Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi, Mwenyezi Mungu akubariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kusimama hapa. Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kwa Bunge hili la Kumi na Mbili, nichukue nafasi hii kuwashukuru wanawake wa Morogoro walionipa kura za kishindo na za heshima yake. Nasema nawashukuru sana akina mama wa Morogoro, nakishukuru sana Chama changu cha Mapinduzi kwa kunileta humu Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru pia Mheshimiwa Rais kwa mambo yote aliyoyafanya. Hotuba zake mbili ni nzuri sana, unaangalia ya kuongelea na kuacha unakosa, unatamani uwe na muda mrefu kusudi uongee kila kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na maji. Serikali imefanya vizuri kwenye maji ingawa siyo vizuri sana lakini imejitahidi. Nawashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri kwa upande wa maji. Mheshimiwa Rais jinsi alivyosema kwenye upande wa maji, naomba kila kitu kilichoongelewa kiweze kutekelezeka, kuna miradi ambayo imekamilika na mengine bado haijakamilika. Wananchi wanaomba na wanataka maji, kwa hiyo, miradi ambayo haijakamilika nashauri iweze kukamilika kusudi wananchi waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa pongezi kubwa kwa hotuba ya Mheshimiwa Rais na jinsi anavyofanya hasa kwa kuchukua kutoka Ziwa Viktoria kuyaleta mpaka Tabora na tunategemea yatakuja mpaka Dodoma, hiyo tunashukuru. Mkoa wangu wa Morogoro una mito mingi lakini mpaka sasa hivi tuna shida ya maji. Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wananisikia muuangalie vizuri sana Mkoa wa Morogoro tuweze kupata maji ya kutosha na miradi ile kichefuchefu iweze kuisha kabisa twende vizuri na nikiwa Mwenyekiti wa Kamati naamini nitakuwa pamoja nanyi bega kwa bega. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa miundombinu, Mheshimiwa Rais ameongelea vizuri sana kwenye ukarabati wa reli ya kati, sasa hivi imekarabatiwa vizuri na ukarabati na ujenzi wa reli ya mwendo kasi. Sisi wananchi wa Morogoro kwa kweli tunafaidika vizuri sana na reli hii ya mwendo kasi. Kinamama, kinababa na vijana wote nawashauri muwe tayari kwa sababu ajira imepanda reli hii ikianza. Ila tunauliza ni lini reli hii itafunguliwa kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro ili wananchi waweze kujiweka vizuri kwa mwendo kasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naweza kuliongelea ni kwenye uchumi. Mheshimiwa Rais amesema kwenye uchumi hasa ataangalia upande wa kilimo, mifugo na maji na hasa mifugo na uvuvi kwani ndiyo sekta zinazoleta ajira kwa wananchi wengi. Kwa upande wa kilimo unakuta asilimia 65.5 wanategemea kilimo na asilimia 100 inazalishwa na wakulima wa vijijini na kila mmoja anategemea chakula kutoka kijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, amesema ataangalia upande wa pembejeo, mbegu na mbolea. Nachoomba kwa Mawaziri wanaohusika ambao tupo pamoja waangalie sana upande wa mbegu. Mpaka sasa hivi hatujitoshelezi kwa upande wa mbegu, kwa hiyo, tuangalie jinsi ya kuzalisha mbegu hasa kwa upande wa taasisi hivi zinazozalisha mbegu pamoja na wananchi waweze kufundishwa na kuelekezwa jinsi ya kuzalisha mbegu tuweze kupata mbegu za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia jambo lingine ambalo naomba kuliongelea ni kuhusu mbegu zetu za asili. Naomba sana tusidharau mbegu zetu za asili tuone jinsi ya kuziboresha kusudi ziweze kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu Maafisa Ugani. Nashukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ameanza kuwaita Maafisa Ugani na kuongea nao. Nashauri Maafisa Ugani wawe karibu na wakulima kusudi waweze kuwapa elimu ya kutosha tuweze kuzalisha kwa wingi. Tukizalisha kwa wingi ndiyo tutaweza kupunguza umaskini na ajira kwa kila mmoja.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili tayari Mheshimiwa.

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nimeongelea kitu kimoja kinatosha na kuwashukuru wanawake wa Morogoro, ahsante sana. (Makofi)