutupatia fedha nyingi ni umeme uwe mwingi, bei itashuka nchini, viwanda vitazalisha kwa bei ya chini na vile vile tunataka tuuze umeme nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo naligusia ni LNG (Liquefied Natural Gas). Tuna gesi kule baharini karibu 57TCF. Ni lazima tuharakishe ili tuweze kupata hizo 15 metric tones per annum ambazo tumepanga kuzalisha pale Lindi. Sasa hii LNG itatusaidia sana kuleta fedha nyingi ndani ya nchi. Ukichukua nchi kama Qatar, nimechukua mfano. Qatar haina uchumi mkubwa wa kutegemea mazao, inategemea gesi tu. Yenyewe GDP per capita ya Qatar ni dola 52,000. Ni among the top ten in the world, GDP per capita ya Qatar na wana-depend on gas. Kwa nini sisi gesi yetu isiharakishe huu uchumi na hizi fedha za mipango yetu tunayoifanya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipanga kuzalisha ule wa kuzalisha, yaani two trains, maeneo ya kuzalisha. Qatar wana 14 trains, hatuwezi kushindana nao. Wenzetu Msumbiji sasa hivi wamejipanga watazalisha train moja 13 million metric tones per annum halafu na nyingine itaenda mpaka 43. Tatizo la Msumbiji wakitutangulia ni kwamba wataweka mikataba ya muda mrefu na nchi ambazo sisi tunataka kwenda kuuza gesi. Kwa hiyo, lazima tushindane na Msumbiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nimelileta, nadhani nina muda wangu; nimechukua kwenye fedha nyingi tu. Nilimsikia yule Mheshimiwa Mbunge wa Rukwa akiongea kuhusu gesi ya helium. Sasa hivi duniani, ilikuwa inazalishwa kwa wingi Marekani, kule Texas na Oklahoma, wakaingia nao vita ya kwanza, ya pili inaanza kupungua. Duniani mahitaji ya helium ni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Profesa.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Kwa hiyo,…

MWENYEKITI: Nakushukuru sana.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kusema kwamba hii gesi ambayo tunayo nyingi sana, kwa makisio ya awali ya wale vijana wa Oxford ni kwamba tuna 2.8 billion cubic feet; na sasa hivi Soko la Dunia ni six billion. Kwa hiyo, tunaweza ku-sustain Soko la Dunia kwa miaka kati ya 20 mpaka 30, hatutakuwa na tatizo la kung’ang’ana na uzalishaji mdogo mdogo wa viazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)