Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Ramadhan Suleiman Ramadhan

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chake Chake

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. RAMADHANI SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia kwenye Hotuba ya Rais ya kufungua Bunge aliyoitoa katika Bunge hili tukufu Novemba pamoja na ile ya kufunga.

Kwa kuwa na mimi ndio mara yangu ya kwanza kuchangia ndani ya Bunge lako hili tukufu, naomba kwa heshima kabisa nitoe shukrani zangu kwa chama changu Chama Cha Mapinduzi kwa imani yake iliyonipa, hasa kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wetu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa utumishi uliotukuka. Pia, nichukue fursa hii kutoa shukrani zangu kwa wananchi wa Chakechake kutokana na support waliyonipa na imani waliyonipa ili nije niwawakilishe katika Bunge hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu ambao nataka niongezee kwenye hii guide book ambayo ni hotuba ya Mheshimiwa Rais ni kwenye suala la utalii. Mheshimiwa Rais vision yake aliyoiweka kwenye guide book hii ya hotuba ni kwamba, anasema ndani ya miaka mitano kutoka 2020 mpaka 2025 anatamani aone watalii wameongezeka Tanzania mpaka kufika milioni tano ambao watachangia kwenye pato la Taifa kwa Dola za Kimarekani bilioni sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ushauri wangu kwa wasaidizi wa Rais ambao wamepewa kazi ya kumsaidia Rais kufikia hayo malengo ya ku-promote utalii Tanzania ni kwamba, ninavyoona mimi ili hili lengo lifikiwe, la watalii milioni tano ambao watachangia zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni sita, moja katika eneo ambalo tunalikosea ni mawasiliano mazuri baina ya taasisi zinazokuza utalii za Tanzania Bara na Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi unahisi inakuwa ni very normal mgeni kutua Zanzibar akatumia zaidi ya siku nane akiwa Zanzibar, katoka ulaya, halafu akaondoka kurudi Ulaya bila kupita Tanzania Bara, hili jambo sio sahihi. Inavyoonekana ni kwamba, hizi taasisi zetu za kukuza utalii au idara za utalii baina ya bara na Zanzibar hazina mawasiliano mazuri. Hakuna juhudi za makusudi zinazochukuliwa baina ya pande mbili hizi kuwasiliana ili kuwashawishi wageni wapate kutumia siku zao wanazokuwa Tanzania kwenye pande zote mbili za Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtalii ameshakuja Zanzibar au yuko Serengeti anatumia siku nane, unaachaje kutumia fursa hiyo kumshawishi mgeni atumie siku mbili za siku nane zake akiwa Serengeti wakati ameshakuja Tanzania? Kwa hivyo ilivyo sasa haiku vizuri sana. Ushauri wangu kwa kaka yangu Waziri wa Utalii, Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, ni kwamba anaweza akatafuta namna ya kuzi-link hizi idara za utalii zilizoko Tanzania Bara na zilizoko Zanzibar ili tuwashawishi wageni wanaokuja Tanzania waweze kutembelea pande zote mbili za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano ni kwamba, mwishoni mwa mwezi Desemba, Wizara ya Utalii ya Tanzania Bara ilipata ugeni wa Bwana Drew Binsky alitoka Marekani. Huyu jamaa ni mtu maarufu sana ambaye ametengeneza makala nyingi za utalii duniani. Ni mtu ambaye kwenye face book page yake ana zaidi ya follower milioni 30, video yake moja aliyoi-post akiwa Moshi imetazamwa na viewers zaidi ya milioni 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kusikitisha hizo fursa watu wameshindwa kuwasiliana baina ya Zanzibar na Tanzania Bara maana yake hata siku moja huyu Drew alishindwa kuwa Zanzibar akapiga picha akiwa Stone Town, ambayo pengine ingeonekana leo na watu zaidi ya milioni 20 duniani watu wangeshawishika kufika Zanzibar nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu, ili tumsaidie Mheshimiwa Rais afike hilo lengo la hao watalii milioni tano tuna haja ya kufanya jitihada za makusudi. Watalii wanakuja kutembelea Zanzibar kwenye fukwe pia tuweze kuwashawishi wawe wanakuja kutembelea kwenye mbuga zetu za Serengeti na nyingine zilizopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo mchango na ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri anapokwenda kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufikisha vision yake ya kukuza pato la Taifa hasa kupitia utalii kwa kukusanya zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 6. Ahsante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. RAMADHANI SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)